Mwimbaji nyota wa kundi la TOT -
Taarab, Mariam Hamis 'Mapepe', aliyetamba na wimbo wa "Paka Mapepe",
amefariki dunia usiku wa kuamkia jana wakati akijifungua ambapo
anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Magomeni jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa katibu wa kundi la TOT, Gasper Tumaini, mwimbaji huyo
alikutwa na mauti katika hospitali ya Mwananyamala ambapo mtoto yuko
hai.
Tumaini alisema kuwa msiba upo nyumbani kwao marehemu eneo la Magomeni
Makuti wakati mipango ya mazishi ikiendelea na anatarajiwa kuzikwa leo
jioni.
"Tumepoteza mmoja wa waimbaji nyota wa TOT-Taarab ambaye alikuwa
akitegemewa na kundi letu kwa umahiri wake katika uimbaji," alisema
Tumaini.
Akifafanua zaidi, alisema Mariam alijiunga na TOT-Taarab mwaka jana
akitokea Five Star Modern Taarab ambapo alikuwa miongoni mwa waanzilishi
wa kundi hilo ambalo baadaye lilipata ajali na kupoteza baadhi ya
wasanii wake.
Alisema kuwa mchango wake ulikuwa mkubwa kutokana na uwezo wa kuimba
aliojaliwa na mwenyezi Mungu pamoja na ushirikiano aliouonyesha kwa
wasanii wenzake.
Enzi ya uhai wake alianza kusikika kwenye muziki wa mwambao akiwa na
kundi la Zanzibar Stars na baadaye akahamia East African Melody kabla ya
kwenda Five Star na kisha TOT- Taarab ambako hadi anafariki alikuwa
akifanya kazi.
0 Comments