KIONGOZI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven
Ulimboka, amepanga kumwaga taarifa nyeti kuhusu kutekwa na kuteswa kwake
na kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, Bunju, jijini Dar es
Salaam.
Mmoja wa ndugu na rafiki wa karibu wa Dk Ulimboka, ameliambia
Mwananchi kuwa, kiongozi huyo wa jumuiya, amepanga kuanika hayo katika
mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema Dk Ulimboka, atatumia mkutano huo kueleza siri ya kutekwa kwake.
“Siku
yoyote kuanzia sasa umma, utafahamu ukweli halisi wa kilichompata
kijana wetu. Niliongea naye juzi na amenithibitishia kuwa atakutana na
waandishi wa habari na kueleza kila kitu katika masahiba yaliompata,”
alisema ndugu huyo wa Ulimboka ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake
litajwe gazetini.
Alisisitiza “Ni kweli kwamba Steven (Dk.
Steven Ulimboka) amepanga kukutana na waandishi wa habari. Anataka
kutumia mkutano huo, kuanika wote walioshiriki kumtesa, kumteka na kisha
kumtupa katika msitu wa Mabwepande,”
Alipoulizwa kuhusu kipya
ambacho daktari huyo ataueleleza ulimwengu ambacho hakijafahamika,
mwanafamilia huyo alisema: “Tuvute subira. Steven amepanga kutaja wote
waliohusika katika kutaka kuangamiza maisha yake. Ameniambia kuwa
anataka kuwaambia Watanzania ukweli wa kilichompata,”
Dk Ulimboka
alitekwa usiku wa Juni 26 mwaka huu, katika maeneo ya Leaders Club
jijini Dar es Salaam na baadaye kusukumizwa kwenye gari, kupigwa,
kufungwa mikononi na miguuni kabla ya kunyofolewa kucha na meno; katika
Msitu wa Mabwepande.
Aliokotwa na wasamaria wema asubuhi yake na
kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kabla
ya kupelekwa Afrika Kusini Juni 30 kwa matibabu zaidi.
Tangu
aliporejea nchini Agosti 12 mwaka huu, kumekuwa na shinikizo kubwa
kutoka ndani na nje ya nchi, kumtaka azungumze kwa madai kuwa kauli yake
itasaidia kujulikana kwa ukweli kuhusu kilichompata.
Kufanyika kwa
mkutano huo kunatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa kunaweza kuondoa
kiwingu hicho, ikiwa ni pamoja na kujibu baadhi ya maswali yaliyobuka
juu ya tukio hilo.
Katika mahojiano yake ya kwanza na gazeti
hili, wiki iliyopita, Dk. Ulimboka alisema hali yake inaendelea
kuimarika siku hadi siku na kwamba anamshukuru Mungu na wote
waliomuombea, ingawa bado anahitaji matibabu zaidi.
“Madaktari
wangu bado wanaendelea na uchunguzi kuhusu figo zangu ili waone kama
zinaweza kufanya kazi au zinahitaji kuondolewa na kuwekwa nyingine.
Lakini kwa jumla, hali yangu inaleta matumaini kidogo.
0 Comments