
Baadhi ya wazee wa Mau Mau
MAHAKAMA nchini Uingereza imetoa maamuzi kuwa wazee
watatu wa Kenya ambao waliteswa na majeshi ya utawala wa kikoloni wa
Uingereza wanaweza kufungua mashtaka dhidi ya Serikali ya Uingereza, na
hivyo kuendelea mbele madai yao mengine ya ukatili. Maamuzi hayo
yametolewa Oktoba 05, 2012 katika mahakama hiyo mjini London.
Serikali ya Uingereza ambayo kwa miaka mitatu imekuwa ikiajribu
kuzuia hatua zozote za kisheria kuchukuliwa, imesema leo kuwa
imesikitishwa na uamuzi huo na kwamba inapanga kukata rufaa. Ofisi ya
Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa haipingi kuwa kila mdai wa kesi
hiyo alinyanyaswa na kuteswa wakati wa utawala wa kikoloni, lakini hata
hivyo itakata rufaa kutokana na kwamba maamuzi hayo yanaweza kuwa na
madhara makubwa ya kisheria.
Wazee hao Paulo Nzili mwenye umri wa miaka 85, Wambugu Wa Nyingi
mwenye umri wa miaka 84 na Jane Muthoni Mara mwenye umri wa miaka 73,
walifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo kuhasiwa, kubakwa na
kupigwa wakiwa kizuizini katika miaka ya 1959, wakati wa ukandamizaji wa
majeshi ya utawala wa Uingereza na washirika wao wa Kenya wakati wa
harakati za Mau Mau kupigania uhuru pamoja na ardhi.
Wazee hao watatu wanaitaka Uingereza kuwaomba radhi na kuwalipa fidia
kwa manufaa ya waathirika wote walioteswa na majeshi ya ukoloni. Wakati
maamuzi hayo yanatolewa, wazee hao watatu hawakuwepo mahakamani mjini
London. Wafuasi wa wazee hao waliokuwa wapiganaji wa Mau Mau
walikumbatiana na kufuta machozi ya furaha katika mahakama hiyo, baada
ya Jaji Richard McCombe kutoa maamuzi hayo.
Mwaka 2011, Jaji McCombe alitupilia mbali hoja ya serikali ya
Uingereza ambayo ilisema kuwa matukio yaliyotokea wakati wa vita vya Mau
Mau yalitokea wakati Kenya ikipigania uhuru wake 1963. Kwa mujibu wa
Uingereza, madai hayo yametolewa muda mrefu baada ya muda halisi wa
kisheria kupita.
Wakili anayewatetea wazee hao, Martyn Day, ameitaka serikali kuacha
kutumia sababu za kisheria kupambana na kesi hiyo na badala yake
ikubaliane namna ya kuimaliza kesi hiyo mapema iwezekanavyo kutokana na
wapiganaji hao wa zamani wa Mau Mau kuwa dhaifu na wazee.
Nzili aliyelazimishwa kujiunga na Mau Mau mwaka 1957 na ambaye
alijiondoa kwenye harakati hizo miezi sita baadae, alikamatwa akiwa
nyumbani kwake. Alihasiwa wakati yuko kizuizini kwenye kambi ya
Embakasi. Nyingi, ambaye hakuwa kabisa mwanaharakati wa Mau Mau,
alikamatwa mwaka 1952 na kuwekwa kizuizini kwa miaka tisa bila
kufunguliwa mashtaka yoyote. Aidha, Nyingi alikuwa akipigwa mara kwa
mara, likiwemo tukio ambalo wenzake 11 walipigwa hadi kufa na yeye
kujeruhiwa vibaya huku akiwa ameacha kwenye rundo la maiti kwa siku
tatu.
Mara ambaye wakati huo alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 15,
alinyanyaswa kingono, ikiwemo kubakwa kwa kuingiziwa chupa ya soda
iliyokuwa na maji ya moto kwenye sehemu zake za siri.
Maelfu ya waasi waliuawa na majeshi ya kikoloni na inakadiriwa kuwa
Wakenya 150,000, wengi wao wakiwa hawahusiki na harakati za Mau Mau,
waliwekwa kizuizini katika kambi ambazo zinafananishwa na kambi za kazi
zilizokuwa zikisimamiwa na shirika la Gulag wakati wa utawala wa
Kisovieti.
0 Comments