Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Ban Ki-moon na kujadili pamoja na mambo mengine, mgogoro wa
mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Taarifa
iliyotolewa na Ikulu jana, imeeleza kuwa viongozi hao walikutana jijini
New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu amesifia jitihada za Tanzania
katika kupatia suluhu suala hilo.
“Majuzi nilikutana na Rais
Joyce Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na
Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zenu mbili zinafanya
ili kupata ufumbuzi wa amani. Hii ndiyo njia sahihi na UN inaunga mkono
njia hiyo,” alisema Ban Ki Moon.
Katika mazungumzo hayo, Rais
Kikwete alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania bado inaamini kuwa
njia sahihi na ya maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa
mpaka kwa njia ya mazungumzo.
“Wazo la awali la kutafuta
ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa
Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka
nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo,
ndivyo tulivyoanza kuzungumza,” alisema Rais Kikwete
Aliendelea:“Mpaka
kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilohilo, umekuwa katikati ya
ziwa tangu mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha
makosa ya kuuweka mpaka huo nje ya ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi
kwenye mto mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati
ya mto wenyewe.”
Rais Kikwete alibainisha kuwa kila mahali ambako
nchi zinatenganishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. “Sisi
tunadhani hata kwenye mpaka wetu na Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima
uwe katikati ya ziwa,” alisema Rais Kikwete na kuendelea:
“Katika
hali ya sasa wananchi wetu wanapokunywa maji ya Ziwa Nyasa wanakunywa
maji ya Malawi, kila watu wetu wanaposafiri ndani ya ziwa kufanya
shughuli zao wanasafiri kwenye maji ya Malawi. Hili ni jambo
linalohitaji majadiliano ya kuliweka vizuri.”
Msimamo wa Malawi
Mazungumzo
ya viongozi hao yamekuja huku Rais wa Malawi, Joyce Banda akiwa
ametangaza kujitoa kwenye mazungumzo hayo kwa madai kuwa Tanzania
imechukua hatua korofi kwa kuchapisha ramani inayoonyesha kuwa mpaka wa
ziwa hilo uko katikati.
Rais Banda alitangaza uamuzi huo wakati
alipokuwa akilihutubia taifa hilo baada ya kurejea nchini kwake akitokea
Umoja wa Mataifa (UN) alikokuwa kwa ziara ya kikazi.
"Wakati
naondoka kwenda UN nilidhani suala la mpaka wa Malawi na Tanzania
lilikuwa likihitaji mazungumzo, lakini nikiwa huko nikasikia kwamba
Tanzania imezindua ramani mpya inayogusa ziwa hilo," alisema Banda na
kuendelea;
"Baada ya hatua hiyo wavuvi wa Malawi wameanza
kufukuzwa ufukweni na boti zetu zinaondolewa Tanzania. Ni suala zito
sasa ambalo tunatakiwa kuchukua hatua nyingine," alisema.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John
Haule alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa Tanzania kwa kauli hiyo ya
Malawi alisema: "Jana sikumpata Waziri (Membe) kupata ushauri wake, ila
ninaendelea kuwasiliana na Balozi wetu Tanzania wa Malawi aifuatilie
kauli hiyo kujua kama ni kweli imetolewa na Rais."
Katibu Mku
huyo alisema ikithibitika kuwa ni kauli ya Rais Banda, atawasilina na
Waziri Membe ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi ili baadaye ajadiliane na
Rais Kikwete wakiwa huko Canada.
Katika hotuba yake ya mwishoni
mwa mwezi Septemba, Rais Jakaya Kikwete alielezea hatua zilizochukuliwa
na Serikali yake kushughulikia mzozo huo kuwa tume ya pamoja ilipanga
kukutana Septemba 10 hadi 15 mwaka huu, lakini mkutano huo
haukufanyika kwa maombi ya Serikali ya Malawi.
0 Comments