MICHEZO

  Ngassa kiini cha burudani Taifa leo


Mrisho Ngassa
Sosthenes Nyoni

WINGA Mrisho Ngassa wa Simba, leo anatarajia kuwa kiini cha utamu wa mchezo wa soka, pale atakaipoikabili kwa mara ya kwanza timu yake ya zamani, Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Simba, mabingwa wa soka Bara walimsajili Ngassa kutoka kwa washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Azam. Kabla ya kutua Simba, Ngassa alikuwa akiwaniwa na Yanga ya Dar es Salaam.


Mbali na Ngassa, mwingine ambaye leo huenda akawa kivutio, ni Ramadhan Chombo 'Redondo' atakayekuwa na timu yake mpya Simba.


Redondo ambaye usajili wake ulizua utata, alisajiliwa na Simba kutoka Azam FC, ambao nao awali walimsajili kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi.


Pambano la timu hizo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki hii, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


REKODI

Kwa mwaka huu pekee, Simba na Azam zimekutana mara tano katika mechi za mashindano mbalimbali. Hazijawahi kutoka sare, huku Simba ikishinda michezo mitatu na Azam miwili.


Mechi ya karibuni ni ile ya nusu fainali ya michuano ya Super8, ambapo Simba iliyochezesha kikosi 'B' dhidi ya kikosi kamili cha Azam, ilishinda mabao 2-1.


Vikosi:


Kwa kiasi kikubwa Simba itakuwa na mwonekano tofauti kwa vile ina sura kadhaa mpya kutoka ndani na nje ya nchi.


Miongoni mwa nyota wapya mbali na Redondo na Ngassa kwenye jeshi la Simba leo, wengine ni mshambuliaji wake mpya kutoka Ghana, Daniel Akufo na beki raia wa Mali Komanbill Keita na Mkenya, Pascal Ochieng.


Nayo Azam kama ilivyo kwa wenzao wa Simba, inatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo hasa hasa katika mpangilio wa kikosi na hii ikitokana na kutokuwapo kwa Ngassa na  Redondo.


Mfumo:


Wakati Simba itakuwa na kocha mwenye uzoefu na timu hiyo Milovan Cirkovic, Azam itaongozwa na kocha wake mpya Boris Bunjak aliyeukwaa ubosi, baada ya kutimuliwa Mwingereza Stewart Hall.


Timu zote zinatumia mfumo mmoja wa 4-4-2 na hata aina ya soka lao pia linafanana, likipingwa pasi nyingi fupifupi.


Wakizungumzia pambano baina yao, makocha wa timu hizo wakiwa katika hali ya kujiamini walijinasibu kila moja kufanya kweli na kuibuka na ushindi.


"Itakuwa mechi ngumu, lakini ni wakati wa sisi kulipa kisasi baada ya wao kutufunga Kombe la Kagame. Tupo vizuri kiakili na kisaikolojia," alisema Cirkovic.


Naye Bunjak alisema, "Ili ushinde unahitaji maandalizi, na kwa upande wetu tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na kutuongezea morali katika ligi."


Kwa upande mwingine, wachezaji wa kuchungwa zaidi leo ni pamoja na mshambuliaji nyota wa Simba  Mganda Emmanue Okwi,  kama itakavyokuwa kwa mpachika mabao hatari wa Azam John Boko 'Adebayor'.


Rekodi kamili Simba/ Azam mwaka 2012.


Mapinduzi Cup: Azam     2-0 Simba

Ligi Kuu:           Simba     2-0 Azam

Urafiki Cup:      Simba 3 -1 Azam (pen)

Kagame Cup:     Azam   3- 1 Simba

Super 8:            Simba 2- 1 Azam.


 

Wachovu Liverpool wauvaa muziki wa Man City


LONDON, England

MABINGWA wa England, Manchester City kesho watashuka kwenye Uwanja wa Anfield kuwavaa wachovu Liverpool.

Manchester City wataingia uwanjani huku wakiwa na rekodi nzuri ya ushindi wa mabao 3-2 waliopata dhidi Southampton wiki iliyopita ukiwa ni ushindi wa tano katika mechi tano za karibuni.

Wapinzani wao, Liverpool wakiwa mbele ya mashabiki wao watakuwa na jukumu moja la kuhakikisha wanarudisha imani kwa mashabiki wao baada ya kuchapwa 3-0  na West Brom kwenye mchezo uliopita.

