PATASHIKA ya uchaguzi imeendelea ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa kuchagua wenyeviti wa mikoa, huku baadhi ya
wenyeviti wa zamani wakiangushwa, sura mpya kuibuka na wengine wakitetea
nafasi zao.
Jijini Dar es Salaam, kada wa siku nyingi wa chama
hicho, Ramadhani Madabida ameibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa
CCM, Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumbwaga John Guninita aliyekuwa
akishikilia nafasi hiyo. Madabida ameshinda kwa kupata kura 310
akimng'oa John Guninita aliyekuwa mwenyekiti, ambaye alipata kura 214
huku Madison Chizii akipata kura 52.
Katika uchaguzi huo wajumbe walianza kuingia ukumbini hapo saa 2.00 asubuhi na kuanza kupiga kura saa sita mchana.
Awali
Madabida alijikuta katika wakati mgumu wakati akijinadi baada ya mjumbe
mmoja kumuuliza swali kuhusiana na kiwanda chake kudaiwa kutengeneza
dawa bandia za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi za ARV.
Hata hivyo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Assa Simba alimzuia Madabida kujibu swali hilo akisema kwamba haukuwa wakati wake.
Awali,
akifungua mkutano wa uchaguzi huo, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal
alisema kuwa chama hicho kimelenga kurudisha majimbo yake yote
yaliyochukuliwa na wapinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Natumaini
uchaguzi utakuwa wa haki bila vurugu zozote, nawaomba msiwe na wasiwasi
kwani chama chenu kipo imara kuwakabili wapinzani,” alisema Dk Bilal.
Kambi ya Sitta yapeta Habari
kutoka mkoani Tabora, zinaeleza kuwa kambi ya Samuel Sitta imeibuka
mshindi mkoani humo baada ya mtu anayetajwa kuwa mgombea wake katika
nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoani humo, Hassan Wakasuvi kuchaguliwa
kukiongoza chama hicho.
Wakasuvi alichaguliwa katika nafasi hiyo
kwa mara ya pili, alipata kura 921 kati ya kura 1012 zilizopigwa, huku
Mwamba Z mwamba akiambulia kura 75, ambapo kura 16 ziliharibika.
Kimbisa ambwaga Kusila Mzizi
wa fitina ndani ya CCM, mkoani Dodoma ulikatwa juzi baada ya Mbunge wa
Afrika Mashariki, Alhaj Adam Kimbisa kushinda kiti cha uenyekiti wa
chama hicho mkoani humo kwa kumbwaga Mwenyekiti wa zamani, William
Kusila.
Baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho, Kimbisa alisema
kuwa bado kuna watu wanaoendeleza siasa za ukabila na kuongeza kuwa
jambo hilo ni hatari kwa siasa hasa mkoani Dodoma.
Wagombea watatu
waliwania kiti hicho, ambapo Kimbisa aliibuka na ushindi wa kimbunga
kwa kupata kura 948 katika kura 1198 zilizopigwa akiwaacha Kusila
aliyepata kura 216 na Denis Bendera aliyeambulia kura 30.
Ushindi
wa Kimbisa ulianza kuonekana mapema juzi asubuhi, baada ya mkutano huo
kuanza ambapo wajumbe kutoka wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma
walipokuwa wakiingia walikuwa wakiimba wimbo wa kumsifu Kimbisa.
Baada
ya aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk
Rehema Nchimbi kumtangaza Kimbisa kuwa ndiye mshindi ukumbi mzima
ulilipuka kwa nderemo na shangwe.
Baada ya kutangaza matokeo hayo,
Dk Nchimbi aliwaita wagombea walioshindwa, ambapo wote walikubali
matokeo na kueleza kuwa uchaguzi ulikuwa ni wa haki, huku Kusila
akieleza kuwa ushindi wa Kimbisa ulikuwa ni wa kimbunga.
Kimbisa aliwashukuru waliomchagua na kueleza kuwa ubishi wa ukabila kwa mkoa wa Dodoma sasa umekwisha. Hata
hivyo, alisema kuwa Mkoa wa Dodoma bado una watu watatu ambao bado
wanaendekeza suala la ukabila na kueleza kuwa hao wamefilisika kisiasa.
“Haiwezekani
kuendeleza siasa za ukabila katika kipindi hiki cha mitandao, Dodoma
bado kuna watu watatu ambao wanaendekeza ukabila, mimi nasema
wamefilisika kisiasa na ningeomba muwapuuze kabisa,” alisema Kimbisa
bila ya kuwataja kwa majina.
