ASKARI watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) wamekufa maji kwenye mji wa Darfur, Kusini mwa Sudan wakiwa
katika Operesheni ya Kulinda amani katika nchi hiyo. Msemaji wa JWTZ,
Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi wakati
askari hao pamoja na wengine wakiwa kwenye doria ya kawaida mchana
ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kawaida wakiwa nchi humo. Alisema
katika doria hiyo, walitakiwa kuvuka Mto Malawasha ulioko katika Kijiji
cha Ahamada kuelekea maeneo jirani kabla ya kukutwa na ajali hiyo.
Mgawe
aliwataja waliokufa kuwa Sajini Taji Julius Chacha na Private Anthony
Daniel ambao wote wanatoka Kikosi Jeshi 34 kilichopo Lugalo, Dar es
Salaam. Mwingine aliyefariki ambaye hata hivyo maiti yake bado
haijatikana, ni Koplo Yusuph Said kutoka Shule ya Mafunzo ya Infantilia,
Arusha.
“Ni kweli askari watatu, wamefariki Dunia, waliondoka
wiki iliyopita kuelekea Jimbo la Darfur, Sudan kulinda amani, walikuwa
kwenye operesheni ya kawaida ambayo inaratibiwa na Umoja wa Mataifa
(UN), hivyo basi wakiwa nchini humo, askari hao wanakuwa chini ya Umoja
huo,” alisema Mgawe.
Aliongeza, hii ni bataliani ya sita ya
kulinda amani nchini humo, ambapo batariani zote zilizowahi kwenda
zimerudi salama, hivyo basi ni ajali ya kawaida kama zilivyo ajali
nyingine, na kwamba kila jambo linapangwa na Mungu, hawana budi
kumshukuru.
Kwa mujibu wa mgawe, wakati tukio hilo linatokea,
marehemu hao pamoja na wengine jumla yao wakiwa zaidi ya watano,
walikuwa katika gari aina ya Deraya ambalo linafanya kazi ya doria,
walipofika kwenye mto huo, walikuta kina cha maji kimepungua, jambo
ambalo likawafanya waamini kuwa, maji yao ni kidogo na kwamba wanaweza
kuvuka kama kawaida.
Alisema, kutokana na hali hiyo, mmoja wao
alishuka na kutembea ndani na maji hayo kwa ajili ya kupima kina,
alivuka salama na kurudi kwenye gari hilo ili aweze kuwaruhusu wenzake
kuvuka. Alisema walipojaribu kuvuka tena kwa mara nyingine, ndipo maji
hayo yalijaa ghalfa na kusababisha gari hilo kupinduka, jambo ambalo
lilisababisha kila mmoja kutafuta njia ya kujiokoa.
Katika ajali hiyo baadhi walinusurika, lakini hao watatu walifariki dunia wakiwa kwenye harakati za kujiokoa.
Utaratibu
za kusafirisha miili ya wapiganaji hao, utajulikana hivi karibuni baada
ya kupatikana kwa maiti moja ambayo haijulikani ilipo, huku wakifanya
mazungumzo na Umoja wa mataifa(UN) ambao ndio wenye jukumu la kuratibu
safari za kulinda amani Duniani.
“Askari wote wanaokwenda
kulinda amani wanaingia mkataba na Umoja wa Mataifa(UN), hivyo basi kwa
sasa tupo kwenye mazungumzo ili tuweze kujua maiti hizo zitarudishwa
lini na kwa utaratibu gani, wakati askari wetu wakiendelea kutafuta
maiti iliyopotea,” aliongeza. Alisema kutokana na hali hiyo
wanawasiliana na ndugu zna jamaa za marehemu hao ili waweze kujua
utaratibu wa mazishi pindi maiti hizo zitakapowasili nchini. mwisho
0 Comments