Na Mwandishi wetu
Mtu anayesadikiwa kuwa muumini wa kiislam Ahamad Fadhili (63),
amenusurika kuuawa kwa kipigo, akihusishwa na jaribio la kubaka ndani ya
msikiti.
Tukio hilo limetokea katika msikiti wa Mwembe Mmoja uliopo Ujiji,
mkoani Kigoma na kushuhudia na umati wa watu wakiwamo waumini wa msikiti
huo.
Fadhili anadaiwa kujaribu kumbaka msichana wa umri wa miaka 24 (jina tunalihifadhi), anayesumbuliwa pia na ugonjwa wa kifafa.
Vyanzo kadhaa vya NIPASHE Jumamosi katika eneo hilo, vilieleza kuwa
katika tukio hilo la Februari 19, mwaka huu, majira ya saa nane mchana,
Fadhili alikutwa akimbaka msichana huyo ikiwa ni baada ya swala ya
adhuhuri.
Mrekwa Kabichi, muumini katika msikiti huo alisema, baada ya
kuswali, alimuona kiongozi wa msikiti huo, akimtaja kwa jina la Mzee
Sande, akitoka ndani ya msikiti huku akifoka.
“Tukamuuliza, kuna nini mbonaunafoka, kasema nimemkuta Ahamad
Fadhili akimbaka binti ndani ya msikiti wetu, tukamuuliza wako upande
gani akatwambia ni yule ambaye anakimbia,” alisema.
Aliongeza, “tukamkimbiza hadi kumkamata, tukampa kipigo kisha
tukampeleka kituo cha polisi kati ili sheria ichukuwe mkondo wake.”
Imamu wa msikiti huo, Shabani Hashimu Juma, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kusema kuwa kitendo hicho kimeisikitisha jumuiya ya
waislamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba
atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.
NIPASHE Jumamosi ilienda hospitali ya mkoa, Maweni katika wodi namba tano, na kumkuta msichana huyo akiwa amelazwa.
Msichana huyo alisema siku ya tukio, majira ya saa saba mchana, alienda msikitini hapo kuomba msaada, kwa vile anaugua kifafa.
“Nilipofika, nilikutana na huyo baba akaniambia ni kiongozi wa
msikiti, hivyo nimsubiri akanichangie fedha kwa waumini,” alisema.
“Ndipo mimi nikaingia ndani ya msikiti, upande wa wanawake
kuswali, baada ya kumaliza mzee huyo aliniita na kuniingiza ndani ya
eneo jingine nikafikiri naenda kuchukua mchango, kumbe naenda
kubakwa,”aliongeza.
Alidai kuwa mtuhumiwa alimpapasa, na kwamba alijitahidi kukataa,
lakini ‘aliishiwa nguvu’ hivyo kutoa fursa ya kuangushwa chini na
kubakwa.
Kwa mujibu wa msichana, wakati tukio hilo likiendelea, alitokea mzee mwingine (Sande) na kuwatenganisha.
“Alimtoa juu yangu na huyo baba (mtuhumiwa) kuanza kukimbia, ndipo
waumini wa msikiti walimkimbiza na kumkamata na kuanza kumpiga,” alidai.
Alisema wakati huo, alikuwa amezimia na kwamba alipozinduka alijikuta akiwa wodini hapo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Maweni, Yakayashi Macrice,
alithibitisha kupokea mgonjwa aliyebakwa, ikielezwa kwamba tukio hilo
lilitokea msikitini.
Alisema msichana alipata matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
0 Comments