JK ammwagia sifa Waziri Magufuli

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2012/10/h8.jpg

Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuashiria kufungua rasmi barabara ya kutoka Mkuu Rombo hadi Tarakea yenye urefu wa kilomita 32 iliyojengwa kwa kiwango cha lami, katika kijiji cha Tarakea, wilaya ya Rombo, mkoa wa Kilimanjaro jana. Wengine ni Mbunge wa Hai Freeman Mbowe (kulia kwa Rais), Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (wa kwanza kushoto), na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama (kulia).


Na Mwandishi wetu

Rais  Jakaya Kikwete amemwagia sifa  Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kutokana na jinsi anavyofuatilia kwa karibu ujenzi wa barabara zinazojengwa nchini, hali inayopelekea zijengwe kwa kiwango bora na kwa wakati mwafaka.

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2012/10/h7.jpg Rais Kikwete litoa pongezi hizo kwa Waziri Magufuli jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kwasadala hadi Masama iliyopo wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, yenye urefu wa kilomita 12.5 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Rais alimsifu Waziri Magufuli kuwa amekuwa mfuatiliaji mzuri wa barabara hali ambayo imeleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kutokana na kujengwa kwa barabara nyingi kwa kiwango cha lami ambazo zimeunganisha wilaya na mikoa kadhaa nchini.

Rais Kikwete alisema kutokana na umakini wa Dk. Magufuli ndiyo maana alikabidhiwa zawadi yenye picha ya kifaru na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoani Kilimanjaro inayoashiria jinsi anavyofuatilia masuala ya kijamii na kukemea maovu.

Awali, kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuweka jiwe la msingi, Waziri Magufuli akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo na kutoa siku 60 kwa mkandarasi wa kampuni  ya Itlantic Market Limited kuendeleza shughuli za ujenzi wa barabara hiyo iliyokuwa imesimama tangu mwaka jana.

Alisema barabara hiyo itakayogharimu Sh. bilioni 5.5 ilitakiwa kukamilika  mwaka 2011 kwa mujibu wa mkataba, lakini kampuni hiyo imeshindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati licha ya kukabidhiwa fedha zote na serikali.

“Ninashangaa, baadhi ya wakandarasi wazalendo wanapolalamika majukwani wakati wakipewa kazi hawakamilishi kazi kwa wakati,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, aliiomba serikali kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kwa wakati ili kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi.

Aidha, Mbowe alimuomba Rais Kikwete kuifikiria tena Wilaya ya Hai kwa kumalizia kipande cha barabara kinachounganisha Masama na Machame chenye urefu wa kilomita 3.5 ili kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Rais  Kikwete akijibu ombi hilo, alisema serikali itaangalia uwezekano wa kujenga kipande hicho cha barabara na kumwagiza Dk. Magufuli kuangalia na kulifanyia kazi ombi hilo.

Post a Comment

0 Comments