Wakati wananchi na wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kutafakari kubwagwa kwa Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye, katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), yeye (Sumaye), ameibuka na kueleza kuwa
siku tatu zijazo ataeleza kilichojitokeza katika uchaguzi huo.
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka 10 cha
awamu ya tatu ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, aliangushwa juzi na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mary
Nagu, katika kinyang’anyiro cha Mjumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang’
Mkoa wa Manyara.
Akizungumza na NIPASHE jana kwa simu, Sumaye alisema atakapokutana na
waandishi ataeleza kwa kina kilichojitokeza kwenye uchaguzi huo siku
tatu zijazo atakapowasili jijini Dar es Salaam.
“Nimepigiwa simu na waandishi wengi wakinitaka nizungumze suala la
kuangushwa kwangu kwenye nafasi ya NEC, lakini nimewaeleza kuwa
nitaeleza suala hilo siku tatu zijazo nitakapokuwa Dar es Salaam,”
alisema Sumaye.
Dk. Nagu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang, aliibuka kidedea kwa
kupata kura 648 dhidi ya kura 481 alizopata Sumaye ambaye alikuwa Waziri
Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.
Kuangushwa kwa Sumaye katika kinyang’anyiro hicho kumezua maswali mengi
nchini ambayo baadhi ya watu wanaeleza kuwa hiyo ni ishara mbaya kwa
mwanasiasa huyo mkongwe ambaye amekuwa akihusishwa na mipango ya
kugombea urais mwaka 2015 kupitia chama hicho kikongwe.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa zamani wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utawala Bora) na Mbunge wa zamani Jimbo la Makete, Dk. Hassy Kitine,
alisema kuangushwa kwa Sumaye katika nafasi ya NEC hakuwezi kumuathiri
kisiasa kama atachukua uamuzi wa kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM.
“Katiba ya CCM haisemi kuwa kama unataka kuwania urais ni lazima uwe
mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa hiyo nasema kama Sumaye kweli
anatafuta urais, bado ana nafasi ya kuwania,” alisema Dk. Kitine ambaye
pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta, alisema uchaguzi wa NEC ni wa ngazi ya wilaya tu kwa hiyo Sumaye
anaweza akawa anakubalika kitaifa kuliko katika wilaya anayotoka.
“Kimsingi siwezi kumkadiria, sababu suala la urais ni kitu kingine, ni
uamuzi wake binafsi sababu alipochukua fomu kugombea u-Nec alijua kuna
kushinda na kushindwa, pia upo usemi kwamba nabii hakubaliki kwao,”
alisema Sitta.
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu
Lipumba, alisema kuangushwa kwa Sumaye ni dalili mbaya kwake kama
ataamua kuwania urais mwaka 2015.
Prof. Lipumba alimpongeza Dk. Nagu kwa ushindi alioupata dhidi ya
Sumaye. Hata hivyo, Lipumba alisema kushindwa kwa Sumaye hakumaanishi
kwamba hakubaliki ndani ya chama chake.
“Hizi ni dalili mbaya kwa Sumaye na inaonyesha kwamba kila nafasi
atakayogombea atashughulikiwa, pia mwanamke kumbwaga mwanaume ni
changamoto kwa vyama vingine kwamba wanawake wapewe nafasi, wana nguvu
za kuongoza,” alisema Prof. Lipumba.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Philip Mangula,
ameibuka na kujitetea kwa wanachama wa wilaya mpya ya Wanging’ombe
mkoani Njombe kwamba jina lake liliondolewa ili asiwanie nafasi ya Nec
kupitia wilaya hiyo kwa sababu alikuwa nchini Msumbiji.
Mangula aliomba kuwania nafasi ya ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya
Wanging’ombe pamoja na wanachama wengine ambao ni Mbunge wa zamani wa
Jimbo la Njombe Magharibi, Yono Kevela, Julieth Kadodo na Mechard
Msigwa, lakini jina lake lilifyekwa na vikao vya juu vya CCM.
Kuondolewa kwa jina la Mangula kulizua madai kwamba huenda kunatokana na
madai kwamba haelewani na baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya
Taifa.
“Wakati vikao vya juu vya chama vikiendelea Dodoma, nilitumwa na
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwenda Msumbiji
kuwakilisha nchi katika maadhimisho ya chama cha Frelimo,” alisema
Mangula.
Mangula akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wilaya ya Wanging’ombe
juzi, alisema madai kwamba hatakiwi na viongozi wa juu wa chama ni
uzushi.
0 Comments