ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Mkoa wa Dodoma, William Kusila amesema kuwa Tanzania inaelekea kuzimu
na kwamba hakuna namna tena ya kukifanya chama hicho kikawa na heshima.
Kusila
ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, alishindwa
kutetea nafasi yake baada ya kuambulia kura 216 dhidi ya mpinzani wake,
Adam Kimbisa aliyezoa kura 948.
Akizungumza kwa simu kutoka
kijijini kwake Mtitaa, Dodoma, Kusila ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa
Jimbo la Bahi, alisema moyo wake umepata kunyanzi na chama hicho licha
ya kuwa ataendelea kuwa mwaminifu na mtiifu kwacho.
“Kwanza
naililia nchi yangu, pili nakililia chama changu cha Mapinduzi ambacho
daima dumu nitabaki kuwa mwanachama mwaminifu kwake, lakini siogopi
kusema hadharani kuwa nchi hii sasa inaelekea mochwari na chama ndicho
kinaelekea mwisho, ’’ alisema Kusila na kuongeza:
“Watu wanatumia
hela nyingi sana kununua kura, huku vyombo vya dola vikiangalia utadhani
havipo au havioni. Jambo hili linaniuma sana, nikiitazama nchi yangu
ikiyumba mbele ya macho yangu naumia kwa kiasi kikubwa lakini basi.”
Hata
hivyo, Kusila alisema kuwa licha ya kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu
wa chama hicho lakini anadhani kuwa CCM kimeyeyuka moyoni mwake na
kwamba kilichobaki ni mapenzi ya juu-juu na ushabiki kama ilivyo kwa
wengine.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuililia na kuiombea nchi
yao na hasa chama chao ambacho ndicho chenye dhamana ya kuiongoza nchi
na ndicho kilichoshika dola.
Alipotakiwa kueleza juu ya makundi
ndani ya CCM alisema hajui lakini anachofahamu ni juu ya kuwapo wenye
fedha ambao hawana malengo yoyote ndani ya chama hicho zaidi ya
kuonyesha utajiri wao.
Alipoulizwa kama maneno hayo yanatokana na
hasira za kushindwa Kusila alisema: “Kama wanasema kuwa ni maneno ya
mfamaji eti tunasema kwa sababu ya kushindwa nafasi zetu, acha waseme
maana hata Sumaye alisema lakini sijui wanayachukuliaje…Nami leo
nimesema na niko tayari kwa lolote kama watasema kwa nini nilisema
hivyo.”
Iringa wachaguana Kada wa CCM na
Mkurugenzi wa Shule za Star International, Jesca Msambatavangu
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Iringa baada ya
kumshinda mpinzani wake, Joseph Muhumba.
Jesca ameshinda kiti
hicho baada ya uchaguzi huo uliokuwa ukisimamiwa na Naibu Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima kurudiwa kutokana na
kutopatikana mshindi kwa mujibu wa taratibu za chaguzi za chama hicho.
Katika
uchaguzi huo, Jesca alipata kura 387 akifuatiwa na Muhumba ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo aliyepata kura 235.
Katika awamu
ya kwanza iliyoamua kurudiwa kwa uchaguzi huo, Jesca aliongoza kwa kura
271, Muhumba kura 201 na Godfrey Mosha alitupwa nje baada ya kupata kura
183.
Kivumbi Mwanza leo CCM Mkoa wa Mwanza
leo kitapata viongozi wake katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na mchuano
mkali. Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Clement Mabina anatetea nafasi
hiyo huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa
Ilemela na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo.
Wagombea
wengine wanaowania nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa
Mwanza, Joseph Yaredi, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,
Athuman Zebedayo pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,
Hussein Mashimba.
Wachunguzi wa masuala ya siasa wanaeleza kwamba
iwapo nguvu za Diallo na Mabina zitalingana, zinaweza kuwa ahueni kwa
Zebedayo na Mashimba ambao wanaonekana kuwa na kasi inayoweza kutoa
matokeo yasiyotarajiwa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce
Masunga alisema uchaguzi huo utafanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba...
“Ni imani yetu uchaguzi utafuata misingi ya kidemokrasia na wagombea
watapata nafasi ya kujieleza kwa wajumbe wao kisha kuomba kura.” Joto lapanda Kilimanjaro Homa
ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kilimanjaro inazidi kupanda huku
mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Thomas Ngawaiya akibatizwa jina la
‘Kunguru hafugiki’ ili kumchafua.
Mchuano mkali katika uchaguzi
huo unaotarajiwa kufanyika Alhamisi unatajwa kuwa kati ya Ngawaiya na
Meneja Rasilimali Watu wa zamani wa Kiwanda cha Sukari TPC, Idd Juma.
Wengine
wanaowania nafasi hiyo ni Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Usalama
Barabarani nchini, James Kombe na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa
anayemaliza muda wake, Midred Kisamo.
Imedaiwa kwamba sababu za
Ngawaiya kupewa jina hilo ni kutokana na kuhamahama vyama. Kabla ya
kuhamia CCM, Ngawaiya alikuwa Katibu Mwenezi Taifa wa Chama cha Tanzania
Labour (TLP) na kabla ya hapo alikuwa na wadhifa kama huo NCCR
-Mageuzi, chama ambacho kilitikisa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.
Habari
zinadai tangu awali, Ngawaiya hakupewa alama za kuwa miongoni mwa
wagombea watatu na kwamba jina lake lilirejeshwa na Halmashauri Kuu ya
CCM (Nec).
Akizungumzia madai hayo, Ngawaiya alisema siku zote mti
wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe... “Sifugiki kivipi wakati hao
wanaosema hawajafanya kazi kuliko nilizofanya na zote nimezifanya ndani
ya CCM.” Alisema kampeni hizo chafu zinamjenga zaidi kuliko kumchafua.
Guninita akubali matokeo Akizungumza
kwa simu jana, Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam
aliyeshindwa, John Guninita alikubaliana na matokeo akisema:
“Asiyekubali kushindwa si mshindani.” “Katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, nakubali nimeshindwa sikuona tatizo lolote, uchaguzi ulikuwa huru na haki.”
Katika
uchaguzi huo Guninita alipata kura 214 na kuangushwa na Ramadhani
Madabida aliyepata kura 310 huku Madson Chizii akipata kura 52.
0 Comments