Aunty Ezekiel
HIVI karibuni kumetokea sintofahamu kwa msanii wa kike mahiri katika
tasnia ya filamu Swahiliwood Aunty Ezekiel ambaye ameteka vyombo vya
habari kutokana na kashifa inayomkabili ya kutinga katika onyesho akiwa
amelewa na kucheza katika majukwaa akiwa nusu uchi, lakini kama
tunakumbuka siku za nyuma msanii huyo mwenye uwezo wa kuigiza akitokea
katika ulimbwende aliwahi kufanya safari kama hizo bila vituko.
Aunt bakiwa na Wema Sepetu katika Jukwaa.
Aunt akichezeshwa na Steve Nyerere Jukwaani.
Aunty Ezekiel alikuwa katika msafara na wasanii wenzake marehemu
Steven Kanumba, Vincent Kigosi, Irene Uwoya, Blandina Chagula na binti
Hanifa Daud ‘Jenifer’,walipata kuzunguka nchi tatu DRC, Rwanda na
Burundi wakiwa katika safari ya kisanii msanii huyo akiwa na wenzake
hakuonyesha haya ambayo kwa sasa yanaishutua jamii hasa la kupigwa picha
zinazozua utata.
Mengi yanaongelewa kutoka kwa kila mdau wa sanaa lakini anajaribu
kutoa taswira anayojenga kutokana na mtazamo wake au jamii inavyojaribu
kuliona jambo lenyewe, kuna wale ambao wanajaribu kumtwisha Aunty
mwenyewe mzigo wake, lakini kuna wale ambao wanasema kuwa kuna taasisi
zinastaili kubeba lawama hizo kwa kutowasimamia wasanii katika kulinda
maadili.
.
Katibu mtendaji wa BASATA Gonche Materego, BASATA inalalamikiwa na TAFF kuchelewesha marekebisho ya Katiba ya TAFF>
Aunt akiwa Jukwaani akicheza kwa hisia Steve Nyerere akimwimbia
Tulitumia fursa kuongea na taasisi inayotakiwa kulinda maadili
kuhusiana na sakata hilo lakini utafiti unaonyesha kuwa baadhi watu
waliopewa dhamana ya kuhakikisha maadili yanalindwa kwa tasnia nzima ya
sanaa lakini majibu yao yamejaa ukatishaji tamaa huku hali ya unyonge
zaidi wakisukumia suala hilo kwa wasanii ambao sitaki kuamini kama
wanastaili jukumu hilo.
Pia Rais wa Shirikisho la Filamu (TAFF) naye aliongelea kuhusu suala
la ukosefu wa maadili kwa wasanii hasa wa filamu mlengwa mkubwa akiwa
Aunty Ezekiel na Wema Sepetu ambaye katika safari hii ya Serengeti
Fiesta Mwanza yeye hakufanya vituko kama ilivyoripotiwa kwa msanii
mwenzake Aunty Ezekiel Rais wa TAFF Simon Mwakifwamba alisema.
“Ni kweli tumesikia lakini pia kuona kupitia katika vyombo vya habari
na mitandao ya kijamii kuhusu hizo picha alizopiga Aunty Ezekiel,
lakini kwa sasa sisi kama shirikisho la wasanii tunakosa maamuzi kwa
sababu ya BASATA wanatukwamisha kutoa maamuzi kuhusu marekebisho ya
Katiba ya Shirikisho, kwetu BASATA ni kikwazo sana katika kutoa maamuzi,
“anasema Mwakifwamba Rais wa TAFF.
Rais huyo wa TAFF anasema kuwa tayari kamati ya maadili ya shirikisho
hilo imeandaa kanuni zinazoweza kutumika kwa wasanii ambao watahusika
na uvunjifu wa maadili, lakini hayo yote yamekwamishwa na BASATA kwa
kuwachelewesha katika kuipitisha Katiba ya shirikisho hilo na kuweza
kuwa na meno ya kuwaadhibu wasanii watovu wa nidhamu.
.
Simon Mwakifwamba Rais wa TAFF.
Aunt Ezekiel akiwa amepoozi na pozi tulivu.
Baada ya kuongea na wahusika wengine pia FC iliongea na
msanii Aunty Ezekiel ambaye aliongea kwa uchungu na hisia kubwa kuwa
picha zilizopigwa zilipigwa kwa makusudi kabisa katika lengo la
kuhakikisha kuwa anadhalilika kupitia picha zinazomuonyesha msanii huyo
nusu uchi, huku akilia na aliyepiga picha hizo na kuzirusha hewani bila
mawasiliano naye.
