NI AZZAN ZUNGU NA MAKADA WENGINE WA CCM, WAKAMATWA NA TAKUKURU, BULEMBO AELEKEA KUSHINDA
Waandishi Wetu, Dodoma
MMOJA wa
Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu
pamoja na makada wengine wa CCM, juzi usiku walikamatwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma kwa tuhuma za
rushwa.
Habari zilizopatikana mjini hapa juzi usiku zinasema,
Zungu alikamatwa saa 4.30 katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa
kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa
Dodoma, Eunice Mmari, jana alikiri kuwakamata baadhi ya watu
wakijihusisha na vitendo vya rushwa akiwamo Zungu.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake, Mmari alidai kuwa vijana wake
walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku katika Hoteli ya Golden Crown
akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Wazazi.
Alisema taarifa za Zungu kudaiwa kugawa fedha hizo
walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia nyendo zake ambazo
zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.
“Tuliweka mitego yetu kila
mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la hoteli hiyo
akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na nyingine ikiwa
ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema Mmari.
Kamanda
huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa na Zungu
kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi ampigie kura.
Hata
hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja akitoa na hata fedha
hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru walizingira gari dogo
wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika Prado ambalo baada ya
vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.
Akizungumzia madai hayo Zungu
alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba nimekamatwa nikitoa
rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta wakaja watu ambao
walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea: “Samahani, halikuwa
gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi nikawaruhusu, wakaingia
wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia nikaondoka.”
Taarifa za awali
Zungu
alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
(Nec) kupitia Wazazi katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.
Habari
zilizopatikana mapema jana zilisema baada ya kukamatwa, Zungu
alipelekwa Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Dodoma ambako alihojiwa hadi saa
nane usiku alipoachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Mbunge wa Bukene
(CCM), Selemani Zedi.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa,
gari alilokuwamo lilifanyiwa upekuzi kabla ya kupelekwa Ofisi za
Takukuru, pamoja na makada wengine wa CCM ambao walikamatwa kwa tuhuma
hizohizo.
Kamanda Mmari pia alithibitisha kukamatwa kwa makada
wengine watano ambao aliwataja kuwa ni Yahaya Danga, Busuro Pazi na
Frank Mang’ati ambao alidai kwamba walikuwa wakimsaidia Zungu katika
mpango wake huo.
Mbali na watu hao, Takukuru ilimtia mbaroni
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga ambaye
anadaiwa kukamatwa akitoa rushwa ya chakula kwa wajumbe.
Alisema alikamatwa katika Hoteli ya Kitoli, Barabara ya Iringa saa tisa usiku.
Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja waliachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Katika
hatua nyingine, Mmari alisema kuwa taarifa walizokuwa nazo ni kuwa
mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alikuwa
akitoa rushwa zaidi.
“Tatizo ni kwamba wanazungumza lakini hawatoi
ushirikiano, maana kama wangetoa ushirikiano tungeweza kuwakamata kwa
urahisi,” alisema Mmari.
Bunge hawajui
Akizungumzia
kukamatwa kwa mbunge huyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
alisema Ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa zozote kuhusu kukamatwa kwa
mbunge huyo.
“Ndugu yangu, ndiyo nasikia kutoka kwako, sisi hatuna
taarifa hiyo. Ni vigumu kuzungumzia jambo ambalo sijalisikia. Hata
hivyo, nakushukuru sana kwa taarifa,” alisema Joel.
Rushwa CCM
Chaguzi
za jumuiya za CCM zimekuwa zikilalamikiwa kugubikwa kwa vitendo vya
rushwa na hata juzi baadhi ya wajumbe wa mkutano wa wazazi walilalamikia
kuwapo kwa fedha nyingi kwenye uchaguzi huo.
Chaguzi nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa ni zile za Jumuiya ya Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT).
Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa jumuiya hizo
mbili kwa nyakati tofauti, alisema vitendo vya rushwa vinavyokithiri
katika chaguzi za chama hicho, vinatishia uhai wake na kuwataka wanaCCM
kubadilika.
Akifungua mkutano wa Jumuiya ya Wazazi jana, Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal pia alizungumzia rushwa: “Hakuna sababu ya
kumchagua kiongozi kwa kuwa tu amekupa kitu kidogo! Hakuna sababu ya
mgombea kuamini kuwa ukitoa hongo na rushwa ndiyo utachaguliwa.
“Muda
wa kampeni umekwisha na sasa mmebakiza saa chache mpigiwe kura.
Sitegemei kuwa mtawapa tena nafasi wapambe wenu kujihusisha na vitendo
vya rushwa ndani ya ukumbi wa mkutano.”
Mmoja wa wajumbe alimwambia
mwandishi wetu juzi usiku kwamba rushwa iliyokuwa ikitolewa ni Sh100,000
kwa kila mjumbe, lakini fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu, ya
kwanza walipewa Sh70,000, wakati kiasi kilichobaki cha Sh30,000
walitarajiwa kupewa jana.
Nje ya ukumbi
Eneo
linalozunguka Ukumbi wa Chuo cha Mipango ulikofanyika uchaguzi huo, jana
lilihanikizwa na nyimbo za hamasa kuanzia saa 1.30 asubuhi zikitoka kwa
wapambe wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Wapambe hao
walikuwa wakiimba na kuzunguka nje ya uzio uliozunguka ukumbi huo, huku
wakiwa wamevalia fulana zenye picha za wagombea wanaowaunga mkono na
kubeba mabango yenye picha za wagombea hao.
Msafara wa mgombea wa
uenyekiti, John Barongo ulioongozwa na pikipiki, magari madogo kwa
makubwa na basi lililokuwa na wafuasi wake, uliwasili na kulakiwa na
kundi la vijana waliokuwa wakimuunga mkono. Katika msafara huo,
alikuwapo kada mkongwe wa CCM, Mzee Job Lusinde.
Baadaye, takriban
dakika saba hivi, uliwasili msafara wa mgombea mwingine wa kiti hicho,
Martha Mlata na wapambe wake na baadaye msafara wa Bulembo, hali
iliyosababisha eneo hilo la nje ya uzio kushindwa kukalika kutokana na
pilikapilka za kampeni za dakika za mwisho.
Shamrashamra hizo
zilikoma baada ya kuwasili kwa Dk Bilal ambaye alifungua mkutano huo,
kisha kukabidhi kazi ya kuuendesha kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Zakia Meghji.
Habari
tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, Bulembo alikuwa
akielekea kushinda nafasi ya uenyekiti akiwaacha mbali wenzake Mlata na
Barongo.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, uchaguzi huo ulitarajiwa kurudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura.
Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Julius Samuel na Habel Chidawali.
0 Comments