Aliwataka viongozi wa CCM ngazi zote
mkoani humo, kutengeneza mipango kazi yao na kuiweka wazi kwa ajili ya
utekelezaji kuliko kutegemea misaada kwa kila kitu.
Mbunge aukwaa uenyekiti Mkoani
Morogoro Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa baada ya kumpiga
mwereka Injinia Petrol Kingu aliyeshikilia nafasi hiyo kwa awamu mbili. Uchaguzi
huo ulifanyika Oktoba 12 ambapo wajumbe halali waliopiga kura walikuwa
1160 na Kalogeris alipata kura 778, Kingu kura 291 na Hinaya Dimoso
alipata kura 86 huku kura zilizoharibika zikiwa 14.
Akitangaza
matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo, Zakhia Megid alisema kuwa
uchaguzi huo umefanyika kihalali kwa kuzingatia Katiba ya CCM na
kuwataka wanachama wa chama hicho kuwaamini waliowachagua.
Akizungumza
baada ya kutangazwa mshindi, Kalogeris aliwataka wanachama na viongozi
wengine waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali kuvunja makundi na
kuhakikisha kuwa mshikamano unadumishwa ndani ya chama.
Kalogeris
alisema kuwa, kazi iliyopo mbele ya viongozi wa CCM ni kuhakikisha Ilani
ya CCM inasimamiwa na kutekelezwa ili kukiimarisha chama na hatimaye
kiweze kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Aliongeza
kuwa kwa nafasi yake ya ubunge na uenyekiti wa CCM, hatakubali kuona
mtu ama kikundi cha watu kikipanga mbinu au kufanya mambo yanayoweza
kukiweka pabaya chama hicho.
Alisema kuwa katika kutambua mchango
wa viongozi wenzake wakiwamo aliogombea nao nafasi ya uenyekiti, ameamua
kumteua Injinia Kingu, Hinaya Dimoso, Said Ally Abdulatif Twalib kuwa
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ili waweze kutoa mchango wao katika
chama.
Kwa upande wake Injinia Kingu alisema amekubali matokeo na
hana kinyongo na WanaCCM kwa kuwa wametimiza haki yao ya kidemokrasia. Mtopa atetea kiti Lindi Mkoani
Lindi, Alli Mohamedi Mtopa amefanikiwa kutetea nafasi yake baada ya
kumshinda Ali Hassan Gwaja kwenye uchaguzi uliofanyika jana katika
Ukumbi wa Yongolo, wilayani Ruangwa.
Mtopa ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa mikoa, ameshinda tena nafasi hiyo
katika uchaguzi unaodaiwa kukithiri kwa vitendo vya rushwa na makundi ya
wagombea urais wa mwaka 2015.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Bernald
Membe alimtangaza Alli Mtopa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 523 na
kumshinda mpinzani wake pekee Ali Gwaja, aliyepata kura 314.
Hata hivyo, Gwaja hakuwapo ndani ya ukumbi wakati matokeo hayo yakitangazwa huku ikielezwa kuwa alijua mapema kuwa ameshindwa.
Mgombea
pekee wa nafasi ya Katibu Uenezi wa Mkoa, Ibrahimu Said Mpwapwa alipita
bila kupingwa kwa kura za ‘ndiyo’ na nafasi ya Katibu wa Uchumi na
Fedha ilichukuliwa na Frank Raphael Magali aliyewashinda Mohamed Lidume
Lihumbo na Rashidi Hasani Nakumbya.
Mkutano huo uliwachagua
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ambapo kwa Wilaya ya Nachingwea
waliochaguliwa ni Sada Yunus Makota na Maua Mussa Millanzi.
Wilaya
ya Liwale ni Haji Rajabu Mwenyeji na Fatuma Kilola huku Wilaya ya
Ruangwa ni Theodora Elias Mbila na Rashidi Ismail Lipea.
Wajumbe
wa Wilaya ya Kilwa ni Adjut Alli Adjut na Hamisi Omari Ligweje, huku
Wilaya ya Lindi Vijijini akiwa ni Ahmad Mussa Mbonde na Hawa Selemeni
Nameta ambapo Wilaya ya Lindi Mjini waliochaguliwa ni Aisha Alli Issa na
Hamida Abdalah Mohamed.
Habari hii imeandikwa na Bakari Kiango,
Dar, Hamida Shariff, Morogoro, Christopher Lilai, Ruangwa-Lindi, Habel
Chidawali,Dodoma, Tausi Mbowe, Tabora.
0 Comments