“Ni kweli nilikuwa ninacheza katika Jukwaa (Stage) na nilikuwa
nimekunywa, lakini sikuwa nimedhamiria kukaa uchi bali ni mbinu za
wapiga picha ambao walitumia njia ya kuamua kunidhalilisha kwa kunipiga
picha wakiwa chini ya Jukwaa (Stage) ili wapate kuuza magazeti yao, hata
ukiangalia picha zenyewe zimepigwa kiujanja sana, “ anasema Aunty
Ezekiel.
Msanii huyo hakuishia hapo kwa kuongelea suala la kuzagaa kwa picha
hizo za nusu uchi kuwa pamoja kuwa alikuwa amelewa bado anaamini kuwa
alistahili kuheshimiwa au kustiriwa na huyo mtu aliyepiga picha kwani
mpiga picha aliangalia maslahi yake badala ya kuangalia maslahi ya Taifa
kwa kuzingatia kuwa yeye ni kioo cha jamii.
“Na najua kuwa hayo yanafanyika kwa sababu wanajua kuwa wasanii wengi
hatuna mawakili ambao wanaweza kututetea au kufungua mashitaka kwa mtu
ambaye anaweza kumpiga mtu picha bila ridhaa yake, najua wanataka niseme
ili waendelee kuniandika vibaya jambo ambalo mimi sipo tayari kufanya
hivyo, waacha waendelee na mambo hayo yana mwisho,”anasema Aunty
Ezekiel.
Aunty anakiri kuwa ni kweli alikuwa amelewa na kupanda katika jukwaa
na kucheza kisha kupigwa picha ambazo anahisi kuhujumiwa kwa kutolewa
hewani bila ridhaa yake sasa suala linabaki kwa taasisi husika ambazo
kila siku uibuka na kutoa matamko baada ya kusoma au kusikia katika
vyombo vya habari tuna kazi kubwa kuhusu suala la maadili.
Nashangaa Aunty yule yule ambaye alifanya vizuri katika safari za
kisanaa akiwa sambamba na Ray ambaye pia yupo katika safari hizi
kubadilika ghafla na kuwa kituko na machukizo ya wapenzi wake wa filamu!
Na kama chombo kama BASATA kinakuwa kikwazo kwa kutambua mabadiliko
ya chombo ambacho imekisajili yenyewe haya maadili ambayo yana uwanda
mpana zaidi nani ambaye atatakiwa kubeba lawama ya uvunjivu wa maadili
ambayo yanazidi kuchukua kasi katika majukwaa ya matamasha?
Matamasha mengi yanafanyika sehemu za wazi zisizozingatia umri wala
maadili yanayohitaji kulindwa kwa kiwango kikubwa sana, moja kwa moja
unagundua kuwa taasisi zenye mamlaka zinakwepa majukumu kwa kurudisha
majukumu kwa vyombo visivyo na meno kama TAFF ukijuwa wazi kuwa havina
mamlaka kisheria.
Kwa upande mwingine uchunguzi umegundua kuwa baadhi ya wadau wa
filamu imebainika kuwa wanafurahia kuwepo kwa kashifa kwa wasanii wa
filamu wakiaamini kuwa kufanya hivyo kuna mfanya msanii husika kuuza
kazi zake, jambo ambalo linaweza kuwa si kweli kwani tuna mifano ya
wasanii wanaongoza kwa mauzo na hawana kashifa.
Mfano mzuri ni msanii mkongwe wa vichekesho kama King Majuto anafanya
vizuri lakini hana kashifa, kwa mantiki hiyo kama dada yangu utakuwa
uliangukia huko basi unaweza kupotea katika jamii kwani hawa wanaonunua
kazi zako kama watakereka kutokana na hilo basi ni wazi kuwa ajira yako
inaweza kuwa hatiani.
Vyombo kama BASATA ndio hasa wahusika wa maadili yetu kama tunasubiri
jamii yenyewe ndio ijilinde wakati kisheria nyinyi ndio wenye mamlaka
suala la maadili litakuwa ni ndoto kwa Tanzania, sheria lazima uchukue
mkondo, hatupaswi kusubiri mitazamo na maamuzi ya jamii au msanii kuamua
kufanya jambo anavyofikiri.
Mwisho Aunty apewe naye nafasi ya kujiendeleza, kwani siku ya siku
tutaulizwa maadili ya Mtanzania ni yapi takakosa jibu, wengi tunajaribu
kuamini kuwa kuvaa suti na nduo zingine ndio Utamaduni wetu, huku
tukiruhusu miziki ya Kwaito mingineyo ikiteka soko letu na kuua Mchriku
Sindimba, Mangala na Mdumange wakipotea tukitegemea eti wasanii ndio
wasimamie, basi tutakwisha na kubaki na wimbo wa Maadili.
0 Comments