Kasi ya mfumuko wa bei yashuka

 Na Mwandishi wetu

Kasi  ya mfumuko wa bei nchini imeshuka kwa kiwango cha asilimia 14.9 ya Agosti  hadi asilimia 13.5 ya Septemba, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, kuhusu fahirisi za bei za kitaifa za Semptemba, mwaka huu, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo, alisema kasi hiyo imeshuka kutokana na bei ya bidhaa za vyakula majumbani na migahawani kupungua.

Alisema bei hizo zimepungua hadi kufikia asilimia 15.8 Septemba, mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 18.5 ya Agosti.

Aidha, alisema kasi ya mfumuko wa bei nchini imepungua ikilinganisha na ya mfumuko wa bei za nchi jirani.

Alisema bei za nchi jirani zimepanda na kutolea mfano nchi ya Uganda akisema imepanda kwa asilimia 5.9 kutoka 5.4 wakati Zambia alisema imepanda kwa asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.4.

“Mfumuko wa bei wa wastani kwa mwaka wa bidhaa vyakula kama unga kilo 1 Sh. 800 hadi 1,000 na mchele kilo ni Sh. 1,200 hadi 1,500 kwa Tanzania, ambapo kwa Uganda  kilo ya unga ni Sh.1200 na mchele ni Sh. 2,100 hadi Sh. 3,000 kwa fedha za Kitanzania,” alisema Kwesigabo.

Hata hivyo, alisema mfumo wa bei wa Septemba, umeongezeka kwa asilimia 1.1 ikilinganisha na asilimia 0.7 kwa Agosti, mwaka huu, fahirisi za bei zimeongezeka hadi 132.58 kutoka 131.09 ya mwaka huu.

Alisema ongezeko la mfumo huo wa bei kumechangiwa na ongezeka la bei za bidhaa zisizo za vyakula, kama vile mafuta ya taa asilimia 2.4, mkaa kwa asilimia 8.0, dizeli asilimia 6.8 na petroli asilimia 11.4.


Post a Comment

0 Comments