Muumini akishuhudia Kanisa la Pentekoste (MMPT)
lililopo Buronge la Manispaa ya Kigoma/Ujiji, liliteketezwa kwa moto na
watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.
Saa chache baada ya Rais Jakaya
Kikwete kuwasihi viongozi na waumini wa dini za Kikiristo na Kiislamu
nchini kuwa wavulilivu na kujiepusha na vitendo vya kulipiza visasi,
Kanisa la la Pentekoste (MMPT) lililopo Buronge katika Manispaa ya
Kigoma/Ujiji limechomwa moto na kutetekezwa kabisa na watu
wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema jana kuwa
tukio hilo lilitokea juzi usiku majira ya saa 4:00 usiku katika eneo la
Buronge mjini Kigoma.
Kashai alisema kanisa hilo lilichomwa na watu wasiojulikana na kwamba
mali mbalimbali zenye thamani ya Sh. 1,337,000 ziliteketea.
Alisema sababu za kuchomwa kwa kanisa hilo hazijafahamika na kwamba
hakuna mtu aliyejeruhiwa huku upelelezi wa tukio hili ukiendelea ili
kuwabaini wahalifu hao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
MCHUNGAJI ANENA
Mchungaji wa Kanisa hilo, Emmanuel Simon, alisema:
“Nilipata taarifa kuwa kanisa langu limeteketea kwa moto, nilikwenda
Polisi Central kutoa taarifa ndipo tulikwenda eneo la tukio tukakuta
kanisa lote limeteketea kwa moto.”
Alisema katika kanisa kulikuwa na mabechi 14, mlango mmoja, virago
vitatu, masanduku ya sadaka na ubao wa kufundishia, vyote vikiwa na
thamani ya Sh. 1,337,000.
Mchungaji Simon alisema hajui watu waliochoma kanisa hilo na kuiomba
serikali iangalie matukio ya uchomaji wa makanisa yanayoendelea nchi
nzima.
Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa makanisa.
Alisema kanisa ni taasisi ya jamii, hivyo anaomba serikali ichangie
gharama ya ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa
hilo wapate sehemu ya kuabudia.
KANISA LA WAADVENTISTA LALAANI
Kanisa la Waadventista Wasabato limetoa tamko rasmi dhidi ya tukio la
kuharibiwa kwa jengo la ibada la kanisa hilo lililoko Mbagala, jijini
Dar es Salaam na kuchomwa moto kwa makanisa mengine ya Kikristo na watu
wanaodaiwa kuwa ni waumini wa Kiislamu.
Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mjini Morogoro jana,
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Mashariki mwa Tanzania, Mark
Malekana, alitaka serikali kulichukulia suala hilo kwa uzito wa kipekee.
Alisema licha ya kanisa hilo licha ya kupongeza kauli za viongozi wa
madhehebu mengine ya dini na serikali za kukemea na kulaani viendo
hivyo, lakini viongozi wa dini ya Kiislam nao wanapaswa kuwachukulia
hatua za kinidhamu waumini wao wanaohatarisha amani .
“ Lazima hawa viongozi wa dini ya Kiislam wawachukulie hatua hao waumini
ambao wameanza kuharibu amani ama sivyo jamii itakuwa na picha isiyo
sahihi,” alisema.
Askofu huyo alisema matukio ya kushambulia na kuharibu majengo
matakatifu ya ibada ya Kikristo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na
hata kusababisha wasiwasi kwa waumini wa dini hiyo, jambo ambalo
likiachwa liendelee linaweza kuharibu amani nchini.
“Kanisa halikufurahishwa kabisa na kitendo cha mtoto kudhalilisha kitabu
kitukufu cha Kuran na nailipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua
zilizochukuliwa za kumuweka kituoni mtoto huyo kwa uchunguzi zaidi na
kwa usalama,” alisema.
Aliongeza: “Kitendo cha kukamatwa na polisi kinaonyesha jinsi dola
isivyochukulia kirahisi mambo yayoweza kuvuruga amani miongoni mwa
jamii. Kwa kweli kitendo cha mtoto huyo ni cha aibu.”
Alisema kuwa bado kanisa lake linalaani vitendo vya watu wazima wenye
kujua sheria za nchi, tena watu wa kiroho kuamua kuchukua hatua mkononi
kwa kuvamia kituo cha polisi na kufanya uharibifu wa makanisa ambayo
hata hayakuhusika na kitendo kilichofanywa na mtoto huyo.
“Kwa kweli vitendo hivyo havikupaswa kabisa kutendwa na watu wanaomcha
Mungu, kwani mcha Mungu ni mtu anayetegemewa kuwa muhimili wa amani
katika jamii na kutokana na hali hiyo, ninawaomba pia viongozi wa dini
ya Kiislam wawachukulie hatua za kinidhamu hawa waumini wao
wanaohatarisha amani yetu ama sivyo jamii itakuwa na picha mbaya isiyo
sahihi,” alifafanua Askofu Malekana.
