Msanii wa fani ya Filamu nchini Elizabeth Michael 'Lulu'
*Sasa kutinga Kisutu Jumatatu
Jopo la Majaji
watatu wa Mahakama ya Rufaa imeamua kusitisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya
kutaka kuchunguza umri wa Msanii wa fani ya Filamu nchini Elizabeth
Michael maarufu kama Lulu na badala yake imeelekeza jalada la kesi
lirudi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendea na kesi ya msingi.
Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya jopo la majaji hao wa Mahakama hiyo
kusikiliza hoja za pande zote mbili kufuatia maombi yaliyowasilishwa
mahakamani hapo na upande wa mashitaka ukiomba mahakama hiyo ifanye
marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
Juni mwaka huu, Mahakama Kuu
ilikubali kufanya uchunguzi wa umri halali wa mshitakiwa huyo, kufuatia
maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea
Mshitakiwa huyo.
Akisoma maamuzi yaliyofikiwa na jopo hilo jana jijini Naibu Msajili wa
Mahakama ya Rufaa, Zahra Maruma,alisema kuwa Jaji Dk. Fauz Twaibu hakuwa
na mamlaka ya kutenda alivyotenda kwani alitumia nguvu zake za marejeo
katika kutaka mahakama yake ichunguze umri wa mshitakiwa.
Alisema hata katika marejeo yao
hayakuwa sahihi kwani bado kulikuwa na makosa katika hilo na kwamba
upande wa Jamhuri haukutoa sababu za kuomba marejeo katika mahakama ya
Rufaa.
Maruma alisema Jaji Dk. Fauz alikosea kufanya maamuzi kwa mujibu wa
kifunga cha sheria alichokitumia cha kutaka umri wa mshitakiwa
kuchunguzwa na Mahakama Kuu.
Alisema kama palikuwa na mapungufu alitakiwa kurudisha jadala hilo
likiwa na maelekezo katika Mahakama ya Haklimu Mkazi Kisutu na sio kutoa
maamuzi ya kutaka umri wa mshitakiwa kuchunguzwa.
Maruma alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu mpaka hapo upelelezi utakapokamili.
Kwa upande wake wakili anayemtetea mshitakiwa huyo, Peter
Kibakara,alisema wamekubaliana na maamuzi hayo ya kurudi katika mahakama
ya kisuti kwa ajili ya kuendelea kwa shauri hilo.
Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii
mwenzake, Steven Kanumba. Anadaiwa kutenda kosa hilo April 7 mwaka huu
nyumbani kwa marehemu, Sinza jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, umri wake umezua mvutano mkali baina ya upande wa mashitaka
katika kesi hiyo na jopo la mawakili wanaomtetea mshitakiwa huyo, hali
ambayo mvutano huo ulipelekea kufikia ngazi ya Mahakama ya Rufaa ikiwa
kesi ya msingi bado haijaanza kusikilizwa.
Awali utata huo ulitokea pale ilipodaiwa umri wa mshitakiwa ni chini ya
miaka 18 na kwamba kesi hiyo ilitakiwa kusikilizwa katika Mahakama ya
watoto na sio katika Mahakama ya Kisutu huku upande wa mashitaka ukidai
umri wa mshitakiwa ni zaidi ya miaka 18.
Vielelezo vilivyowasilishwa Mahakamani Kuu na upande wa mashitaka
ambavyo ni hati za viapo vya wazazi wa mshitakiwa ambao ni Lucresia
Kalugila na Michael Kimemeta ikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo
vikionyesha umri wake ni miaka 17.
Hata hivyo, vielelzo vilieleza kuwa mshitakiwa huyo alizaliwa April 16
mwaka 1995 katika kituo cha afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa
namba B.0318479 cha Julai 23 mwaka 2004.
Lakini vielelezo vya upande wa mashtaka vilionyesha mshitakiwa huyo ana
umri zaidi ya miaka 18 vielelezi hivyo ni pamoja na maelezo ya
mshitakiwa alivyoitwa polisi wakati alipohojiwa kuhusiana na tuhuma
zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria na maombi la leseni ya
udereva.
Pia kuna mkanda wa video aina ya CD ya mahujiano kati ya mshitakiwa na mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga nchini.
Hivyo kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Oktoba 8 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kumbukumbu muhimu za shauri la Lulu:
Aprili 7, 2012: Steven Kanumba anafariki dunia, Lulu anadaiwa kusababisha kifo hicho.
Aprili 11, 2012: Lulu anafikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kifo cha Kanumba kutokea.
Mei 28, 2012: Utata wa umri wa Lulu waanza kuibuliwa mahakamani.
Julai 9, 2012: Shauri la utata kuhusu umri wa Lulu kuwasilishwa mahakamani.
Oktoba 5, 2012: Mahakama ya Rufaa yabainisha Lulu anastahili kushitakiwa
0 Comments