Rais Jakaya Kikwete ameanza rasmi ziara ya kikazi nchini Marekani na ya kiserikali nchini Canada.
Rais Kikwete na ujumbe wake aliondoka nchini juzi na aliwasili katika jiji la New York, Marekani jana, tayari kwa ziara hizo.
Atakuwa Marekani kwa siku mbili kabla ya kwenda Canada kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili.
Katika ziara yake mjini New York, Rais Kikwete leo atakutana na kufanya
mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ofisini kwa
Katibu Mkuu huyo wa UN.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete ataungana na Ban Ki Moon, Meya wa
Jiji la New York na mfadhili mkubwa wa misaada ya kibinadamu duniani,
Michael Bloomberg; Mama Helen Agerup ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya
Misaada ya Kibinadamu ya H&B Agerup na Dk. Kelly Henning, Mkurugenzi
wa Mipango ya Sekta ya Afya ya Taasisi ya Bloomberg Philanthropies
kwenye uzinduzi wa matokeo ya Mpango wa Ubunifu wa Afya ya Akinamama
Tanzania.
Kwenye sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Green kwenye
makao makuu ya UN, Rais Kikwete, Ban Ki Moon, Bloomberg na mama Helen
Agerup kwa pamoja watazindua matokeo ya mpango huu uitwao Innovative
Maternal Health Program.
Kwenye shughuli hiyo pia Meya Bloomberg atatangaza matokeo ya miaka
mitatu ya misaada ya kiafya chini ya mpango huo kwa akinamama
iliyotolewa na taasisi ya inayomilikiwa na Meya Bloomberg ya Bloomberg
Philanthropies.
Aidha, kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg pia atatangaza msaada mpya
wa mabilioni ya fedha kuboresha afya ya akinamama Tanzania chini ya
mpango huo na atatangaza mshirika mpya ambaye atasaidiana na taasisi ya
Bloomberg Philanthropies katika kuunga mkono huduma bora za afya kwa
akinamama wa Tanzania.
Misaada ya taasisi ya Bloomberg Philanthropies huelekezwa katika maeneo
ya vijijini yasiyokuwa na huduma bora zaidi za kiafya na huduma ambazo
hutolewa ni zile za kuokoa maisha ya akina mama hasa wakati wa uzazi.
0 Comments