Ziwa Tanganyiko
WATU 21 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tanganyika, baada ya
boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama baada ya kupigwa na
mawimbi.
Taarifa za tukio hilo lililotokea juzi usiku
zinaeleza kwamba boti hiyo inayojulikana kwa jina la Yarabi Tunusuru,
ilikuwa imebeba abiria 85, ambapo 64 kati yao waliokolewa.
Katika harakati za uokoaji, miili ya watu tisa
waliokufa maji iliopolewa na watu 12 hawajulikani walipo huku hofu
ikitanda kuwa wamefariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema ilitokana na uzembe wa
kiongozi wa boti, kutosikia malalamiko ya abiria.
Nahodha wa boti hiyo, Akilimali Seif, alisema kuwa
walianzia safari yao katika Kijiji cha Kipili mkoani Rukwa, Jumatano
iliyopita, kuelekea Mji wa Uvira uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC).
Alisema kuwa ikiwa njiani, boti hiyo ilikuwa
ipitie mji wa Rumonge nchini Burundi, ambako ingeshusha sehemu ya mzigo
iliyobeba ambayo idadi kubwa ilikuwa ni chakula.
“Tulianza safari salama tukienda Uvira, DRC
kupitia Burundi katika mji wa Rumonge, kupeleka mizigo ya
wafanyabiashara. Lakini, hali ilianza kubadilika juzi (Alhamisi),”
alisema nahodha huyo na kuongeza:
“Saa nane mchana tukiwa Kijiji cha Kalilani
(kilichopo jirani kabisa na Hifadhi ya Taifa ya Mahale), mvua kubwa
ilinyesha na mawimbi yakawa makubwa. Kwa kweli siamini kama baadhi yetu
tumeokoka.”
Alifafanua: “Kilichosababisha boti yetu ipasuke ni
ubishi wa aliyekodi; … Licha ya abiria kumlalamikia wakitaka aegeshe
boti ufukweni, yeye alikataa na kulazimisha tuendelee na safari. Matokeo
yake mawimbi yakazidi, hadi ilipofika saa nne na nusu usiku injini ya
boti ilizimika, ndipo maji yakawa yakiingia.”
Seif aliendelea kuhadithia kuwa maji yaliendelea kutanda kwenye boti na muda mfupi baadaye ilipasuka na kuzama.
Alisema kwamba kabla ya kupasuka, boti hiyo
ilikuwa ikisukumwa na mawimbi kuelekea eneo la ufukweni mwa ziwa, ambapo
abiria walianza kuweweseka na kila mmoja akawa anatafuta cha kumwokoa.
Kwa mujibu wa Seif, wachache walibahatika kuvaa
majaketi ya uokoaji yaliyokuwapo na wengine ilibidi wajaribu kutumia
mapipa ya mafuta, matenga ya samaki na magunia ya mihogo.
0 Comments