MAWAKILI wanaomtetea aliyekuwa Mbunge wa Arusha,
Godbless Lema wamedai mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa mteja
wao yuko huru kwa kuwa mahakama haikutengua ubunge wake.Katika kesi
hiyo, Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande anawaongoza wenzake wa Mahakama
ya Rufani, Salum Massati na Natalia Kimaro kusikiliza maombi ya rufani
hiyo, inayopinga Lema kuvuliwa ubunge.
Mawakili hao wa Lema jana
walitoa hoja ya kupinga hukumu hiyo kufuatia mabishano baina yao na
upande wa utetezi kwa maelezo kuwa taratibu za ufunguaji wa rufaa hiyo
zimekosewa.
Awali wakili Alute Mughwai aliiomba mahakama hiyo
kutupilia mbali rufani hiyo kwa kile alichoeleza kuwa ina upungufu
mwingi wa kisheria na kikanuni.
Wakili huyo alitaja baadhi ya
kasoro za rufani hiyo kuwa ni hati ya kukaza hukumu (tuzo) ambayo
imewasilishwa mahakamani hapo kutokuwa na mhuri wa Jaji Gabriel
Rwakibarila aliyetoa hukumu ya kesi hiyo.
Alidai kuwa katika
rufani hiyo pia kuna upungufu kuhusu tarehe za kuwasilishwa kwa rufani,
pia baadhi ya vifungu vimekosewa.Wakili Mughwai alitoa kumbukumbu ya
kesi kadhaa ambazo mahakama ya rufani ilizitupa baada ya kukosa hadhi
ya kisheria kusikilizwa.
“Mawakili wa Lema walipaswa kabla ya
kuwasilisha mahakamani rufani yao, kujiridhisha kama kuna upungufu
katika nyaraka ambazo wanawasilisha mahakamani.”
Alisema kubwa
katika makosa ambayo amebaini katika rufani hiyo ni kuwasilishwa bila
kuwekwa mhuri hati ya kukaza hukumu (tuzo) iliyotolewa na Jaji aliyetoa
hukumu katika kesi ya awali.
“Hapa nani ambaye anajua sahihi ya
Jaji? Alihoji. Hawa mawakili walipaswa kushinikiza kuwekwa mhuri wa
mahakama katika hukumu hiyo ili kuthibitisha uhalali wake,” alisema
Alute.
Hata hiyo, wakili huyo alisema badala yake, mawakili hao
waliwasilisha mahakamani rufani hiyo ndani ya siku 29 tu baada ya
hukumu, badala ya siku 60 ambazo walipewa.
“Kwa kuwasilisha mahakama ya rufani, hukumu ambayo bado haina mhuri wa Jaji ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mahakama.”
Mughwai
alidai kuwa katika mazingira ya sasa hakuna cha kurekebishwa katika
rufani hiyo, badala yake itupwe na kuwataka wakata rufani kulipa gharama
zote za kesi.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa
Lema ambao ni Tundu Lissu na Method Kimomogoro, ambao walidai kuwa
hawakuwa na mamlaka ya kumlazimisha Jaji Rwakibarila kuweka mhuri.
Lissu alidai "Kama inaonekana sasa kuwa ni batili, basi hata uamuzi wa kumvua ubunge Lema ni batili," alisema.
Wakili Kimomogoro
Kwa
upande wake, Wakili Kimomogoro alisema kisheria kasoro hizo ya mhuri wa
mahakama na tarehe, haziwezi kusababisha rufani hiyo kutupwa kwani
haziathiri madai ya msingi katika rufani.
Alidai kesi hiyo ya
Lema ilikuwa ya kipekee kwani mara tu baada ya hukumu kutolewa faili
lilipelekwa jijini Dar es Salaam na maombi ya nyaraka kadhaa za kesi
hiyo yalitumwa kutoka Dar es Salaam.
“Katika mazingira kama haya hatuwezi kuepuka makosa ya kibinadamu ambayo yanatambulika kisheria,” alidai Kimomogoro.
Aliongeza
kuwa katika hoja hiyo, waliandika kifugu namba 114 badala ya 113
kimakosa ya kiuchapaji, lakini hakipotoshi kitu chochote kwani kifungu
hicho hakipo.
Wakili Kimomogoro alisema wakili mwenzake, Mughwai
ameshindwa kuzungumzia uamuzi ya kesi ambazo, hazikufutwa kutokana na
kuwa na upungufu mdogo wa aina hiyo ambao kimsingi hauathiri rufani.
