MASHINDANO ya kumsaka mrembo wa Tanzania wikiendi iliyopita yalinoga
ingawa kulikuwa na kasoro kidogo. Mrembo wa Kitongoji cha Sinza na
Kanda ya Kinondoni, Brigitte Alfred alitwaa taji la Miss Tanzania 2012
huku akiondoka na gari aina ya Noah na kitita cha Shilingi 8 milioni za
Tanzania.
Taji hilo lililokuwa linashikiliwa na Salha Israel, lilikuwa
likigombewa na warembo 30. Lakini Brigitte amedhihirisha ukali wake
baada ya kuwabwaga warembo wenzake 29 waliokuwa wakiwania taji hilo
kutoka Kanda mbambali.
Mrembo kutoka Kanda ya Ziwa Eugene Fabian alishika nafasi ya pili.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Malkia wa Kitongoji cha Kigamboni City
na Miss Temeke 2012, Edda Sylvesta huku nafasi ya nne ikichukuliwa na
Mrembo wa Dar Indian Ocean na Kinondoni, Magdalena Roy na nafasi ya Tano
ikienda Kanda ya Ziwa tena kwa Mkoa wa Mwanza, Happyness Daniel.
Warembo waliokata tiketi ya kuingia 15 bora ni Lucy Stephano mrembo
mwenye mvuto kwenye picha 'Miss Photogenic', Magdalena Roy (Top Model),
Mary Chizi (Top Sport Woman), Babylove Kalala (Miss Talent) na Happiness
Daniel (Miss Personality).
Wengine ni Waridi Frank, Happyness Rweyemamu, Edda Sylvester, Anande
Raphael, Eugene Fabian, Fina Revocatus, Irene Veda, Briggite Alfred,
Joyce Baluhi na Catherine Masumbigana.
Shughuli hiyo iliyoshereheshwa na Taji Liundi akishirikiana na Miss
Tanzania namba mbili kwa mwaka 2007 Jokate Mwegelo, ilikuwa ya utofauti
na miaka mingine huku akiwa vitu vingi vipya ambavyo havikuwahi kutokea
kwenye mashindano hayo kwa miaka ya nyuma.
Wabunifu
Hilo ni jambo jipya ambalo kwa mwaka huu washiriki walijipata
akishonewa nguo maalumu za kuvaa katika jukwaa la Miss Tanzania, kutoka
kwa wabunifu wa mitindo kwa hapa nchini.
Warembo hao walionekana kuvaa mavazi yenye rangi zinazofanana,
ambayo yalikuwa yamebuniwa na Ally Rhemtulla, Asia Idarous, Gabriel
Mollel, Kemi Kalikawe na Mustapha Hassanali.
ubunifu wa mavazi hayo ulileta picha ya kipekee, huku warembo wengi
waliovalia mavazi yenye asili ya Kimasai akiwemo Briggite Alfred,
yaliyobuniwa na Gabriel Mollel wakionekana kung'ara zaidi.
Hata hivyo, kuna baadhi ya sehemu wabunifu walichemka. Katika vazi
la ufukweni wageni waliohudhuria hafla hiyo walisikika wakiguna, kitendo
cha warembo kuvalia vazi hilo na viatu virefu. "Huwezi kwenda ufukweni
na kiatu kirefu, mambo mengine tunatakiwa kufikiria kwanza kabla ya
kuyafanyia kazi," alisikika mgeni mmoja ukumbini humo.
Walimbwende
Mazoea ya kutembea na viatu virefu yalionekana kuwa kitendawili kwa
warembo kadhaa, waliolazimika kutembea kwa shida ingawaje wasio na
macho iliwawia vigumu kutambua hilo.
Hata hivyo kujiamini lilikuwa ni jambo ambalo liliwapa wakati mgumu
warembo hao hasa baadhi waliobahatika kuingia katika hatua ya tano bora.
Namna ya kujibu maswali, kutetemeka na kutojiamini ni suala ambalo
liliwapa wakati mgumu zaidi baadhi yao.
Diamond na Recho walitumbuiza huku Wayne Star akitumia nyimbo kadhaa
za kundi la Makhirikhiri. Ni msanii ambaye watu wengi sana
wanamwamini, sijajua ni nini kilichosababisha kuimba nyimbo za wasanii
hao kutoka Botswana ilhali ana kazi zake nzuri zinazokubalika na wengi.
Watazamaji
Mwitikio ulikuwa mkubwa. Lakini sehemu husika ya tukio haikutosha.
Baadhi ya wageni kukosa hata viti vya kukaa na kusimama nyuma ya ukumbi
licha ya kulipa viingilio vikubwa.
Wageni wengi walionekana kulalamikia huduma hasa ya vyakula ambavyo viliisha mapema.
|
||
0 Comments