Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow
Na George Ramadhan
Baadhi ya walimu
wa Shule ya Msingi Nyamagana wamevunja ukimya na kueleza kile
kinachodaiwa ni mahusiano kati ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Mwanza, Leberatus Barlow, na mwalimu mwenzao, Dororth Moses.
Wakizungumza na NIPASHE shuleni hapo jana, pia walielezea kusikitishwa
kwao na jinsi tukio hilo la mauaji ya RPC lilivyotokea mbele ya mwalimu
mwenzao, Doroth Moses aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia
Jumamosi eneo la Kitangiri, jijini Mwanza.
Mwalimu Doroth ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi
Kamanda huyo.
Katika mahojiano hayo Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mary Ngalula,
alisema wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio
hilo la kutisha.
Alisema wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa
kudhani anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.
“Tunamuonea huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia,
lakini sisi tuko pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi, na hivi
tunajiandaa kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake
kwani ni mjane,” alisema.
Mwalimu Baraka Magafu alisema tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu
uhusiano wa Mwalimu Doroth na Kamanda Barlow, wao (walimu) wanafahamu
kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja huko Vunjo mkoani
Kilimanjaro.
Alibainisha kuwa Mwalimu Doroth amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na
shughuli mbalimbali za watu wa kabila lake (Wachaga), hivyo hakuna
sababu ya kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu aliyekuwa amemsindikiza
nyumbani wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya harusi aliuawa kwa
kupigwa risasi.
“Ukifuatilia mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni
bahati mbaya na kingeweza kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa
akimsindikiza Mwalimu Doroth nyumbani kwake, na hata baada ya tukio,
alipowapigia simu wenzao waliokuwa nao kwenye kikao walikuwa ndipo na
wao wanafika majumbani mwao,” alisema.
Aliongeza kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa kuwa na mtazamo
hasi dhidi ya Mwalimu Doroth kama ambavyo baadhi ya watu wameanza
kuvumisha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Wakati huo huo, majonzi, simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni
mwa mambo yaliyogubika shughuli ya kuuaga mwili wa Barlow.
Mwili wa Barlow uliagwa na wakazi wa Jiji la Mwanza wakiongozwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, katika shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana jana.
Baada ya shughuli ya kuagwa mwili wa Barlow, ulisafirishwa baadaye jana
jioni kwa ndege kuelekea jijini Dar es Salaam kabla ya leo kusafirishwa
kwenda kijijini kwake Vunjo, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
WAZIRI LUKUVI
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wakazi wa Jiji la Mwanza waliojawa
na majonzi, Waziri Lukuvi alisema Jeshi la Polisi halijafilisika kwani
wapo makamanda wa kutosha ambao wataendeleza mapambano aliyoyaanzisha
Kamanda Barlow.
RC MWANZA: TUKO VITANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alisema hivi sasa vyombo vyote
vya dola vipo kazini vikifanya uchunguzi wa tukio la mauaji hayo na
kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni haraka iwezekanavyo.
“Leo Kamanda na jemedari wetu katika mapambano dhidi ya uhalifu
ameondoka, lakini nataka niwahakikishie kwamba tupo vitani, hatupaswi
kuweka silaha chini, kama mkoa tuweke silaha zetu vizuri hadi ushindi
utakapopatikana,” alisema.
Aliongeza kwamba jamii ya Mwanza na Tanzania kwa ujumla iwe na imani
kuwa waliohusika na mauaji ya Barlow hawako salama, kwani lazima
watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Naomba niwahakikishie kwamba vyombo vyote vya dola viko kazini,
waliotenda mauaji haya hawako salama, watakamatwa na kufikishwa katika
vyombo vya sheria, na jambo hili litafikia tamati mapema iwezekanavyo,”
alisisitiza Ndikilo.
DCI MANUMBA
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba,
aliwaambia waombolezaji kwamba taarifa ambazo Jeshi la Polisi limezipata
kutoka kwa wananchi zimeongeza kasi ya upelelezi wa mauaji hayo.
Aliwataka askari kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi lakini
akawataka kulipa kisasi dhidi ya mauaji ya RPC Barlow kwa kuhakikisha
wanawakamata wote waliohusika.
“Umma utambue kwamba hatutalala hadi tuwatie mbaroni wauaji, na hii
inapaswa kuwa ndiyo kawaida yetu kuhakikisha uhalifu wa aina yoyote
unashughulikiwa kwa uzito ule ule kama tunavyofanya hivi sasa katika
mauaji ya RPC Barlow,” alisema Manumba.
RPC WA MARA
Akitoa salaam za rambirambi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom
Mwakyoma, alisema kama kuna wananchi wenye taarifa za watu waliohusika
na mauaji hayo wampelekee yeye na atazifanyia kazi.
“Ningependa kuwaambi wananchi wenye taarifa za muaji ya RPC Barlow kama
wanaona shida kuzipeleka kwingine waniletee mimi tutazifanyia kazi,”
alisema Mwakyoma ambaye alimfananisha Barlow sawa na kitabu cha marejeo
(encyclopedia) kutokana na jinsi alivyokuwa akimsaidia kutatua masuala
mbalimbali.
