JK: Pamoja na kejeli, tutaendelea kuvutia uwekezaji wa China

Rais Jakaya Kikwete, na mwenyekiti wake, Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper (wapili kulia) wakishuhudia wakati Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe (kushoto) akibadilishana hati na waziri katika baraza la seneti la nchi hiyo jana. Mkataba huo ulihusu makubaliano ya ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Na Mwandishi wetu

Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa pamoja na maneno ya kejeli na maswali mengi, bado Tanzania itaendelea kuvutia na kupokea wawekezaji na uwekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China kama zinavyofanya nchi za Magharibi.

Rais Kikwete amesema kuwa kamwe Tanzania haiwezi kukataa uwekezaji wa makampuni ama Serikali ya China kwa sababu uwekezaji katika Tanzania hauongozwi na itikadi bali unaongozwa na uwezo wa mwekezaji na masharti ya uwekezaji yaliyowekwa na Tanzania yenyewe.

Rais Kikwete alitoa ufafanuzi huo wakati yeye na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, walipozungumza na waandishi wa habari kwenye Bunge la Canada mjini Ottawa mara baada ya viongozi hao wawili kumaliza mazungumzo yao ya faragha kwenye siku ya pili na ya mwisho ya ziara rasmi ya Kiserikali ya Rais Kikwete nchini Canada.

Rais Kikwete alitakiwa kuelezea ni kwa nini Tanzania inapokea uwekezaji, wawekezaji na misaada kutoka China, nchi ambayo mwandishi aliyeuliza swali alidai kuwa haina demokrasia na wala haina misingi ya utawala bora inayofuatwa na Tanzania.

“Kwanza, sisi katika Tanzania tuna masharti yetu ya uwekezaji. Masharti hayo hayana kipengele cha kutaka mwekezaji awe mwana demokrasia ama iwe ni nchi ya kidemokrasia,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:   

   

“Lakini isitoshe hili ni swali lisilo na miguu kabisa. Nilipotembelea China mara ya mwisho katika lile eneo la uwekezaji la Tianjin, nilikwenda kwenye Kiwanda cha Kampuni ya Toyota ya Japan kinachotengeneza magari 600,000 kwa mwaka. Nikaambiwa kuwa kuna jumla ya viwanda vitatu vya Toyota katika China. Hii ni kampuni ya Japan.”

Amesisitiza Rais Kikwete, “Toyota ni mfano tu lakini ukweli ni kwamba uwekezaji wote mkubwa katika China ni kutoka nchi za Magharibi. China inawekeza katika chumi nyingi za nchi za Magharibi. Sasa hili ni swali gani?”

Rais Kikwete ameishukuru kwa mara nyingine tena Canada, wananchi wake na Serikali yake kwa msimamo wake wa kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania tokea uhuru mwaka 1961.

Post a Comment

0 Comments