SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi
kutoa taarifa yake ya uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, umeibuka utata wa mali
alizokuwa akimiliki, huku akidaiwa kumiliki utajiri wa kutisha likiwamo
jengo la ghorofa.
Habari za kiuchunguzi zilizopatikana zinaeleza
kuwa mbali ya jengo hilo, Kamanda Barlow anadaiwa pia kumiliki magari
zaidi ya saba yakiwamo malori mawili aina ya Fuso, malori mawili ya
mchanga, gari dogo aina ya Toyota Cresta pamoja na Toyota Hilux Double
Cabin.
Magari hayo yanadaiwa kuhifadhiwa eneo la Nyakato mjini Mwanza, yakisimamiwa na mfanyabiashara mmoja kwa niaba yake.
Mbali
na magari hayo kamanda hyo anatajwa kumiliki nyumba ya kifahari mkoani
Mara, ambayo aliijenga alipokuwa RPC mkoani humo, huku nyumba nyingine
ikiwa maeneo ya Capri-Point jirani na Ikulu ndogo mkoani Mwanza,
inayoelezwa kuwa aliinunua baada ya Serikali kutangaza uuzaji wa nyumba
zake kwa watumishi wake.
Umiliki wa mali hizo umeibua maswali
mengi, wengi wakitaka kujua iwapo zinalingana na kipato cha Kamanda
Barlow, licha ya kuwa na cheo cha Kamanda wa Polisi wa mkoa.
Jengo la ghorofa
Moja
ya mali za Kamanda huyo ambazo zimeanza kuwa gumzo mjini Mwanza ni
jengo la ghorofa ambalo ujenzi wale ulikuwa ukiendelea katika kiwanja
Namba 173 Block G, eneo la Nyakato Mahina kwa kibali Na. 6400 (Building
Permit), kilichotolewa na ofisi ya Mhandisi Jiji la Mwanza kikiruhusu
kujenga jengo la ghorofa tatu.
Mhandisi wa Jiji
Mhandisi wa
Jiji la Mwanza, Boniface Nyambele alikiri Kamanda Barlow kuomba kibali
cha kujenga jengo la ghorofa katika kiwanja hicho na kwamba, hata ujenzi
wake walikuwa wakiufuatilia kwa karibu.
“Kibali kilichotolewa
hapa kilikuwa ni kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa tatu, alipoanza
ujenzi alieleza kuwa anataka kujenga ghorofa tano, lakini baada ya
kukagua jengo hili tulikuta foundation yake ikiwa na uwezo wa kuhimili
ghorofa tatu tu, tulimzuia,” alisema Nyambele.
Hata hivyo, mmoja
wa wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake
alisema kuwa marehemu Kamanda Barlow, aliwasisitiza kujenga ghorofa
tano.
Alisema kwamba kila mara kamanda huyo alikuwa akiwaeleza
kuwa masuala ya vibali kutoka Jiji wanapaswa kumwachia yeye licha ya
wakaguzi kumkatalia.
“Baada ya kuwa tumejenga hapa ,mwezi mmoja
kabla ya kufariki alituita na kumweleza fundi wetu mkuu kuwa alikuwa
amebadili mawazo ya kujenga jengo la ghorofa tatu na kwamba, mpango wake
sasa ulikuwa ni kuongeza ghorofa nyingine mbili juu,” alisema mmoja wa
wasimamizi wake wa ujenzi na kuongeza:
“Alipoelezwa kama kisheria haikubaliki, alidai hayo hayamuhusu atasimamia yeye huko kwenye sheria.”
Mwandishi
wa habari hizi alifika eneo linapojengwa ghorofa hilo na kushuhudia
ubao unaoonyesha kuwa kibali cha ujenzi wa jengo hilo kimetolewa kwa
Liberatus Barlow.
Wizi ulikwamisha ujenzi
Hata hivyo,
majuma machache kabla ya kifo chake, eneo hilo la ujenzi kulitokea wizi
wa nondo za ujenzi, ambapo baada ya tukio hilo mwangalizi wa jengo hilo
na baadhi ya mafundi wake walikamatwa na kuwaweka mahabusu kwa siku nne
katika Kituo cha Polisi Nyakato Mwatex huku ikielezwa kuwa kamanda huyo
aliwatoa baada ya kukubaliana nao kumlipa nondo zilizopotea.
“Siku
ya wizi huo ujenzi ulisimama na tulikamatwa na kulazimishwa kulipa
nondo 10 alizodai zimeibwa, lakini msimamizi wetu nakumbuka aliamua
kulipa yeye badala yetu na kesi iliishi baada ya kuwekwa ndani siku nne.
Alilipa nondo 60 badala ya 10 na huo ulikuwa mwisho wake wa kuendelea
na kazi pamoja nasi, ” alisema kijana huyo aliyewahi kufanya kazi ya
kibarua katika jengo hilo.
Umiliki wa magari na utata
Mali
nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Kamanda Barlow ni pamoja na magari,
ambapo katika idadi ya magari hayo, gari moja aina ya Toyota Hilux
ambalo ndilo alipata nalo ajali limeonekana kuwa na utata katika umiliki
wake kutokana na namba hiyo ya usajili kubainika kuwa siyo yake kwa
vile ilisajiliwa kwa gari aina ya Nisan Premier inayomilikiwa na
wamiliki wawili.
Ingawa umiliki wa magari mengine unadaiwa
kusajiliwa kwa majina ya mfanyabiashara maarufu jijini Mwanza, lakini
umiliki wa gari ambalo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo,
alipotangaza kifo cha kamanda huyo, alilitangaza pia kuwa ni mali ya
marehemu, imebainika kuwa alilipata wiki moja kabla ya kifo chake.
Katika
uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, imebainika kuwa hata bima ya gari hilo
iliyoonyesha imekatwa kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar, ilikuwa
haitambuliki.
Kamanda Barlow alilichukua gari hilo kwa mmoja wa
wafanyabiashara jijini Mwanza, ambaye bado jeshi hilo la polisi
linamsaka kutokana na utata wa umiliki wake, kuonyesha namba hiyo siyo
halisi ya gari hilo.
Meneja wa Kampuni ya Bima
Meneja wa
Tawi la Kampuni ya Bima Zanzibar Mkoa wa Mwanza, Suzan Masele
alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema kuwa stika ya bima ya
gari hilo alilokuwa nalo Kamanda Barlow, wamefuatilia kwenye mfumo wao
wa malipo wakabaini kuwa haipo.
"Tumeangalia katika system (mfumo) yetu hakuna bima ya malipo hayo, kwa hiyo ni feki," alisema.
Aidha,
utata wa umiliki wa gari hilo pamoja na bima yake ulithibitishwa na
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, ambaye alisema jijini
Mwanza kuwa jeshi lake lilikuwa likiendelea na uchunguzi wa umiliki wa
gari hilo, pamoja na bima yake kujua ukweli na jinsi lilivyoingia
mikononi kwa marehemu siku kadhaa kabla ya kifo chake.
“Suala la
gari alilokuwa akilitumia marehemu mpaka siku mauti yanamkuta, pamoja na
bima yake, hatuwezi kulieleza hapa, kwa sasa bado tunachunguza,”
alisema IGP, alipoulizwa na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kumaliza kutoa taarifa za awali za uchunguzi wa kifo Kamanda Barlow.
0 Comments