Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
WALIMU wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Ruaruke wilayani Rufiji,
Mkoa wa Pwani, wameitelekeza shule hiyo kutokana na kukithiri kwa
vitendo vya baadhi ya wanafunzi kuwadhalilisha kimapenzi, ikiwamo
kuwabaka baadhi yao.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza
kuwa mbali na udhalilishaji huo, wanafunzi hao wamekuwa wakiwatishia
maisha walimu wao kwa namna mbalimbali. Katika moja ya vitisho hivyo,
wamechoma moto nyumba zao tatu.
Habari hizo zimeeleza kwamba walimu hao
wamelazimika kuikimbia shule hiyo baada ya baadhi ya walimu wa kike
kutongozwa na wanafunzi, kupigwa mabusu kwa nguvu hadharani, kutishiwa
kuchomwa visu na kuchorwa vikatuni vya kudhalilisha.
Mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka kutajwa
gazetini akihofia kushughulikiwa na wanafunzi hao alisema amelazimika
kuikimbia pamoja na walimu wenzake wote, kwa kuwa wameshindwa kudhibiti
tabia hiyo kutokana na vijana hao kuungwa mkono na wazazi wao.
Akizungumza kwa simu akiwa Dar es Salaam,
mwalimu huyo alisema shule hiyo yenye wanafunzi 485, imepoteza mwelekeo,
haitawaliki na mazingira yake hayavutii walimu, hasa wa kike, kuishi na
kufanya kazi.
“Tumevumilia vya kutosha, lakini kila kukicha
hali inazidi kuwa mbaya. Walimu wanafikia mahala wanabakwa! Kibaya zaidi
wazazi na mamlaka nyingine hazionyeshi ushirikiano kwetu, wazazi
wanawa-support (wanawaunga mkono) watoto wao,” alieleza.
Hata hivyo,
mwalimu huyo hakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu vitendo hivyo vya
ubakaji lakini alieleza kwamba vimekuwa vikitokea walimu hao wanapokuwa
katika matembezi usiku.
Vitendo hivyo vimekuwa vikitokea baada ya wanafunzi hao kuwatongoza walimu wao na kukataa kufanya nao mapenzi.
Mwalimu huyo alidai kuwa walimu wamekuwa
wakitishiwa kuchomwa visu na nyumba zao kuchomwa moto, huku walimu wanne
wa kike wakidhalilishwa kimapenzi kwa kupigwa mabusu na kutongozwa na
wanafunzi.
“Wanafunzi wamefanya mtihani wa kidato cha pili chini ya
ulinzi wa askari polisi wenye silaha kitu ambacho si cha kawaida,”
aliongeza.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ofisa Elimu Sekondari,
Adnan Mwenda alisema asingependa kuzungumzia tatizo hilo kwa kuwa siyo
msemaji. Akashauri atafutwe mkurugenzi wa wilaya… “Unaweza kuzungumza
mambo mengine yakakuletea matatizo,” alisema Mwenda kabla ya kuelekeza
atafutwe mkurugenzi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rufiji, Leonard Rwegasira alithibitisha walimu hao kuikimbia
shule hiyo na kusema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya,
itakutana hivi karibuni kujadili suala hilo.
“Ni kweli shule hiyo
imetelekezwa, walimu wamekimbia na wanafunzi hawaendi shule. Tatizo
tunalifahamu na Mkuu wa Wilaya anafanya jitihada mbalimbali kurekebisha
tatizo hilo,’ alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruaruke, Hemedi
Mpullu pia alithibitisha walimu hao kuitelekeza shule hiyo na kusema
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu ameagiza kufanyika kwa kikao cha
dharura ili kupatikana mwafaka kati ya walimu hao, wanafunzi na wazazi.
“Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa amepanga pia kufanya mkutano hapa Ruaruke ili kutafuta mwafaka,” alisema Mpullu.
Katibu
wa Chama Cha Walimu (CWT), Wilaya ya Rufiji, Manyama Lazaro alisema
kuondoka kwa walimu hao, kumefanya shule hiyo ijifunge yenyewe, kwani
wanafunzi nao sasa hawaendi shule.
“Wanafunzi wamefikia hatua ya kuwachora walimu
wa kike wakifanya mapenzi na walimu wa kiume katika kuta za vyoo! Huu
ni udhalilishaji mkubwa,” alisema.
Lazaro alieleza kuwa katika siku
za hivi karibuni, wanafunzi hao walichoma moto nyumba tatu za walimu na
Bodi ya Shule iliamua kuwa wanafunzi hao waitwe na wazazi wao ili walipe
gharama za uharibifu.
0 Comments