Harusi ya Consaliva Kudaga (33), imegeuka kilio na simanzi baada ya
mtarajiwa huyo kupata ajali na kufariki dunia eneo la Ngiloli, Gairo
mkoani Morogoro, siku moja kabla ya harusi.
Consaliva alikufa peke yake katika ajali
hiyo, iliyohusisha pia wapambe wake wakati wakisafiri kuja Dar es
Salaam kutoka Mwanza kusherehekea harusi yake ilikuwa ifungwe jana
mchana.
Wakiwa ndani ya gari aina Coaster yenye
namba T 146 CDG iliyokuwa inaendeshwa na Ahmed Rashid waligongana na
lori aina ya Isuzu lenye namba B 3839 ikiendeshwa na raia wa Burundi
Juma Galungu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo kwenye
barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.
Alisema ilitokea juzi jioni baada ya
isuzu hiyo mali ya Nduwaye Erick raia wa Burundi lililokuwa likitokea
Dar es Salaam kuelekea Burundi, kugongana uso kwa uso.
Marehemu Consaliva wakati wa uhai wake alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kanilo iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Baadhi ya mashuhuda walisema biharusi huyo
alikuwa kwenye gari hiyo ya kukodi alikuwa ameambatana na walimu
wenzake, ndugu na marafiki kwa ajili ya ndoa yake iliyotarajiwa kufungwa
jana jijini.
Aidha NIPASHE Jumapili ilitaarifiwa kuwa gari la bibi harusi lilikuwa na abiria 29 walikuwa wakimsindikiza.
Akizungumzia zaidi mkasa huo Shilogile
alisema katika ajali hiyo mbali ya kifo hicho abiria wengine
21walijeruhiwa wakiwamo madereva wa magari hayo. Mwili wa marehemu huyo
umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Serikali ya
Dodoma.
Alisema dereva Galungu ambaye gari yake
ndiyo lilikuwa chanzo cha ajali hiyo kutokana na kuwa kwenye mwendo wa
kasi hali yake ni mbaya na kwamba alikimbizwa katika hospitali ya mkoa
wa Dodoma wakati mwenzake amevunjika miguu.
Kamanda Shilogile alisema kati ya majeruhi
hao, 11 walitibiwa na kuruhusiwa wakati wengine wanatibiwa katika
hospitali za: Taifa ya Muhimbili, Berega Misheni na ya Mkoa wa
Morogoro.
0 Comments