Patricia Kimelemeta na Newstar Rwechungura
SHIRIKA la Fedha la
Duniani (IMF), limetoa tathmini ya ukuaji uchumi kipindi cha nusu mwaka,
huku ikionyesha hadi sasa uchumi imeimarika.
Akizungumza Dar es
Salaam juzi, Kiongozi wa tathmini hiyo kutoka IMF, Paolo Mauro alisema
tathmini hiyo ilifanywa chini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi
(PSI), ambao umeonyesha pato la taifa linatarajiwa kukua kati ya
asilimia 6.5 hadi 7.
Mauro alisema ukuaji huo unatokana na
serikali kusimamia vizuri suala la ukusanyaji mapato, kupunguza gharama
za matumizi, kulinda matumizi ya huduma za jamii na utoaji fursa ya
uwekezaji katika miundombinu muhimu.
Alisema kutokana na hali
hiyo, serikali imesimamia mikopo ya biashara kutoka nje ili iendane na
deni la taifa, jambo ambalo linaweza kuleta maendeleo ya kuridhisha
katika utekelezaji wa malengo ya mfumo chini ya mpango maalum, ili
kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Katika kipindi cha nusu mwaka,
serikali ya Tanzania imesimamia kwa umakini ukusanyaji kodi ya mapato,
uwekezaji na kuboresha miundombinu mbalimbali inayochochea ukuaji
uchumi, jambo ambalo limesaidia kupunguza ukubwa wa deni la taifa,”
alisema Mauro.
Aliongeza kuwa ili kuongeza ufanisi zaidi,
wanapaswa kuhakikisha wanasimamia kwa umakini ulinganifu wa hesabu, ili
kuongeza mapato katika nyanja mbalimbali ikiwamo biashara, huduma,
mapato ya uchumi na uhamisho wa mali za nje ya nchi.
Alisema
kutokana na hali hiyo, serikali inapaswa kupunguza gharama za uagizaji
mafuta ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kupanda kwa gharama za
maisha, kuboresha miundombinu ya gesi asilia ili iweze kutumika kwa
shughuli mbalimbali.
“Iwapo Tanzania itasimamia kwa umakini
matumizi ya gesi asilia na kuingiza kwenye gridi ya taifa ili kuzalisha
2,500 za umeme, gharama za maisha zinaweza kupungua kwa asiliamia
kubwa,” alisema.
Pia, alisema gesi hiyo itaweza kutumia viwandani na majumbani, jambo ambalo linaweza kuongeza uzalishaji bidhaa na ajira.
Waziri
wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa alisema kutokana na tathmini hiyo,
serikali imepanga kusimamia mfumko wa bei ili kupunguza gharama za
maisha kwa wananchi.
Dk Mgimwa alisema mazao ambayo yamepanda zaidi ni mchele, sukari na mahindi.
0 Comments