Ndege ya Rais wa Tanzania
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
anaanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Taifa la Kifalme la
Oman, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Kiserikali kufanywa na Rais wa
Tanzania katika nchi hiyo.
Rais Kikwete na ujumbe wake ameondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya
Oktoba 15, 2012, kwenda Oman kuanza ziara hiyo inayofanyika kwa mwaliko
wa Kiongozi wa Ufalme wa Oman, Mfalme Qaboos bin Said, ambaye atakuwa
mwenyeji wake kwa siku zote nne.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat, Rais Kikwete
anatarajiwa kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Yousef bin
Abdullah bin Alawi ambaye ataandamana naye hadi Jumba la Muscat Gate
ambako Rais atapokelewa na Mfalme Qaboos. Kutoka hapo wataandamana hadi
Kasri ya Kifalme ya Al Alam ambako atapokelewa rasmi kwa heshima zote za
Kiserikali.
Shughuli kubwa ya jioni ya leo ya Rais itakuwa ni kufanya mazungumzo
rasmi ya Kiserikali kati ya Serikali za Tanzania na Ufalme wa Oman na
pia kuhudhuria dhifa rasmi ambayo Mfalme Qaboos atamwandalia mgeni wake
kwenye Kasri ya Al Alam.
Kesho, Jumanne, Oktoba 16, 2012, Rais Kikwete atatembelea Jumba la
Makumbusho la Majeshi ya Ulinzi ya Oman, atafungua Mkutano wa
Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman, atashuhudia utiaji saini
makubaliano ya mikataba miwili kati ya nchi hizo mbili, ukiwamo ule wa
kuundwa kwa Baraza la Biashara la Tanzania na Oman na ule wa Kuendeleza
na Kulinda Uwekezaji katika nchi hizo mbili.
Jioni, Rais Kikwete atatunukiwa nishani ya juu kabisa ambayo Ufalme
wa Oman hutoa kwa viongozi wa nchi za nje ya First Order Medal kwenye
Chakula Maalum cha Usiku kitakachoandaliwa na Mfalme Qaboos kwa heshima
ya Rais Kikwete.
Rais Kikwete na ujumbe wake pia utakutana na kuzungumza na Watanzania
wanaoishi Oman katika mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Kifalme ya
Al Bustan. Hii itakuwa mara ya pili kwa Kikwete kutembelea Oman.
Aliitembelea nchi hiyo mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo akiwa ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
0 Comments