RPC KAGERA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, alisema idadi ya
wahalifu ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya raia wema, hivyo ana
imani wakiunganisha nguvu ushindi utapatikana.
RPC SIMIYU
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alisema Jeshi la Polisi
halitakata tamaa kupambana na wahalifu licha ya Kamanda Barlow kuuawa.
RPC GEITA, TABORA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lenard Paul na Kamanda wa Polisi mkoa
wa Tabora Anthony Ruta, katika salaam zao za rambirambi walisema kwamba
Jeshi la Polisi limepoteza Kamanda shupavu, mkweli, mweledi na mwalimu
kwa makamanda wengine.
SALAMU ZA CCM
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, alisema Kamanda Barlow
alizingatia sana sheria katika utendaji wake wa kazi na alikuwa tayari
kuitika wito hata kama ni usiku wa manane.
SALAMU ZA CHADEMA
Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Carlos Majura, alisema kifo
cha Barlow ni pigo kwa wapenda amani wote, hivyo wananchi watumie nguvu
ya umma kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
POLISI WAFICHUA MAPYA
Wakati huo huo habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza
Kitengo cha Upelelezi zimeeleza kwamba simu ya upepo (radio call) ndiyo
iliyomponza Kamanda Barlow na kumsababishia kifo.
Mmoja wa maofisa upelelezi ambaye hata hivyo, hakupenda jina lake
litajwe, alisema baada ya Kamanda Barlow kuwa amemfikisha Mwalimu Doroth
nyumbani kwake, walitokea watu wawili waliokuwa na tochi ambao
walimtaka azime taa za gari, lakini yeye (Barlow) akagoma.
Alibainisha kuwa upelelezi zaidi unaonyesha kwamba walipomsogelea
walimlazimisha azime taa za gari, lakini aliendelea kushikilia msimamo
wake huku akiwaambia kuwa yeye ni RPC.
Aliendelea kusema kwamba ghafla walitokea watu wengine takribani watatu
ambao inaonekana bado hawakuamini kama kweli huyo ni RPC, lakini
alipotoa radio call ili kufanya mawasiliano ndipo walipomfyatulia risasi
na kumuua.
JK ATUMA RAMBIRAMBI
Rais Jakaya Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa mno na mauaji ya Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, yaliyotokea usiku wa
kuamkia Jumamosi jijini Mwanza.
Katika salamu za rambirambi alizompelekea Mkuu wa Jeshi la Polisi,
Inspeka Jenerali Saidi Mwema, Rais Kikwete ameagiza jeshi hilo
kuhakikisha linachukua hatua za lazima kuwakamata na kuwafikisha mbele
ya sheria watu wote wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ACP
Liberatus Barlow kilichotokea usiku wa Ijumaa katika Jiji la Mwanza
ambako watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumwua ofisa huyo
mwandamizi wa Jeshi letu la Polisi.
“Historia ya ACP Barlow ni historia ya mfano katika utumishi wa umma na
hususan katika Jeshi la Polisi. Kwa hakika, Jeshi la Polisi limempoteza
kamanda hodari na wananchi wa Tanzania, hususani wale wa Mkoa wa Mwanza,
wamempoteza mlinzi shupavu wa usalama wao na mali zao,” amesema Rais
Kikwete katika salamu zake na kuongeza:
“Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirambi kufuatia mauaji hayo.
Kupitia kwako nalitumia Jeshi zima la Polisi pole zangu kwa kuondokewa
na mwenzao na katika mazingira yenye kutia uchungu sana. Aidha, kupitia
kwako, naomba uniwasilishie salamu zangu za dhati kwa familia ya ACP
Barlow ukiwajulisha kuwa niko nao katika wakati huu mgumu sana. Naungana
nao katika kuomboleza kifo cha baba yako na mhimili wa familia yao na
katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu.
Amen.”
Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kulitia moyo Jeshi la Polisi kwa
kusema: “Kitendo hiki ni kazi ya watu waoga, lakini nawasihi kitendo
hicho kisiwakatishe tamaa katika kutekeleza wajibu wenu na kufanya kazi
nzuri ambayo mnaendelea kuifanya katika nchi yetu ya kulinda usalama
wetu na mali zetu.”
Aliongeza: “ Badala yake kitendo hiki cha woga kiwahamasishe kuongeza
kasi ya kudumisha usalama wa nchi yetu. Na kwa kuanzia, tuhakikishe kuwa
wote walioshiriki katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo wanakamatwa
na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.”
MWILI KUAGWA LEO DAR
Mwili wa marehemu Barlow utaagwa leo kuanzia saa tano asubuhi katika
Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Augustine Ukonga, jijini Dar es Salaam
na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Kilema, Moshi Vijijini,
mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho mchana kwa kufuata
taratibu za kidini na kuhitimishwa na taratibu za kijeshi.
Taarifa iliyotolewa Jana na Jeshi la Polisi Makro makuu ilieleza kuwa
taarifa zitaendelea kutolewa mara kwa mara kadiri ya mipango
itakavyokuwa inaratibiwa.
0 Comments