Hata
hivyo, alisema kama wakili huyo alibaini makosa hayo, katika
uwasilishaji wa hoja zake, alipaswa pia kurekebisha kwa mujibu wa sheria
ya mwaka 2009 ya mahakama.
Kimomogoro pia aliwasilisha
mahakamani hoja kadhaa za kisheria na uamuzi ya Mahakama ya Rufani za
ndani na nje ya nchi, ambazo hazikutupilia mbali rufani ambazo zilikuwa
na upungufu mdogo, kwani lengo la mahakama hizo ni kutafuta haki.
“Siyo
kila kasoro au usumbufu kwenye hukumu unaweza kusababisha kutupwa
rufani kwani kasoro zote zilizotajwa ni za makosa na uchapaji na
nyingine ni za kiutaratibu tu,” alisema.
Alifafanua kuwa makosa
ambayo yanaweza kusababisha rufani kutupwa ni kama aina namba ya kesi,
majina na wadhifa wa wadau katika shauri husika, mambo yanayolalamikiwa
na mahakama imeamua nini.
Wakili huyo alifafanua kuwa jambo la
kukosekana mhuri wa mahakama wa Jaji siyo kubwa na kusababisha kutupwa
rufani kwani hakuna ambaye anapinga hukumu iliyowasilishwa mahakamani.
Kwa
upande wake, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Vitalis Timoth alisema
anaunga mkono hoja za mawakili wa Lema, kuwa pingamizi ya wakili Mughwai
haina msingi wa kisheria.
Alisema hati ya kukaza hukumu (Tuzo)
inatolewa chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na siyo chini
ya sheria ya masijala za mahakama.
Alisema siyo kazi ya jaji
aliyetoa hukumu, kuweka mhuri hukumu yake bali hiyo ni kazi ya msajili
wa mahakama na masijala za mahakama.
“Kama hati ya kukaza hukumu
ina matatizo anayepaswa kulaumiwa siyo mawakili bali ni mahakama ambayo
ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kuweka mhuri,” alisema.
Alidai kuwa
pingamizi ya awali ya rufani inapaswa kuwa na sifa mbili, kwanza iwe na
suala la kisheria na pili iendane na kesi ya msingi.
“Katika
hoja za wakili Mughwai ni wazi inathibitika pingamizi hili halina
matakwa ya kisheria kwani hata kama ikipitwa siyo kuwa itazuia
kurejeshwa tena na kusikilizwa kwa rufani ya msingi.”
Alidai ni busara kuacha kuwa na pingamizi ambazo zinaongeza gharama za kesi na muda wa kusikiliza.
“Ushauri wangu kila shauri liamuliwe kwa mazingira yake na uamuzi wa sasa uzingatie mahakama katika kutenda haki,” aliongeza.
Alidai
kwamba kutupwa kwa hoja ya kutaka waomba rufani wachapwe mijeledi
kwani kazi ya mahakama siyo kuchapa watu bali ni kutoa haki.
“Tunashauri kusikilizwa rufani kwa kuzingatia sheria na ushahidi,” alisema.
Jopo la Majaji
Baada
ya kutolewa kwa hoja za pande zote za mawakili, Jaji Chande na Jaji
Massati waliwauliza maswali kadhaa mawakili hao na kujieleza na baadaye
Jaji Chande alitangaza kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi hapo
itakapotangazwa.
Jaji Chande alisema vikao vya Mahakama ya Rufani
Kanda ya Arusha vimemalizika jana, hivyo uamuzi wa kutupwa kwa
pingamizi la rufani hiyo au la utatolewa siku itakayopangwa na mahakama.
Baada
ya uamuzi huo umati wa wafuasi wa Chadema, uliokuwa ndani na nje ya
mahakama ulianza kuimba nyimbo mbalimbali kama vile Lema Jembe na bila
Lema patachimbika.
Katika hatua ya kuepuka vurugu, Lema
alizungumza na wafuasi hao nje ya mahakama na kuwataka kuondoka kwa
amani kwenda katika ofisi ya Chadema iliyopo Ngarenaro kwa amani bila
vurugu.
Warufaniwa katika kesi hiyo ni makada wa CCM, Happy
Kivuyo, Mussa Mkanga na Agnes Mollel ambao walishinda kesi ambayo
hukumu yake ilimvua ubunge Lema Aprili 4, mwaka huu.
0 Comments