Askofu huyo alisema kuwa kanisa lake limefarijika kwa kauli zilizotolewa
na viongozi mbalimbali akiwAmo Rais Kikwete; Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Mecky Sadiki; Kamanda wa Polisi Kanda na Maalum ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova na Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kwamba
zinazooneshwa kukerwa na matendo hayo na kuwataka waamini wa dhehebu
hilo na Watanzania kwa ujumla kuwa wavumilivu wakati serikali
ikishughulikia suala hilo.
Alisema Kanisa la Waadiventista Wasabato haliwezi kutafuta haki kwa
kuvunja sheria, bali linapoona kuwa halitendewi inavyostahili, huitafuta
haki kwa mujibu wa sheria.
Katika vurugu zilizotokea Oktoba 12, Mbagala jijini Dar es Salaam, jumla
ya makanisa saba yalichomwa moto na mengine kuharibiwa na kikundi cha
watu wanaotumia kivuli cha dini ya Kiislam kufanya vurugu hizo.
MBATIA: TUJADILI MUSTAKABALI
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amemuomba Rais
Jakaya Kikwete kuwakutanisha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam
pamoja na wanasiasa ili kujadili namna ya kumaliza chuki inayozuka kati
ya dini hizo mbili.
Mbatia alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari juu ya mstakabali wa vurugu zilizojitokeza wiki
iliyopita huko Mbagala, baada ya kwa waumini wa Kiislam kuchoma makanisa
kufuatia kijana mmoja wa anayedaiwa kuwa Mkristo kukojolea Kuran.
Mbatia alisema tukio hilo siyo jambo la kuchukulia kibusara eti kwamba
lilisababishwa na watoto, bali kutafuta ufumbuzi wa chanzo cha matatizo
hayo.
“Vitendo hivi havijaibuka jana wala juzi, tumeshuhudia mara kadhaa
makanisa yakichomwa hata Zanzibar tumeshuhudia, hivyo watoto nao
wanajifunza kutoka kwa wakubwa kwamba chuki ipo kati ya pande hizo,
tusisubiri itokee kama nchi za wenzetu kwa sababu nao walianza hivi
hivi,” alisema.
Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, aliongeza: “Tunaiomba serikali
isifumbie macho jambo hili, bali ichukue jukumu la kuwakutanisha
viongozi wa dini hizo pamoja na wanasiasa kuzungunguza kwa pamoja na
kuangalia namna ya kumaliza chuki iliyopo hivi sasa.”
Alisema ni jambo la kushangaza kuona viongozi wa dini na wanasiasa
wamenyamaza na pasipo kusema jambo lolote kuhusiana na vurugu
zinazojitokeza.
“Ni jambo la kushangaza kuona kwamba hali inazidi kuwa tete, lakini
wenye kuchukua maamuzi na kukemea wamekaa kimya, ni shetani gani
ameingilia nchi hii au wana lao jambo?” alihoji.
Aidha, alisema baadhi ya wanasiasa nao wamekuwa ni kichocheo cha kujenga
matabaka ya udini na kwamba kitendo hicho kinatakiwa kukemewa mara
moja.
126 KORTINI LEO
Watu 126 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Dar es Salaam
kufuatia vurugu zilizotokea katika eneo la Mbagala Kizuiani wiki
iliyopita ambazo zilisababisha kuchoma moto makanisa na kuharibu mali.
Vurugu hizo zilisababishwa na kitendo mtoto wa miaka 14 kukojolea kurani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alisema jana kuwa askari
polisi waliendelea na msako ili kubaini wahalifu katika tukio hilo,
hata hivyo, alisema kuwa walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine sita
juzi.
“Unajua jana asubuhi nilikuwa kwenye kikao kujadili suala hilo na kuamua
kuwa muda wowote kuanzia leo (jana) watuhumiwa wote watakufikishwa
mahakamani baada ya taratibu za kisheria zitakamilika,” alisema Misime.
Watu hao wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani imedaiwa kuwa ni waumini wa
dini ya Kiislam, waliovamia makanisa manne na kuyakuchoma moto, kwa
madai kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 14 alikojolea kitabu cha Kurani
tukufu.
Kufuatia vurugu hizo, mali mbalimbali ziliharibiwa ikiwa ni pamoja vifaa
vya kuendeshea ibada, vioo vya magari vilivunjwa, hasara kamili ya
uharibifu huo haijafahamika.
Rais Kikwete katika hotuba yake juzi ya kuzima mbio za Mwenge wa uhuru
na Kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Nyerere, aliwataka viongozi wa dini hizo na waumini wao kuwa
watulivu na wavumilivu wakati Jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi.
Pia alisema wahusika wa vurugu hizo watakamatwa na kuchukuliwa hatua
kali za kisheria.
0 Comments