KATIKA siku ya mwisho ya harambee ya kumchangia
mjane wa marehemu Daud Mwangosi, Zitto Kabwe amejitolea kumchangia mjane
wa marehemu kwa kumlipia ada ya uanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya
Kijamii (NSSF) kwa kila mwezi na kwa miaka mitatu mfululizo.
“Nimeona nami niunge mkono harambee hii. Pamoja na michango ya fedha
iliyotolewa kumsaidia mjane kuanzisha mradi wa kujikimu, mimi naona ni
muhimu pia mjane akawa na hakika ya huduma ya afya yake na watoto wake
wanne. Hivyo, mchango wangu utakuwa ni kwenye eneo hilo Bima ya Afya na
kwa miaka mitatu.” Anasema Zitto Kabwe alipoongea na Mjengwablog.com,
mtandao wa Kijamii ulioratibu harambee ya mjane wa Daud Mwangosi.
Hii ni mara ya pili kwa Ndugu Zitto Kabwe kuchangia kwenye masuala ya
kijamii kupitia mtandao wa kijamii wa Mjengwablog.com, mara ya kwanza
ni alitoa mchango wake pale Mtandao wa Mjengwablog.com ulipoendesha
harambee ya kuwachangia watoto wa Somalia waliokuwa katika hatari ya
kufa kwa njaa.
Katika harambee iliyomalizika Jumapili ya Septemba 30 mwaka huu na
iliyochukua kipindi cha mwezi mmoja, zaidi ya shilingi milioni tano na
nusu zimekusanywa.
Mchango huo wa Ndugu Zitto Kabwe una maana mjane wa marehemu ataweza
kuwa na hakika ya yeye na watoto wake wanne kupata huduma za afya bila
kufikiria malipo kwa kipindi cha miaka mitatu. Baada ya hapo, michango
ya mjane huyo ya kila mwezi kwa mfuko huo wa hifadhi ya kijamii (NSSF)
ambayo atakuwa akilipiwa na Ndugu Zitto Kabwe itakuwa ni malimbikizo ya
akiba yake ambayo mjane atakuwa na uwezo wa kuichukua kama akipenda. Kwa
sasa mjane wa Daud Mwangosi hayuko kwenye utaratibu wowote wa Bima ya
Afya, kwake yeye na wanawe.
Harambee ya mjane wa Daud Mwangosi iliyoendeshwa kwa uwazi kwa njia
ya MPESA, Tigo Pesa, Airtel Money, NMB Mobile na Western Union
ilimwezesha mchangiaji kuliona jina lake na mchango wake kwenye orodha
ya wachangiaji iliyokuwa ikiwekwa mtandaoni kila siku. Michango ilikuwa
ni hiyari, hakuna aliyeombwa kutoa na utaratibu haukuruhusu ahadi za
kuchangia, bali, mwenye nacho alitoa na hapo hapo kuorodheshwa kama
mchangiaji. Utaratibu haukuruhusu pia michango iliyofungamana na siasa
za vyama.
Hatua hiyo ya uwazi na kutanguliza ubinadamu na si itikadi kwenye
uchangiaji imechangia kupelekea Watanzania wengi wa kada zote, kwa namna
moja au nyingine kushiriki kwenye kuchangia. Kuna waliochangia shilingi
elfu moja na kuna waliochangia mpaka shilingi milioni moja.
Ari hii ya Watanzania kujitolea kusaidiana kwenye hali kama
iliyomkuta mjane wa Daud Mwangosi imedhihirisha umoja na upendo tulionao
kama Watanzania, na pia imeonyesha jinsi tunavyoijali amani yetu na
hivyo jamii, kupitia michango hii, imeonyesha pia kwa vitendo, dhamira
ya kulaani kwao vitendo vya maovu na vinavyotokana na matumizi ya nguvu
yasiyo ya lazima kama kile kilichomtokea mwandishi Daud Mwangosi.
Baadhi ya watu maarufu katika jamii waliojitokeza kwa hiyari yao
kumchangia mjane wa Daud Mwangosi kupitia mtandao wa kijamii wa
Mjengwablog.com ni pamoja na Shy- Rose Bhanji, Ananilea Nkya, John
Bukuku (Mmiliki wa Fullshangwe.blog) na Ndugu Mobhare Matinyi aliyepata
kuwa mhariri wa gazeti la Majira.
Michango kwa mjane wa Daud Mwangosi itaingizwa kwenye akaunti ya
mjane ya CRDB, Iringa leo alhamisi, Oktoba 4, 2012. Vielelezo vya
kibenki vitawekwa kwenye mtandao wa Mjengwablog.com kwa kila mmoja kuona
jumla iliyowasilishwa kwa mjane na orodha ya majina ya wachangiaji.
0 Comments