Tibaijuka azua tafrani Kigamboni

  Madiwani kuitisha kikao kumpinga

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka

 Na Moshi Lusonzo

 Tangazo la Serikali kulichukua eneo lote la Kigamboni na kuliondoa chini ya mamlaka ya Manispaa ya Temeke, limezua tafrani baada ya madiwani kutaka kuitisha kikao maalum cha kupinga hatua hiyo.


Katika kutimiza azma yao hiyo, wameanza kukusanya saini za madiwani wanaofikia nusu na robo ili kiitishwe kikao walichokiita kuinusuru Temeke.


Hivi karibuni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alitangaza kulitwaa eneo la Kigamboni na kuongeza ukubwa wa eneo kwa kuchukua kata zingine kwa ajili ya uanzishwaji wa jiji la kisasa la Kigamboni.


Katika hatua hiyo, Profesa Tibaijuka alitangaza kuanzishwa kwa chombo cha Wakala wa Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA) ambapo hatua hiyo inaiondoa kutoka Manispaa ya Temeke kiutawala.


Madiwani hasa kutoka Kigamboni wameliambia gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao kuwa kuondolewa kwa kata zao kuwa chini ya Manispaa ya Temeke imewafanya kutojua hatma yao pamoja na wananchi kukosa sehemu ya kukimbilia.


Walisema kitendo cha Serikali kuwaondoa kibabe bila kuwashirikisha kimezidisha hofu kwa wananchi wa eneo hilo ambao tangu mradi huo uanze kuandaliwa, wamerudishwa nyuma kimaendeleo.


Mmoja wa madiwani hao alisema wameanzisha zoezi maalum la kukusanya saini za madiwani kwa ajili ya kuomba kuitishwe kikao cha dharura cha madiwani kwa ajili ya kujadili kauli ya Waziri huyo.


"Tumeshtushwa sana na kauli ya waziri Profesa Tibaijuka, ni hatua ya kibabe iliyochukuliwa bila kutushirikisha sisi madiwani, haiwezekani kutuondoa manispaa ya Temeke bila kufuata utaratibu wa kisheria," alisema diwani huyo.


Alisema kitu cha kushangaza, Serikali imeongeza kata zingine nne na kuziingiza kwenye mradi bila kutoa taarifa kwa wananchi ili waweze kujadili na kutoa maoni yao.


Kata zilizoingizwa kwenye mradi huo ni Kisarawe 11, Kimbiji, Somangila na Pembamnazi, ambapo kata zilizokuwa awali ni Kigamboni, Tungi, Kibada, Mjimwema na Vijibweni.


"Tutalazimika kukutana haraka kuona jinsi gani tutaijibu serikali kwa maamuzi yake haya ya ukandamizaji, sisi ni wawakilishi wa wananchi kwa nini wanafanya mambo yao kwa usiri mkubwa na kisha kutupa taarifa kama vile huku hakuna mamlaka inayokubalika," aliongeza kusema Diwani mwingine.


Imeelezwa mpaka jana tayari saini za madiwani zilikuwa zimepita nusu ya idadi inayotakiwa na hivyo wakati wowote kuna uwezekano wa kuitishwa kwa kikao hicho.

Madiwani hao wamepingana na kauli ya Waziri huyo kwamba wataingia katika Baraza la Ushauri la KDA kwa sababu mpaka jana hakukuwa na taarifa zozote za kikao.


Awali Profesa Tibaijuka alisema kutokana na kuanzishwa kwa KDA, kata zote za Kigamboni, zitaungana na madiwani wake na mbunge wao watakuwa wakikutana katika Baraza la Ushauri la KDA.


Alisema wananchi wa Kigamboni ambao wako kwenye maeneo ambayo yatahitajika kwa ajili ya ujenzi huo watashirikishwa ipasavyo katika mchakato mzima ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia zao kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments