JESHI la Kenya limekiri kuwa mwanajeshi wake mmoja
amefyatua risasi na kuwaua raia sita wa Somalia juzi. Pamoja na hayo
jeshi hilo limesema linafanya uchunguzi na mara baada ya uchunguzi
litachukua hatua zinazostahili kwa muhusika.
Taarifa kutoka nchini Somalia zinasema tukio hilo lilitokea katika
Kijiji cha Janaay Abdalla, ambacho kiko umbali wa kilomita sita kutoka
Mji wa Kismayo ambao umekuwa ngome kubwa ya wapiganaji wa Al Shabaab.
Msemaji wa Jeshi la Kenya, Kanali Cyrus Oguna alikana madai kuwa
mauaji hayo yalifanywa kwa maksudi na kuelezea kuwa wanajeshi wake
walivamiwa na wanamgambo hao ambao waliwaua wanajeshi wawili wa Kenya.
Hapo awali Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kudumisha amani nchini Somalia
AMISOM, ulisema utachunguza mauaji hayo.
Msemaji wa kikosi cha Somalia, Mohemmed Hirsi, alisema mauaji hayo
yalitokea wakati Jeshi la Kenya lilipovamiwa na wapiganaji wa Al Shabaab
takriban kilomita sitini kutoka kwa ngome kubwa ya kundi hilo. Msemaji
wa AMISOM kanali Adi Aden amesema wakati ukweli wa kesi hiyo
utakapojulikana watachukua hatua.
Msemaji huyo aliongeza kuwa wanajeshi wa Kenya waliwafyatulia risasi
wanaume hao waliokuwa wameketi nje ya duka moja katika Kijiji cha Janaay
Cabdalla. Wanajeshi wa Kenya na wale wa Somalia awali walivamiwa na
wapiganaji wa Al Shebaab huku ripoti zikisema kuwa pande hizo mbili,
zilipata majeruhi.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, wanakijiji waliouawa ambao ni wanaume
saba hawakuwa wanamgambo bali raia wa kawaida. Taarifa zaidi zinasema
kuwa wanaume hao walikuwa wamepiga foleni kununua sukari.Aidha msemaji
wa jeshi la Muungano wa Afrika nchini Somalia, (AMISOM) alisema kuwa
hawezi kuthibitisha tukio hilo, lakini madai hayo yatachunguzwa.
Wanajeshi wa Somalia wakiungwa mkono na wale wa Uganda na Kenya
pamoja na vikosi vingine kutoka nchi tofauti za Afrika, wanakaribia
kuuzingira mji wa Kismayo, na ili waweze kufanikiwa katika kuuteka
mjihuo, wanachi wa pale watahitaji kushirikiana nao.
Wanajeshi wa Kenya wamewahi kutuhumiwa kwa kuwaua raia wakati
wakifanya mashambulizi katika maeneo ya Al Shabaab. Shirika la
kuwahudumia wakimbizi UNHCR linakadiria takriban wakimbizi 10,000
wameutoroka mji wa Kismayo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
0 Comments