Wanaharakati waandamana kupinga mauaji ya Mwangosi na kufungiwa kwa Mwanahalisi
Baadhi ya wanaharakati wakiwa wamebeba mabango ya jumbe mbalimbali kupinga mauaji ya Mwangosi
Baadhi ya wanaharakati wakiwa katika Kongamano la kupinga mauaji ya Mwangosi kwenye viwanja vya TGNP
Markos Albania (aliyesimama mwenye kipaza sauti) akizungumza na wanakongamano hilo.
UMOJA wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania
(UTPC) unakamilisha taratibu za kuanzisha Mfuko wa Mwangosi (Mwangosi
Foundation) ambao licha ya kuwa na majukumu ya kuisaidia familia ya Daud
Mwangosi aliyeuwawa akitekeleza majukumu yake hivi karibuni mkoani
Iringa, utakuwa na kazi ya kuwasaidia wanahabari wengine ambao watapatwa
na matatizo kama yaliompata Mwangosi.
Taarifa ya kuanzishwa kwa mfuko huo huo umetolewa leo jijini Dar es
Salaam katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) na Makamu wa
Rais wa UTPC, Jane Mihanji alipokuwa akielezea mazingira ya kuuwawa kwa
Mwangosi katika Kongamano la Wanaharakati waliokutana kupinga vitendo
vya mauaji anuai yanayofanywa na Jeshi la Polisi wanapokuwa wakitekeleza
majukumu yao.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC),
Ayoub Rioba (kulia) akiwa meza kuu ya Mkutano wa Kongamano hilo pamoja
na viongozi wengine.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (wa kwanza kushoto)
akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF), Nevilli Meena. Kulia ni Mkurugenzi wa Gazeti la Mwana Halisi,
Sued Kubenea (mwenye miwani).
Mihanji alisema tukio la mauaji ya Mwangosi ambalo limefanywa kinyama
litaendelea kulaaniwa na kuwa chachu ya mabadiliko na utendaji wa nguvu
wa wanahabari katika kazi zao. “Mwangosi Foundation mbali na kusaidia
familia ya mwanahabari huyo utakuwa na kazi ya kuwasaidia waandishi
wengine wanapokuwa katika matatizo yanayofanana na hayo,” alisema
Mihanji ambaye pia ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi kutoka Gazeti la
Uhuru.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Tanzania
Tunayoitaka, Markos Albania alisema hali ya nchi kwa sasa ni tete
kutokana na taarifa za mauaji ya mara kwa mara yanayotokea bila hatua
stahiki ya kuthibiti kufanywa.
Alisema ni hatari hali kama hiyo kuachwa iendelee kwani sasa imefikia
hatua hata wanahabari wanauwawa wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao,
hivyo kuitaka Serikali kuhakikisha inasimamia sheria ili wanaohusika na
mauaji ya Mwangosi wachukuliwe hatua inayostahiki.
“Ukimuua mwandishi umeuwa vyombo vya habari…ukiona Serikali inauwa
wanahabari ujue ni Serikali mfu,” alisema mwanaharakati huyo. Aidha
aliwataka Watanzania wote kuhakikisha wanasimamia na kupata Katiba Mpya
na sio iliyopo sasa kwani imeshindwa kuwawajibisha baadhi ya viongozi wa
Serikali wanaokwenda kinyume,” alisema Albania.
1 Comments
Betway Casino Bonus Code is MAXBONUS | ᐈ 30 Free Spins
ReplyDeleteCasino Review, Bonuses, FAQ & More! gri-go.com New players welcome bonus $10 no deposit aprcasino bonus + 100% up to $1000 in 스포츠 토토 사이트 Betway febcasino.com Casino Bonuses! casinosites.one