Maafa tena Rufiji


Meneja Mwandamizi wa Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Moi,Jumaa Almasi.


Na Waandishi wetu

Pepo  la ajali limezidi kuing’ang’ania wilaya ya Rufiji mkoani Pwani baada ya watu wanane kuhofiwa kufa maji, zikiwa zimepita saa 22 tangu magari mawili aina ya Mitsubishi Canter na Toyota Hiace kugongana Jumamosi usiku na kusababisha vifo vya watu 21 na kujeruhi tisa.

Mbali na watu wanane kuhofiwa kufa maji, pia wengine wanane wameripotiwa kujeruhiwa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kugonga pantoni iliyokuwa imesimama katika Mto Rufiji, eneo la kata ya Utete, wilayani humo na kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili saa 12 jioni, mtumbwi huo ukitokea eneo la Mkongo kwenda Utete.

Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu, pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Uirich Matei, wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Babu, mtumbwi huo ulikuwa ukiwavusha wakulima waliokuwa wakitoka kulima mashamba yao katika kata ya Utete.

Alisema mtumbwi huo uliigonga kwa nyuma pantoni hiyo iliyokuwa imesimama  katika maegesho yake baada ya maji kumzidi nguvu nahodha na kuyumba na kupoteza mwelekeo kisha kupinduka.

 Babu alisema baada ya mtumbwi huo kupinduka, kati ya abiria 16 waliokuwamo, wanane wanahofiwa kufariki dunia, huku wengine wanane wakiokolewa.

Aliwataja wanaohofiwa kufariki dunia kuwa ni Prisca Kulwa (20), Diana Kulwa (14) Husna Mussa (13), Zambina Mussa (8) Uwesu Mbonde (7) Zaria Mbonde (14) na Ratifa Kibega (16).

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni nahodha wa mtumbwi huo, Abdallah Yusuph (21), Ramadhani Mkono (22), Nasra Magimba, Pili Hungwa, Shabani Mbonde, Ramadhani Gido, Karim Salemu na Khalid Mbonde.

Babu alisema baada ya kuokolewa, majeruhi walipelekwa katika Hospitali ya Utete kwa matibabu na kwamba baadaye waliruhusiwa baada ya hali zao kuendelea vizuri.

Alisema nahodha wa mtumbwi huo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Utete kwa mahojiano zaidi.

Kwa mujibu wa Babu, hadi kufikia jana mwili wa mtu mmoja ulikuwa umepatikana katika eneo la kivuko cha zamani na kwamba juhudi za kutafuta watu wengine zinaendelea kwa kutumia boti.

Aliwaomba wakulima wanaokwenda kulima kandokando ya mto huo katika kipindi hiki cha mvua kuwa makini kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya.

Hata hivyo, alisema serikali imejipanga kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kuwavusha watu kwa kutumia vyombo salama.

Wakati Babu akisema hayo, Mwenyekiti wa Mji Mdogo wa Utete, Masudi Ali Jaha, alisema kati ya watu 16 waliokuwamo kwenye mtumbwi huo, waliookolewa ni watano na kwamba, wanaoendelea kutafutwa ni 10, wakati mwili wa mtu mmoja ukiwa umeopolewa.

Alisema hadi kufikia jana, familia nne zilijitokeza na kusema kuwa zimepotelewa na watoto.

Masudi alisema kati ya familia hizo, moja ilidai kuwa imepotelewa na watoto watatu, nyingine mbili, watoto wawili kila moja na familia moja ilidai kupotelewa na mtoto mmoja.

Alisema mwili wa mtu aliyeopolewa ni Zarubiya Mussa Lwambo, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka minane hadi tisa.

Naye Kamanda Uirich alisema watu waliookolewa wamepelekwa katika Hospitali ya Utete na kwamba nahodha wa mtumbwi huyo anashikiliwa na polisi.

MAJERUHI WAENDELEA VIZURI MOI
Katika hatua nyingine, majeruhi wa ajali iliyotokea usiku wa juzi Ikwiriri, Rufiji, mkoani humo wanaendelea na matibabu kwenye Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Fahamu (Moi).

Meneja Mwandamizi wa Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alisema jana kuwa Mniko Magigo (53), ambaye ni mmoja wa majeruhi hao, anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu na kuwekewa vyuma.

Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Mohamed Mengine, (44), Anthony Jonathan, pamoja na Abdallah Issa, ambaye amekwisha kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo baada ya matibabu.

Aidha, majeruhi Charles Rogatian, ambaye amelazwa Hosptali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwenye wadi namba 11 Kibasila aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa tumbo, hali yake haijawa nzuri, lakini amekwishapata fahamu na kwamba, anaweza kuongea, lakini kwa taabu.

CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

0 Comments