Dereva
wa Mbunge akiwa katika gari la Wagonjwa wakisubiri ndege kuelekea Dar
es Salaam kwa matibabu zaidi pamoja na Mbunge, Mary Mwanjelwa. Hawa ni
miongoni mwa waliopata ajali ya lori la mafuta jana. Picha kwa hisani ya
Mbeya Yetu Blog.
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amewatumia salamu za Rambirambi
Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Shinyanga kufuatia ajali zilizotokea Oktoba
2, 2012 mikoani humo kwa nyakati tofauti. Katika salamu zake kwa Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kufuatia ajali iliyotokea katika Mlima
Mbalizi, Barabara Kuu ya Mbeya /Tunduma, ambapo watu wapatao kumi na
mmoja (11) wanasadikiwa kupoteza maisha na wengine ishirini na moja
(21) kujeruhiwa.
Ajali hii inasadikiwa ilihusisha lori la mafuta kugonga magari
mengine matatu ya binafsi na kusababisha moto ambao umeteketeza watu na
mali.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa, habari za ajali za kusikitisha za
ajali mbaya mkoani mwako” Rais amesema na kumuambia Mkuu wa Mkoa “Nakupa
pole kwa ajali hiyo ambayo imesababisha msiba mkubwa mkoani mwako na
kuleta simanzi na huzuni kubwa, sisi sote tumehuzunishwa na kushtushwa”
amesema.
Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Nassoro Rufunga
kufuatia ajali iliyotokea Kahama, ambapo watu watatu (3) wamefariki na
wengine ishirini na tatu (23) kujeruhiwa ambapo inasemekana basi la
abiria liligongana na lori la mizigo.
Rais amewaomba Wakuu wa Mikoa kuwafikishia salamu za rambirambi ndugu
wa marehemu na pia kuwatakia heri majeruhi wote ili waweze kurudi
katika shughuli zao za maendeleo.
Rais ametuma salamu hizo akiwa anatarajia kuanza ziara ya kiserikali
nchini Kanada kuanzia tarehe 3-6 Oktoba, 2012 kufuatia mualiko wa Gavana
Jenerali wa Kanada Mheshimiwa David Johnston.
Katika salamu zake, Rais pia amewataka viongozi wote kutochoka
kuwakumbusha raia, wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva kuwa
waangalifu na makini wakati wanapokuwa safarini kwani usalama
barabarani ni jambo muhimu sana wakati wanapokuwa barabarani.
Rais ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja wapo kuhakikisha usalama
wa kila mtumiaji unazingatiwa, na ni jukumu la ziada kwa madereva
wanaoendesha vyombo hivyo. Rais pia amewakumbusha madereva wote nchini
kuwa makini na magari yao na pindi wanapokuwa barabarani.
“Nawaomba viongozi wote tusichoke kuwakumbusha madereva na wananchi
kwa ujumla kuwa usalama barabarani ni usalama wa maisha na mali zao,
hivyo wote wanatakiwa kuwa makini wakati wote.”
Rais amekumbushia kuwa sherehe za siku za usalama barabarani zisiwe
zinaazimishwa na kusahaulika siku hiyo hiyo, ziwe za kudumu na siku zote
wananchi, wamiliki wa vyombo vya moto, na madereva watambue kuwa
usalama barabarani ni kitu cha kudumu, hivyo sheria na taratibu zinafaa
kuzingatiwa siku zote, ili kujiepusha na vifo, ulemavu na uharibifu wa
mali.
Rais Pia amewataka wakuu wa vyombo vya Usalama nchini kufanya
uchunguzi wa vyanzo vya ajali hizi, kuwafikisha mbele ya sheria na
kuwachukulia hatua wale wote watakaokuwa na hatia na kusababisha
uharibifu huu mkubwa wa maisha na mali za watu.
0 Comments