Mlipuko mkubwa umesikika mjini Kismayo huku wanjeshi
wa Somalia wakishirikiana na majeshi ya AU, ambao wamedhibiti maeneo
muhimu ya mji wa Kismayo.
Wenyeji wanasema kuwa mlipuko huo ulisikika kama
bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara ingawa hakuna majeruhi
wameripotiwa.
Shambulizi hilo linakuja baada ya
wapiganaji wa Al-Shabab wanaohusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda,
kuondoka Kismayo ambayo ndiyo ngome yake kubwa mwishoni mwa wiki.
Jeshi la Somalia limesema vikosi vyake
vikishirikiana na wanajeshi wa kudumisha amani wa Muungano wa Afrika,
AMISOM tayari vimeuteka Mji wa Kismayo, ambao ndiyo ngome kuu ya mwisho
ya kundi la wapiganaji la Al - Shabaab.
Kamanda wa Jeshi katika eneo hilo Ismael
Sahardiid ameiambia BBC kwamba wanamiliki taasisi zote za Serikali,
Bandari pamoja na Uwanja wa ndege.
Jumamosi iliyopita, kundi la Al Shabaab lilisema
limetumia mbinu ya kujiondoa kutoka kwenye Mji huo na linaendelea
kutekeleza mashambulizi ya kujitolea muhanga katika maeneo wasioyamiliki
tena.
Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Kenya Meja
Emmanuel Chirchir, majeshi ya Kenya na Somalia sasa yanasimamia Kituo
kikuu cha Polisi cha Kismayo na Uwanja mpya wa ndege. Aliongezea kuwa
pindi tu hali itakapokuwa shwari na salama, ndege zitaruhusiwa kutua
katika Uwanja huo wa ndege.
Chirchir amesema kuwa wataalamu wa mabomu
wametegua vilipuzi vilivyokuwa vimetegwa katika uwanja huo wa ndege na
wapiganaji wa Al-Shabaab wenye uhusiano na kundi la Al-Qaida.
Vikosi vya Muungano wa Afrika vinaisaidia
Serikali changa ya Somalia kudumisha amani katika Nchi hiyo iliyokumbwa
na misukosuko tangu mibabe wa kivita walipoupindua Utawala wa muda mrefu
wa kidikteta mwaka 1991.
0 Comments