TANZANIA na Oman zina mahusiano ya Kidamu na kindugu
ambayo ni maalum sana yanayopaswa kudumishwa, kuthaminiwa na kuenziwa
kwa dhati. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemuambia Mfalme Qaboos Bin Said
katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika katika nyumba ya kifalme ya Al
-Alam mara baada ya kuwasili katika Taifa la Kifalme la Oman Oktoba 15,
kuanza ziara ya kiserikali ya siku 4.
“Tanzania na Oman zina mashirikiano maalum kuliko nchi nyingine yeyote
duniani kwa sababu ya undugu wa damu uliopo baina ya watanzania na wa
Oman, hivyo hii ni ziara maalum sana katika nchi zetu.” Rais amemuambia
Mfalme.
Mfalme Qaboos amekubaliana na Rais Kikwete na kumueleza kuwa ni muhimu
mahusiano haya yakadumishwa zaidi kwa njia ya uwekezaji katika nyanja
mbalimbali, hasa katika Viwanda. Rais Kikwete amepokelewa rasmi kwa
kupigiwa mizinga 21 na kuandaliwa chakula maalum cha usiku ambapo Rais
na ujumbe wake wamehudhuria.
Katika ujumbe wake Rais amefuatana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa
Tanzania, Bernard Membe, Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter
Muhongo, Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri wa
Kazi, Ushirika na Uwezeshaji , Zanzibar, Haroun Ali Suleiman na Naibu
Waziri Fedha wa Tanzania, Janet Mbene.
Katika Ziara hii, Rais amefuatana na wafanyibiashara kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar ambapo Oktoba 16, 2012 atakuwa na kikao na
wafanyabiashara wa Tanzania na Oman na hatimaye kutia saini makubaliano
ya kibiashara na kiuchumi baina ya nchi mbili hizi. Mbali na kufanya
mkutano na wafanyibiashara, Rais atatembelea makumbusho ya jeshi na
jioni atakutana tena na Mfalme kwa ajili ya chakula binafsi cha usiku.
0 Comments