Imeelezwa kuwa kasi ndogo ya kupungua kwa umasikini nchini inatokana na sekta zinazoendesha uchumi kutoajiri watu wengi.
Hayo yamesemwa na Mshauri Mwelekezi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya
Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Deo Mtalemwa, wakati akizungumza katika
warsha ya siku moja ya kutoa maoni ya wadau wa serikali za mitaa na
asasi za kiraia juu ya malengo ya milenia (MDG), mjini hapa jana.
Mtalemwa ambaye amefanyakazi na Benki ya Afrika (ADB) kama Afisa Mikopo
na Afisa Uhusiano kwa miaka 20, alisema sekta za msingi zinazoendesha
uchumi wa nchi kama vile, madini, viwanda, ujenzi na utalii zimeajiri
idadi ndogo ya Watanzania ikilinganishwa na sekta ya kilimo ambayo licha
ya kuajiri idadi kubwa ya watu lakini imekosa msukumo wa kutosha
kuchangia ukuaji wa uchumi.
Sababu nyingine alizotaja kukwamisha jitihada za Tanzania kupunguza
umasikini ni, kuwepo kwa migawanyo mibovu ya rasilimali za nchi, baadhi
ya mikoa kuwa na rasilimali nyingi na mingine ikiwa haina rasilimali za
kutosha na kuwepo kwa mifumo mibovu ya ukusanyaji kodi na usimamizi
wake.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo, ni lazima Tanzania ikapanua
wigo wa ukusanyaji kodi ili Watanzania wote walipe kodi na kutolea mfano
wa posho za vikao mbalimbali kuwa zimekuwa zikitolewa pasipo kukatwa
kodi jambo ambalo alidai ni eneo jingine linaloweza kupanua wigo wa
kodi.
Aidha, Mutalemwa aliwataka Watanzania kutotumia njia za ujanja ujanja
kukwepa kodi badala yake walipe kodi kwa hiari ili kujenga ujasiri wa
serikali wa kuhoji pale ambapo wanaona matumizi ya fedha zao hayafanywi
kwa usahihi.
Hata hivyo, alisema Tanzania imefanya vizuri katika kukuza uchumi wake
kutoka asilimia 6.8 mwaka jana hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka huu.
Alisema utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa umebaini kuwa, umasikini
nchini umepungua kwa asilimia 5 katika kipindi cha miaka 18 toka mpango
wa milenia wa kupunguza umasikini duniani ulipopitishwa na mataifa 189
Tanzania ikiwemo na kuanza kufanyiwa kazi mwaka 1994 mpaka sasa.
Takwimu za umoja huo zinaonyesha uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia
7.1 mwaka huu toka asilimia 6.8 mwaka 2011, huku Uganda ikionyesha
uchumi wake kukua kwa kasi zaidi kwa toka asilimia 4.1 mpaka kufikia
asilimia 6.0.
Nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki ni Rwanda ambayo uchumi
wake umekua kwa asilimia 9.9 kutoka asilimia mwaka 2011 hadi asilimia
8.8 mwaka huu, huku Burundi ukikua kwa 4.8 mwaka huu toka asilimia 4.2
mwaka jana.
Kwa upande wa Kenya, uchumi wake unaonyesha kushuka kwa asilimia 1.6 kutoka asilimia 5.1 mwaka jana hadi asilimia 3.5 mwaka huu.
0 Comments