Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha, kimefanya
maadhimisho ya miaka miwili kukumbuka mauaji yaliyofanywa na polisi kwa
wafuasi wa chama hicho huku kikisema kitaendelea kuwa imara kusimamia
haki ili taifa lisiharibike.
Katika maandamano yaliyofanywa Januari 5,
2011 na wanachama wa Chadema pamoja na wafuasi wao, inadaiwa kuwa
polisi walitumia nguvu kubwa ikiwemo silaha za moto kuyazuia hatua
ambayo iliwafanya watu zaidi ya 36 kujeruhiwa na kulazwa Hospitali ya
Mkoa ya Mount Meru.
Purukushani hizo zilisababisha watu watatu
Ismail Omary, Denis Shirima na raia mmoja kutoka Kenya aliyekuwa
safarini mjini hapa kuuawa baada ya kupigwa risasi na polisi.
Maandamano hayo yalikuwa mahususi kupinga
kile walichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilifanya hila, njama na
ghilba kupindisha sheria na kumwingiza Gaudence Lyimo kuwa meya wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika maadhimisho hayo ambayo
yalitanguliwa na shughuli ya kutembelea vituo vya watoto yatima na
kuwapatia chakula na vitu mbalimbali kama sadaka, yalihitimishwa kwa
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi
Ngarenaro.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa
Jimbo la Arusha, Godbless Lema, alisema anashangaa kuona mtu anayejiita
meya akiwa bado anatambea na serikali bado inamlinda.
“Haiwezekani, kuna watu wamekufa,
wamejeruhiwa, wapo watoto yatima, wajane wameachwa kwa sababu ya sakata
la umeya, halafu atokee mtu au kikundi cha watu atutake tumalize suala
hilo,” alisema. Alisema atashangaa kama meya Lyimo atafanikiwa kuongoza
kikao kimoja cha Baraza la Madiwani na yeye akiwamo ndani, basi yeye
(Lema) atakuwa mbwa. Alisema madiwani wa Chadema watahudhuria vikao vya
madiwani ambapo pamoja na mambo mengine watakuwa wanapinga masuala
yatakayokuwa yakizungumzwa humo kama yale ya kuwahamisha wafanyabiashara
ndongo ndogo wakiwamo vijana na akina mama.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa,
Amani Golugwa akimkaribisha Lema kuzungumza na wananchi, alisema
wataendelea kuwa imara kusimamia haki bila kuchoka ili taifa lisije
likaharibika.
Alisema msingi wa kazi yao kama chama ni kusimamia haki na kuona kwamba inatawala.
0 Comments