
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera akizungumza
Na Isaac Mwangi, EANA – Arusha
JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inakamilisha
utaratibu wa kutumia viza moja itakayowawezesha watalii kutembelea
sehemu mbalimbali ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Hii ni miongoni mwa hatua iliyokubaliwa kwa pamoja na nchi za Afrika
Mashariki kuvutia watalii na wawekezaji katika kanda hiyo yenye
kujumuiahsa nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi,
linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki(EANA).
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, alisema katika mkutano wa
uwekezaji nchini Ujerumani kuwa hatua hizo ni pamoja na kuhamasisha
maboresho na uwezeshaji katika kuibua ujasiliamali kama vile mikakati ya
uanzishwaji vituo vya kibiashara, kuanzisha fursa za kimaendeleo na
kuharakisha ubadilishaji wa sheria za kitaifa zinazokinzana na nia ya
kuwepo kwa Soko la Pamoja.
Mkutano huo wa siki mbili ulifunguliwa juzi mjini Berlin na kuwaleta
pamoja wawakilishi kutoka EAC na jumuiya ya biashara ya Ujerumani.
Jumuiya pia inaandaa itifaki ya utawala bora yenye nia ya kuweka viwango
na ukomo katika kuinua utawala bora ndani ya kanda. Mapendekezo ya
itifaki hiyo kwa mujibu wa Dk. Sezibera unajumuisha maswala ya kulinda
haki za binadamu, kuzingatia utawala wa sheria na upatikanaji wa haki,
kuzingatia demokrasia na masuala ya chaguzi, uhamasishaji wa washikadau
muhimu na kupambana na rushwa.
“Upanuzi wa mtangamano wa EAC unahitaji mazingira ambayo ni tulivu na
imara katika kuinua uwekezaji wa biashara katika kanda. Migogoro ya
ndani ya aina yoyote, iwe ya ugawaji wa rasilimali au chaguzi, inahitaji
mfumo wa kikanda ambao unajua muktadha wa kanda na mgogoro wenyewe,”
alisema Dk. Sezibera katika hotuba yake ambayo EANA ilipata nakala yake.
Dk. Sezibera alisema msisitizo pia umeelekezwa kwenye upandishwaji na
uboreshaji wa mtandao uliopo wa kilomita 8,100 za reli, kwa kuongezea
upanuzi wake katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa kilomita 5,000 za njia ya reli inategemewa kuongezwa
hivi karibuni wakati mradi wa Lamu-Juba/Addis na ule wa
Isaka-Kigali/Keza utakapokamilika. Miradi hii inakadiriwa kugharimu dola
za Kimarekani billioni 29 inayojumuisha maboresho ya njia zilizopo,
kupandisha hadhi na taratibu nyingine muhimu za kuwezesha utumiaji wa
njia hizo.
Hatua zingine ni kutekeleza Mradi wa mtandao wa Barabara wa Afrika
Mashariki katika Kanda na kukamilisha miradi mingine mbayo inaendelea
kwa sasa kwa nia ya kujenga uwezo wa uhakika wa kusambaza umeme.
“Upatikanaji mpya wa nishati katika kanda umeongezea fursa katika
sekta ya nishati. Matarajio ya hifadhi ya mapipa bilioni 2.5 Uganda,
Tanzania yenye futi za ujazo 3-7 trilioni za gesi na hivi karibuni
kutangazwa kupatikana kwa mafuta nchini Kenya, vyote vinaashiria Afrika
Mashariki kuwa na mwelekeo wa uwekezaji katika miundombinu,” alisema Dk.
Sezibera.
0 Comments