Vurugu zilizosababisha baadhi ya waandamanaji kuchoma majengo eneo la Rahaleo
Maskani ya Kisonge hali ikiwa tete (Picha zote kwa hisani ya Vituko Vya Zenj Blog)
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
HALI ya hewa imechafuka Mjini Zanzibar baada ya
wafuasi wa kikundi cha Uamsho kufanya maandamano huku wakichoma moto na
kuvamia baadhi ya baa na kufanya vurugu, wakitaka kiongozi wao anaedaiwa
kutoweka ghafla.
Vurugu hizo ambazo zilikuwa ni mapambano kati ya FFU Zanzibar,
ziliambatana na kuchomwa moto baadhi ya ofisi za CCM. Taarifa zinasema
Kiongozi wa Kikundi cha Uamsho, Sheikh Farid anadaiwa kukamatwa na watu
wasiojulikana alipokuwa akitokea kwake akiwa na dereva wake na
haijulikani alipo hadi vurugu hizo zilipozuka.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida na
kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali ya ulinzi na
imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohammed Aboud Mohammed alisema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea
kuwa katika hali ya amani na utulivu. Akizungumzia tukio la vurugu
zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri Mohamed Aboud alisema vikundi
vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi
walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani, Michenzani, Muembeladu,
Magomeni, Amani wakidai Sheikh wao haonekani na kudhani amekamatwa na
vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani.
Waziri Mohamed Abud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya Dola
ikiwemo Polisi, Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa
Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, KMKM, JKU, Chuo cha
Mafunzo, Zimamoto na Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza
kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid.
Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya
kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea
kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake
na kuchukua hatua zinazofaa. Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi
likiendelea na upelelezi wake, wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu
tukio hilo kwa vituo vya Polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na
Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache
kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa
kwa mujibu wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo. Katika
tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh
Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto Maskazini
za CCM, kuvunja maduka, kupora mali za watu na kuharibu miundombinu ya
barabara na kusababisha hasara kubwa.
0 Comments