Gari aliyokuwa akiendesha Marehemu Sharomilionea baada ya kuacha njia na kupinduka
Na Raisa Said na Burhan Yakub, Tanga
inShare
JESHI la Polisi mkoani Tanga limefanikiwa
kukamata vitu mbalimbali vya marehemu Hussein Ramadhan, ‘Sharo Milionea’
vilivyoibwa na watu wasiojulikana, muda mfupi baada ya msanii huyo wa
filamu na muziki nchini kupata ajali katika Kijiji cha Songa Kibaoni,
wilayani Muheza na kufariki dunia papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda
wa Polisi mkoani Tanga, Costantine Massawe alisema Jeshi la Polisi
limefanikiwa kukamata begi la nguo, simu ya mkononi aina ya blackberry,
betri ya gari, redio, tairi la gari na saa ya mkononi ya marehemu.
Alitaja vitu vingine vilivyopatikana kuwa ni nguo
ambazo marehemu alivuliwa baada ya kupata ajali, ambazo ni fulana na
suruali ya jeans.
Alisema kuwa,vitu hivyo vilipatikana baada ya
wakazi wa kijiji ilipotokea ajali hiyo kuvisalimisha vitu hivyo kwa
Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa kibaoni, Abdi Zawadi .
“Vitu viliwasilishwa na wasamaria wema kwa
Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa Kibaoni, Abdi Zawadi ambaye alitoa
taarifa polisi kwa ajili ya utambuzi na taratibu nyingine,” alisema
Massawe.
Aliwataka wananchi wa Kibaoni kuendelea kutoa
ushirikiano ili viweze kupatikana vitu vingine vya marehemu na kuongeza
kuwa, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, ili kubaini pesa na vitu
vingine vilivyokuwamo ndani ya gari hilo ambavyo havikupatikana.
“Hivi vitu mnavyoviona hapa vimesalimishwa na watu
ambao huenda walishiriki katika wizi, au waliviona mahali na kwa
mapenzi yao kwa marehemu wakaamua kuvirejesha,” alisema Massawe
Alisema baadhi ya vitu hivyo vilikamatwa nje ya wilaya ya Muheza katika gereji na kwenye nyumba za watu.
Kamanda alifahamisha zaidi kuwa, hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kuhusika na tukio hilo.
“Tunaamini kuna vitu vingi vya thamani
havijapatikana, bado tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na
wananchi na mtu atakayekutwa na kitu chochote cha marehemu atashtakiwa,”
alisema Massawe.
Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa
waliokutwa na vitu hivyo, lakini hakutaja idadi yao kwa kuwa vitu
vingine havijapatikana.
“Pamoja na hayo, vitu vilikuwa vinasalimishwa
usiku na wengine walivileta mchana kwa mwenyekiti wao. Hata hivyo, si
kwamba mtu aliyeleta anakamatwa papo hapo, ila wale watakaokutwa navyo
tutawakamata na kuwashtaki,” alisema Kamanda Massawe.
0 Comments