Oman Chamber of Commerce and Industry (OCCI)
Na Mwandishi Maalumu, Oman
TANZANIA na Oman zimetiliana saini mikataba mitano itakayoziwezesha
nchi hizo kufanya biashara baina yake kwa uaminifu na utaratibu ambao
unaridhisha pande zote. Mikataba hiyo imetiwa saini katika mkutano wa
wafanyabiashara wa Oman tarehe 16 Oktoba, 2012 na kushuhudiwa na Rais
Jakaya Mrisho Kikwete.
Mikataba hiyo inahusu kuundwa kwa Baraza la Biashara baina ya Oman na
Tanzania, kukuza na kulinda biashara, majadiliano ya kisiasa na, Elimu
ya Juu na makubaliano ya utunzaji na uwekaji kumbukumbu. Mara baada ya
kutiliana saini mikataba hiyo, Rais Kikwete amewaeleza wafanyibiashara
wa Oman kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Oman na kwamba
milango iko wazi, hivyo kuwakaribisha wale wote wenye nia na uwezo wa
kuwekeza katika Kilimo, Viwanda,Uvivu, Utalii na Sekta mbalimbali ambazo
Tanzania imejaliwa kuwa nazo.
Rais amesema mbali na Tanzania kuwa na eneo kubwa ambalo linajumlisha
Bara na Visiwani, “Tanzania ni mlango mkuu kwa nchi za Afrika Mashariki
na pia zile zilizopo kusini mwa Afrika na Maziwa Makuu” amesema. Na
kuwaasa wafanyibiashara wa Oman kuja kuwekeza Tanzania.
Mapema kabla ya Rais kufungua rasmi mkutano wa wafanyabiashara,
Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara na wenye Viwanda cha Oman,
Khalil Al Khonji ameelezea jinsi nchi mbili hizi zinavyofurahia na
kuuenzi uhusiano wa kindugu baina yake.
“Mahusiano ya karibu baina ya Oman na Tanzania yanaenziwa na serikali
pamoja na wananchi wake, na tunapoongelea kukuza biashara na uwekezaji
kwa ajili ya nchi zetu, tunategemea kupata suluhisho la kudumu la
kuondokana na tatizo la kutokuwepo kwa uwekezaji katika nchi zetu”
amesisitiza.
Mapema kabla ya kufungua mkutano wa wafanyabiashara, Rais Kikwete
ametembelea makumbusho ya kijeshi Bait Al Falaj ambapo ameelezwa
historia ya nchi ya Oman. Rais pia ameweka jiwe la msingi ambapo
utajengwa ubalozi wa Tanzania nchini Oman.
Katika siku yake hii ya pili, Rais Kikwete amealikwa kwenye chakula
cha usiku na Sultani Qaboos Bin Said. Rais anaendelea na ziara yake
ambapo anatarajiwa pia kukutana na watanzania wanaoishi na kufanya kazi
Oman.
0 Comments