Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki akizungumza na wanahabari
Na Adrophina Ndyeikiza wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
ametoa tamko kali la kuwataka Waislam kuacha mara moja kufanya
maandamano yao yaliyopangwa kufanyika siku ya Ijuamaa ya Novemba 02,
2012 mara baada ya swala ya Ijumaa. Kwa mujibu wa vipeperushi
vilivyoandikwa na kusambazwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislam
(Tz),vimewataka waislam kufanya maandamano makubwa kuelekea katika Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa upande wa Dar es Salaam na Mikoani maandamano hayo
yataelekea kwa wakuu wa Mikoa aidha kwa upande wa Zanzibar yataelekea
Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha,Sababu ya kuandamana kwao wameelezea kuwa ni kushinikiza Serikali
kutenda haki kwa wananchi wote bila ubaguzi kwani waislam wanabaguliwa
kwa mambo mengi kama vile;-Kudhalilishwa Masheikh wao kwa kukamatwa
hovyo bila sababu za msingi mfano,Sheikh Ponda na Sheikh Farid wakati
wakristo hawafanyiwi hivyo.
Akijibu hoja hiyo mbele ya waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa alisema
kuwa Sheikh Ponda hakukamatwa kama Sheikh Ponda bali amekamatwa kama mtu
yeyote yule ambaye anaweza kutuhumiwa kwa kosa fulani. Ameongeza kuwa
Serikali haikumkamata Sheikh Ponda kutokana usheikh wake/dini yake au
uislamu wake bali kutokana na kutuhumiwa kwake. “Hivyo tuache vyombo vya
sheria vifanye kazi yake na haki itazingatiwa tu.“ Alisisitiza Mkuu wa
Mkoa.
-Sababu nyingine ni pamoja na Kudhalilishwa matukufu ya Waislam huku
Serikali ikikaa kimya. Akijibu hoja hiyo pia Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
jambo hili si kweli kabisa kwani Serikali ilikwishachukua hatua stahiki
kwa kumkamata kijana huyo aliyeyekojolea Koran na kumfikisha katika
vyombo vya sheria, hivyo kijana huyo alikwishakamatwa, hata hivyo wale
wote waliokwenda kuchoma makanisa, kupiga vioo vya magari ya watu na
kuiba vitu mbalimbali katika makanisa na ndani ya magari ya watu nao pia
wapo katika mikono ya sheria kwani uislam pia hauagizi hivyo.
-Sababu ya tatu ni kuundiwa chombo cha kusimamia Waislam kwa nia ya
kuwadhibiti na kulazimishwa Waislam kukitii pamoja na ukweli kwamba
kinafisidi Uislam na Wislam.Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
kamwe Serikali haiwezi kufanya hivyo, kwani kila chombo kinaundwa na
wanajamii husika na wala Serikali haina dini hivyo haiwezi kuunda chombo
chochote kile cha kidini.Hata hivyo zipo taratibu maalumu za namna ya
kusajili taasisi yoyote ile kwani lazima kueleza mbele ya msajili ya
kuwa taasisi yenu ni ipi na ina malengo gani kwa jamii husika na msajili
akilizika na maelezo yenu basi huna budi kuisajili taasisi hiyo.
“Taasisi yoyote ile lazima isajiliwe na ifuate taratibu za sheria, na
Serikali inazisikiliza taasisi zote kama zinafuata sheria na taratibu,“
alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Hivyo basi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amesema
kuwa Waislam wote wapenda amani wasifanye maandamano yoyote siku hiyo ya
Ijumaa mara baada ya swala kwani kwa kufanya hivyo HATUA KALI ZA
KISHERIA DHIDI YA WATAKAOHUSIKA KATIKA KUYAANDAA NA KUSHIRIKI
ZITACHUKULIWA kwani maandamano hayo ni BATILI na hayajaruhusiwa na JESHI
LA POLISI. Sheria kali zitachukuliwa katika suala hili “Alisisitiza
Mkuu wa Mkoa”.
0 Comments