Rais Jakaya Kikwete akimjulia hali Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhili Soraga jana.
Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhir Suleiman
Soraga, amemwagiwa tindikali na watu wasiyojulikana huko Magogoni
Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar jana.
Akizungumza na waandishi wa habari makao
makuu ya Jeshi la Polisi Ziwani Zanzibar, Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai,Yussuf Ilembo, alisema Sheikh Soraga alimwagiwa
tindikali majira ya alfajiri alipokuwa akifanya mazoezi ya viungo.
Ilembo alisema wakati akifanya mazoezi,
alimuona mtu akifanya mazoezi akielekea mbele yake na baada ya kukutana
uso kwa uso alimmwagia tindikali na kumjeruhi sehemu za usoni na kifua
kabla ya mtu huyo kutoweka.
“Tumepokea taarifa za kusikitisha na za
kinyama za kumwagiwa tindikali kwa Katibu wa Mufti… mtu mwenye akili
hawezi kufanya kitendo cha kinyama kama hicho,” alisema.
Alisema tayari uchunguzi umeanza kufanyika
na Jeshi la Polisi litahakikisha linatumia nguvu zake zote kuwasaka
watu waliohusika na mpango wa hujuma dhidi ya kiongozi huyo.
“Tayari tumeanza kufanya uchunguzi mkali dhidi ya watu waliohusika na mpango wa kumhujumu Sheikh Soraga,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya
Manazi Mmoja, Dk. Jamala Adam Taib, alisema Sheikh Soraga, amejeruhiwa
usoni na kifuani na kulazimika kusafirishwa kwenda katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MHN) jijini Dar es Salaam kwa matibabu.
Hata hivyo, alisema ni mapema kueleza
Sheikh Soraga ameathirika kwa kiwango gani baada ya kumwagiwa tindikali
hadi hapo uchunguzi wa kitibabu utakapokamilika.
“Ni mapema kusema ameathirika kwa kiwango gani kabla ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitibabu,” alisema Dk. Jamala.
Baada ya kuteremshwa katika gari la
wagonjwa Toyota DFP 5049, Sheikh Soraga alipakiwa katika ndege ya
serikali yenye namba 5H-TGF Tanzania, saa 3:45 asubuhi kupelekwa Dar es
Salaam na kusidikizwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo Makamu
wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali iddi.
KAULI YA MUFTI
Akizungumza na waandishi wa habari katika
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, Mufti wa Zanzibar, Sheikh
Saleh Kabi, aliwataka Waislamu na wananchi kuwa na subira kufuatia tukio
hilo.
Mufti Kabi alisema katika mafundisho ya
Mwenyezi Mungu, binadamu ametakiwa kuwa na uadilifu katika maisha yake
ya kila siku ikiwamo kulinda heshima yake na viongozi wake.
Alisema Zanzibar inaweza kuingia katika
maafa makubwa iwapo watu tawakosa uadilifu utavunjika kidogo na kuwataka
wananchi kurudi katika mafundisho ya mwenyezi muugu ikiwemo kujiepusha
na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na umoja wa kitaifa.
Alisema wakati umefika kwa viongozi wa
dini wafanye kazi ya dini na viongozi wa siasa wafanye kazi ya siasa
badala ya kuchanganya.
Mufti Kabi alisema matatizo yalioikuba
Rwanda na kusababisha maelfu ya raia wake kupoteza maisha yalitokana na
kutozingatiwa kwa mgawanyo wa majukumu baina ya viongozi wa kisiasa na
dini.
CCM YALAANI
Wakati huo huo; Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimeshauri serikali kuomba msaada wa uchunguzi kutoka mashirika
ya kimataifa kufutia matukio ya vitendo vya uhujuma dhidi ya raia na
mali zao Zanzibar.
Ushauri huo umetolewa Katibu Mwenezi wa
CCM Zanzibar, Issa Haji Gavu, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
iliyotolewa jana baada ya tukio la kuwa Soraga kumwagiwa tindikali.
“Kama Jeshi la Polisi uwezo wake mdogo wa
kuwafichua waharifu hawa, basi ni vyema wakaomba msaada kwenye vyombo
vya upelelezi vya kimataifa kama vile Interpol,” alisema Gavu.
Alisema yapo mashirika ya upelelezi ya
kimataifa yenye uwezo mkubwa wa uchunguzi wa mitandao ya makundi ya
uharifu na kama watafanyakazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,
vitendo vya hujuma dhidi ya raia na mali zao vitadhibitiwa kwa muda
mwafaka Zanzibar.
CUF: NI UNYAMA
Chama cha Wananchi (CUF) kimewataka
wananchi wa Zanzibar kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua watu
waliohusika na kitendo hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Salim Bimani,
alisema katika taarifa yake kuwa : “Tunawaomba wananchi watimie
mashirikiano kwa kuwafichua wale wote wanaotenda uovu Zanzibar.”
Aidha, alisema vyombo vya dola likiwamo
Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili waliohusika na uhujuma
dhidi ya kiongozi huyo wachukuliwe hatua ili sheria ichukue mkondo wake.
“Chama cha wananchi CUF kina waomba
wanachama wake, wananchi wote kwa jumla kutojiingiza katika vitendo
viovu vinavyoashiria uvunjifu wa amani nchini,” alisema Bimani.
“Tendo la uovu lililofanywa dhidi ya Sheikh Soraga limeleta huzuni na simanzi kubwa kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema Bimani.
MAMIA WAFURIKA HOSPITALI
Mamia ya wananchi jana walifurika katika
hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kupokea taarifa za kiongozi huyo
maarufu Zanzibar kuwa amemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana
visiwani humo.
Baadhi ya wananchi walishindwa kujizuia na
kulazimika kutokwa na machonzi baada ya kuona uso wa Sheikh Soraga
ulivyoathiriwa na tindikali.
Katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baadhi ya
wagonjwa waliokuwa wamelazwa walilazimika kuacha vitanda na kuanza
kuchungulia wakiwa gholofani wakifuatilia tukio la kingozi huyo.
Tukio la kumwagiwa tindikali Sheikh Soraga
limetanguliwa na matukio ya makanisa 25 na baa 12 kuchomwa moto
Zanzibar katika kipindi cha mwaka mmoja.
JK AMJULIA HALI MUHIMBILI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana alikwenda
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kumjulia Sheikh Soraga katika chumba
cha uangalizi maalumu (ICU) Muhimbili ambako amelazwa kwa matibabu muda
mfupi baada ya kuwasili kutoka visiwani Zanzibar.
Kikwete alitembelea Sheik huyo hospitalini
hapo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka katika ziara ya
kikazi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida baada ya
kupata taarifa kuwa amejeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali na watu
wasiojulikana wakati akifanya mazoezi.
Rais Kikwete amemtakia Sheikh Soraga kupata nafuu ya haraka ya majeraha aliyopata kutokana na tukio hilo.
0 Comments