Man City

Manchester City inakwenda katika mechi hiyo ikiwa na historia nzuri katika siku za karibuni, lakini timu hizo zilipokutana katika mechi tano za nyuma, Liverpool ilipata ushindi mara mbili, Manchester City mara moja na walitoka sare katika mechi mbili.

Liverpool haitakuwa na beki Daniel Agger, ambaye amefungiwa mechi moja na Machester City itawakosa wachezaji watatu majeruhi ambao ni mshambuliaji Sergio Aguero, kiungo Gareth Barry na beki Micah Richards.

Ukiachilia mbali mechi hiyo, Manchester United ambayo Jumatatu wiki hii ilikaribishwa katika ligi kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka Everton huenda ikazinduka wakati itakapokutana na Fulham leo.

Manchester United iliyosajili Shinji Kagawa na Robin van Persie, ilishindwa kutamba mbele ya Everton.
Baada ya mechi hyo kocha, Alex Ferguson alikiri alifanya makosa kutomwanzisha Van Persie na badala yake nyota huyo aliingia uwanjani dakika 22 kabla ya kipenga cha mwisho.

Hata hivyo, wapinzani wao Fulham wapo katika hali nzuri baada ya kuisambatisha Norwich City mabao 5-0 katika mechi ya fungua dimba.

Nayo Chelsea itakuwa na wakati mgumu itakapoivaa Newcastle leo. Katika mechi ya awali, Chelsea iliifunga Wigan mabao 2-0 na katikati ya wiki hii waliinyuka Reading mabao 4-2.  

Newcastle iliyomaliza msimu uliopita katika nafasi ya tano juu ya Chelsea ilianza ligi kwa kutoa kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tottenham.

Nayo Arsenal iliyoanza ligi kwa suluhu dhidi ya Sunderland, itataka kuzinduka wakati itakapokuwa ugenini kupambana na Stoke City kesho Jumapili wakati Tottenham itakwaaana na West Brom leo.



Rais Kagame aipa tano Yanga

Wachezaji wa Yanga wakishangilia ushindi wa kutwa kombe la Kagame

Doris Maliyaga, Kigali Rwanda

RAIS Paul Kagame wa Rwanda, ameipongeza klabu ya Yanga kwa kutwaa mara ya pili mfululizo Kombe la Kagame na kusema mafanikio hayo yanatokana na umoja na mshikamano ndani ya klabu hiyo.


Kagame, ambaye ni mdhamini mkuu wa mashindano hayo, alikutana wachezaji wa Yanga na viongozi wao katika hafla aliyowaandalia kwa ajili ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu ya Kigali Jumatano usiku wiki hii.


Yanga ilitwaa ubingwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Azam FC 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo mwaka jana ilifanya hivyo pia kwa kuifunga Simba 1-0 kwenye uwanja huohuo.


"Nawapongeza kwa ushindi wenu. Ni jambo zuri na inaonyesha ni jinsi gani mlivyo na umoja wa kweli katika michezo," alisema Kagame ambaye katika hafla hiyo uongozi wa Yanga ulimkabidhi jezi ya timu yao.


"Nataka kuwaambia neno moja, mafanikio mliyopata ni furaha kwa wote kwa maana sisi sote ni ndugu. Yanga ni klabu ya Tanzania na Afrika Mashariki, sisi sote ni wamoja.


"Nawaambieni, leo tunaweza kujiona sisi ni tofauti kwa sababu ya utaifa wetu, lakini akifuatilia chimbuko la wazee wetu wa zamani, utagundua sisi ni wamoja kutokana na mchanganyiko wetu," alifafanua.


"Kuna Watanzania wengi hapa Rwanda, lakini pia kuna Wanyarwanda wengi Tanzania. Hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyo wamoja."


Wakati huohuo, Kocha wa Yanga, Thomas Saintfiet ameahidi kukirudisha kikosi chake mjini Kigali kupiga kambi baada ya kufurahishwa na mazingira ya mji huo.


Yanga imeweka kambi katika Hoteli ya La Pallise iliyopo eneo la Remera kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.


"Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Rwanda, lakini hakika nimefurahishwa na mazingira ya hapa, naahidi nitarudi tena kuweka kambi na timu yangu," alisema Saintfiet mbele ya Rais Kagame.


"Nitafanya hivyo lakini pia huenda nikaleta tena kombe hili kwa mara nyingine kwa maana mazingira ni tulivu na mazuri, kila kitu kinaenda sawa,"alisema Saintifiet.


Post a Comment

0 Comments