Baadhi
ya magari ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) wakionekana kudhibiti
ulinzi maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. (Picha na Michuzi
Blog)
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HALI ya ukimya leo imetawala katika maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hasa kati kati ya jiji na hata
maeneo ambayo kikawaida huwa na misongamano mikubwa ya watu. Maeneo ya
Kariakoo ambayo huwa na idadi kubwa ya watu hata kwa siku za Siku Kuu
leo haikuwa hivyo, kwani yalionekana matupu na makundi ya askari
wakionekana kuweka kambi ama kuzunguka hapa na pale kuimarisha ulinzi.
Hali hii imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za baadhi ya Waislamu
kutaka kuandamana kuelekea Ikulu mara baada ya swala ya Ijumaa wakipinga
kitendo cha kukamatwa kwa mmoja wa viongozi wa taasisi za Uislamu,
Sheikh Ponda Issa Ponda na kushikiliwa kwa baadhi ya Waislamu ambao
walikamatwa katika vurugu za uvamizi wa makanisha hivi karibuni eneo la
Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Shughuli za kibiashara hasa za maduka na nyinginezo ambazo huendeshwa
pembezoni mwa Barabara ya Uhuru, Mitaa ya Kongo, Msimbazi, Mnazi Mmoja,
Lumbumba na maeneo mengine ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo
zilisimama na maduka kuonekana yamefungwa kutokana na kuhofia vurugu za
waandamanaji.
Ulinzi wa Askari Polisi wa Kawaida, Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU)
ulikuwa mkali maeneo yote ya jiji, na baadhi ya maeneo mengine
yalionekana magari ya wanajeshi waliokuwa wamevalia mavazi ya kutuliza
ghasia wakionekana tayari kuongeza nguvu kwa Jeshi la Polisi.
Kama hiyo haitoshi polisi walitumia helkopta kufanya doria kuangalia
usalama maeneo mbalimbali ya jiji. Helkopta ya Polisi ilisikika ikipita
angani kwa kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam
kuangalia hali yoyote ya machafuko. Hali ya wasi wasi pia ilionekana kwa
baadhi ya watu na kujiami muda wote, kuhofia kujikuta wakiingia katika
vurugu hizo.
Kwa mujibu ya kipeperushi ambacho mtandao huu umekipata kikionekana
kuwa kimeandaliwa na baadhi ya washawishi wa maandamano ya leo kinasema;
Waislamu wanapaswa kuandamana wakipinga kitendo cha kushikiliwa kwa
Sheikh Ponda, kutoweka kwa Sheikh Farid Mjini Zanzibar juzi na kitendo
cha kushikiliwa na kufunguliwa kesi Waislamu waliokamatwa katika vurugu
zilizotokea hivi karibuni maeneo ya Mbagala na kuchomwa moto kwa baadhi
ya makanisa.
Hata hivyo licha ya Jeshi la Polisi kuweka ulinzi huo maeneo
mbalimbali jioni baadhi ya Waislamu waliokuwa wakitoka kuswali
walipambana na askari polisi pale walipojaribu kuandamana wakidai
wanakwenda Ikulu. Askari walidhibiti maandamano maeneo ya Kariakoo na
kuwakamata watu waliojaribu kupambana na askari waliokuwa wakilinda
usalama.
Eneo la Ikulu Jijini Dar es Salaam na makao makuu ya Wizara ya Mambo
ya Ndani napo ulinzi ulihimarishwa ili kuzuia vurugu zozote ambazo
zingeweza kuibuka. Baadhi ya waandamanaji mmoja mmoja walijikuta
wakikamatwa na polisi pale walipopenyeza na kujaribu kuibukia Ikulu huku
wakiwa wameficha kanzu zao. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya hali hiyo na kuwafahamisha wasomaji wetu.
0 Comments