MBUNGE wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe ameiandikia barua Ofisi ya Bunge kuitaarifu nia yake ya
kuwasilisha hoja binafsi katika Mkutano wa 11 wa Bunge kuliomba liazimie
Serikali iwasiliane na taasisi za kimataifa, hasa benki kusaidia
kurejeshwa nchini fedha zote haramu ambazo zimefichwa na Watanzania
katika benki za nchini Switzerland na kwingineko duniani.
Taarifa
zilizopatikana jana kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni zimeeleza
kuwa Zitto anaomba Serikali ifanye hivyo kwa Benki ya Dunia kupitia
taasisi yake ya Stolen Asset Recovery Initiative, kutekeleza jukumu
hilo.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa katika barua hiyo
Zitto anatumia kifungu cha kanuni za bunge namba 55 (1) na (2), na hoja
yake itaainisha fedha ambazo Benki ya Taifa ya Switzerland ilitangaza
kwamba Watanzania wamezihifadhi, ambazo ni Sh297 bilioni.
Barua
hiyo imeainisha kuwa fedha hizo ni sawa na Dola za Marekani 186 milioni
na Zitto amebainisha kuwa hoja yake hiyo itaainisha namna na njia
ambazo zilitumika kutorosha fedha hizo kwenda katika benki hiyo na
nyingine za nje.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashillilah alikataa kuthibitisha kupokea barua hiyo badala yake
alieleza kuwa hilo ni suala la kiofisi.
"Ni suala la
ndani la ofisi, siwezi kueleza kama ni kweli nimepokea au la, isipokuwa
suala hilo linafahamika na ofisi ya Bunge ililipokea alipoliwasilisha
bungeni hivyo linafanyiwa kazi," alisema Kashillilah.
Mapema
mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari likiwamo gazeti hili, vilifichua
kuwapo kwa fedha zilizofichwa nchini Uswisi na baadaye ilibainika
kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27 wakiwamo wanasiasa na
wafanyabiashara.
Gazeti hili pia lilibaini kwamba mmoja wa walioficha fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika
uchunguzi wake, Mwananchi limebaini pia kuwa kiasi cha fedha
kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za
Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya
kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.
Taarifa
hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo
wengine wanne, ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48
bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila
mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16 bilioni).
Kwa
kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la
Watanzania 27, wanamiliki Dola 126 milioni (Sh201.6 bilioni) sawa na
asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki
Dola 60 milioni (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.
Habari
hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na
kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania
na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na
wafanyabiashara.
0 Comments