WAFUASI WAKE WOTE WALIOGOMBEA WALIPIGWA MWEREKA Mwandishi Wetu, Hanang'
SIASA
za makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimetajwa kuwa chanzo
cha kuangushwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye katika nafasi ya
Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya Hanang’ Mkoa
wa Manyara.
Sumaye ambaye anatajwa kuwa ana nia ya kugombea
urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, alishindwa na Dk Mary Nagu ambaye ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji).
Katika uchaguzi huo, Sumaye alipata kura 481 dhidi ya Nagu, aliyepata kura 648.
Mbali
na Sumaye, wajumbe wengine waliokuwa wakimuunga mkono akiwamo
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Goma Gwantu, pia walishindwa katika
uchaguzi huo.
Dalili za kushindwa kwa Sumaye, ambaye alikuwa
akiungwa mkono na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM wa wilaya hiyo,
zilianza kuonekana wiki moja kabla ya uchaguzi huo.
Kambi ya Dk
Nagu ambayo inatajwa kwamba inaungwa mkono na kambi ya Waziri Mkuu
Mstaafu, Edward Lowassa, ilionekana kuwa na “ushawishi” mkubwa katika
vikao vya kamati ya siasa ya mkoa na kwenye Kamati Kuu ya CCM.
Hali
hiyo, ilitokana na ukweli kuwa Dk Nagu kama taratibu ambazo
zilihitajika, hakupewa baraka na kamati ya siasa ya wilaya hiyo,
kugombea kwa kile ambacho kilielezwa kukwepa mpasuko wa CCM Hanang' na
pia kumpa heshima Sumaye.
Hata hivyo, habari zimeeleza kuwa
tofauti na msimamo wa Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo, Kamati ya Siasa ya
Mkoa wa Manyara, ilionekana kumuunga mkono Dk Nagu hasa kutokana na
ukweli kuwa karibu nusu ya wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wagombea.
Kikao
cha kamati ya siasa ya mkoa, licha ya kurejesha jina la Dk Nagu pia,
kilipendekeza kuondolewa majina ya wagombea kadhaa katika wilaya ya
Hanang' likiwamo jina la Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Goma Gwaltu ambaye
alikuwa kambi ya Sumaye.
Taarifa za kupendekezwa kuondolewa
majina ya wanaomuunga mkono Sumaye, zilitolewa na baadhi ya wajumbe wa
Wilaya ya Hanang’, lakini hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara,
Ndeng'aso Ndekubali alizikanusha.
“Kamati ya siasa ya mkoa ni
kikao cha siri na nadhani ni mapema mno kulalamikia suala hilo, ni vyema
wakasubiri uamuzi wa juu, ” alisema Ndekubali.
Hata baada ya
kurejeshwa majina na Nec, ilibainika kuwa wagombea ambao Kamati ya Siasa
ya Wilaya hiyo, iliwapa alama za chini, wamerejeshwa katika mchakato wa
uchaguzi.
Dalili za kuanguka Sumaye, pia zilijionyesha siku ya
kupiga kura, ukumbini na nje ya ukumbi kutokana na wajumbe waliokuwa
wanamuunga mkono Dk Nagu kuwa na uhakika mkubwa wa ushindi.
Wakati
wa kujieleza ili aombe kura, Sumaye ambaye alionekana kama tayari
amebaini nguvu ya Dk Nagu, alieleza kushangazwa na uamuzi wa Dk Nagu
kugombea nafasi hiyo, hali ya kuwa ni waziri.
Sumaye, pia
alikemea kile alichodai kuwa ni rushwa kwenye chaguzi za CCM na kuahidi
kama akichaguliwa, angeshirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha
anawachukulia hatua kali watoa rushwa.
Awali Dk Nagu katika
maelezo yake, alitumia fursa ya kuomba kura kukanusha kuwa anatumiwa na
kundi la Lowassa ili kumkwamisha Sumaye.
Dk Nagu alifafanua kuwa
yeye kama Mbunge wa Hanang’ na Waziri, kamwe hawezi kutumiwa na kundi
fulani kwa masilahi ya makundi kwani hata yeye ana sifa za kuchaguliwa.
Wakati wa maswali, Dk Nagu hakuulizwa wakati Sumaye aliulizwa maswali matatu ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini hakuchaguliwa.
Mwenyekiti
wa CCM aliyeshindwa, Goma Gwaltu, alieleza kupinga mambo kadhaa
yaliyokiukwa katika uchaguzi, lakini hata hivyo, alisisitiza kujiandaa
kutoa tamko rasmi.
“Nitazungumza siku si nyingi kuelezea uchaguzi huu,” alisema Gwaltu.
Naye Sumaye kwa upande wake, alisema anakusudia kuzungumzia yaliyojiri katika uchaguzi huo hivi karibuni.
“Naomba
uwe na subira, nitawaita wanahabari na tutazungumza. Leo (jana)
nimepigiwa simu na waandishi kama 50, wote nimewaambia kuwa nitazungumza
siku chache zijazo,” alisema Sumaye.
Mbunge wa Viti Maalumu
Chadema, Rose Kamili ambaye kwa muda mrefu alikuwa diwani kwa tiketi ya
CCM kabla ya kuhamia Chadema, alieleza kuwa Sumaye aliangushwa kwa nguvu
ya fedha.
Alisema kuwa kitendo cha Sumaye kutajwa kuwa anataka
kuwania urais katika uchaguzi ujao ndiyo sababu ya kutoswa katika
uchaguzi huo ili kupunguza ushindani.
Kwa upande wake Gwaltu alisema kilichomwangusha Sumaye ni makundi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema
kuwa makundi hayo ambayo yameanza kujipanga kwa ajili ya kushinda
katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, yalifanya kila njia kuhakikisha
kuwa Sumaye hapenyi katika hatua hiyo, lengo likiwa ni kufanya upinzani
kuwa mdogo 2015.
Kada mkongwe wa chama hicho ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Basotu, Samwel Kawoga alisema kuwa makundi hayo
yalianza kuonekana wazi siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Alisema
kuwa makundi hayo ni pamoja na yale yanayoongozwa na makada wa chama
hicho wanaoutaka urais na mengine ni yale yanayoibuka kila unapofanyika
uchaguzi ndani ya chama hicho.
0 Comments