Maelfu ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya msanii
Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia
wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa
kaburini.
MAELFU ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya
msanii Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia
wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa
kaburini.
Mwili wa msanii huyo ulizikwa jana kijijini
kwake Lusanga wilayani Muheza saa 7 mchana, katika tukio
lililomshirikisha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye
alimwakilisha mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Waombolezaji walianza kumiminika kijijini
Lusanga tangu juzi jioni na idadi yao iliongezeka zaidi jana asubuhi.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa
Kamati ya Mazishi.Sala ya mazishi iliongozwa na Sheikh Twaha Juma ambaye
baadaye aliamuru jeneza hilo kupelekwa makaburini, ambako waombolezaji
kadhaa walipoteza fahamu.
20 wapelekwa hospitali
Miongoni mwa
matukio yaliyojitokeza katika msiba huo ni baadhi ya waombolezaji
kupoteza fahamu msibani.Matukio tofauti ya watu kuzirai yalitokea wakati
mwili wa msanii huyo ulipokuwa unapelekwa nyumbani kwao kijijini
Lusanga ukitokea Hospitali Teule ya Wilaya ambako ulihifadhiwa tangu
alipopata ajali Jumatatu usiku na wakati wa mazishi.
Miongoni mwa waliopoteza fahamu katika msiba
huo ni wasanii na waigizaji wa filamu waliokuwa wakiigiza na Sharo
Milionea wakati akiwa katika kundi la AL Riyam.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na MC wa shughuli hiyo, Steve Nyerere, zaidi ya watu 20
walipoteza fahamu katika msiba huo na kupelekwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Muheza.
DC Mgalu aliwaomba waombolezaji kutokuwa na
shaka juu ya waliopoteza fahamu kwa kuwa madaktari maalumu walikuwa
wameandaliwa hospitalini hapo kwa ajili ya kuwapa huduma.
Mwananchi
lilifika katika hospitali Teule na kukuta waliokuwa wamepoteza fahamu,
wengi wao wakiwa ni wasichana, wakipata huduma huku wengine wakiomba
kupewa ruhusa ili wakahudhurie maziko.
JK atuma rambirambi
Rais Jakaya Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,
Dk Fenella Mukangara kutokana na vifo vya wasanii watatu vilivyotokea
hivi karibuni, kikiwamo cha Sharo Milionea.
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete
ameshtushwa na vifo hivyo vya ghafla.
Wasanii hao ambao walifariki
dunia katika mazingira tofauti ni Mwigizaji wa Kundi la Kaole, Khalid
Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia hivi karibuni kutokana na maradhi
yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
Msanii mwingine ni mwigizaji wa filamu, John
Maganga aliyefariki Novemba 24, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Nimeshtushwa na
kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya wasanii hawa ambao kwa
hakika mchango wao mkubwa katika tasnia ya muziki na maigizo hapa nchini
ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi,” ilisema taarifa
hiyo ya Ikulu.
Vile vile, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma
alituma salamu za rambirambi zilizosomwa na DC Mgalu, kuwa ameguswa na
msiba huo na kuwataka ndugu wa marehemu na wasanii wengine kuwa na moyo
wa subira katika kipindi hiki kigumu.
Kwa mujibu wa Mgalu, Mama Salma alituma salamu hizo akiwa Mwenyekiti wa Mfuko wa Wanawake na Maendeleo (WAMA).
“Mke wa Rais kama mnavyojua ni mama wa
Watanzania wote na ni mama wa wasanii, hivyo msiba huu wa Sharo Milionea
umemgusa sana na ameitaka familia ya marehemu kuwa na moyo wa subira
katika kipindi hiki cha majonzi,” alisema Mgalu.
Wenye sare za CCM
wazomewa
Katika
msiba huo watu waliokuwa wamevalia sare za CCM walijikuta katika wakati
mgumu baada ya kuzomewa na waombolezaji ambao walisema hakukuwa na haja
ya kujitambulisha kiitikadi katika msiba huo.
Kundi la vijana waliokuwa kando ya barabara
ielekeayo kitongoji cha Jibandeni, nyumbani kwa mama mzazi wa marehemu,
waliwazomea watu hao huku wakisema kuwa huo haukuwa msiba wa CCM bali ni
wa wasanii wa filamu.
Vijana hao walieleza kushangazwa kwao na
kitendo cha makada hao kuvaa sare katika msiba huo wakati kiongozi wao
ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwasili
msibani hapo akiwa amevaa nguo za kawaida.
0 Comments