Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza (RPC) Liberatus Barlow
Na George Ramadhan
Wakati maswali magumu yakiendelea
kuwatatiza wananchi wengi juu ya kisa hasa cha mauaji ya aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, jeshi hilo limesema
linaamini kwa asilimia 100 kuwa litawatia mkononi wauaji waliohusika.
Hata hivyo, polisi wameamua kuchukua hadhari kali juu nini waseme na
nini wasiseme ikiwa ni pamoja na kutokutaka kusema kama kweli kuna mali
za RPC Barlow alizoporwa baada ya kuuawa zimekwisha kupatikana zikiwa
mikononi mwa raia kama ambavyo uvumi umezaa jijini Mwanza.
Kamanda Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa
kuamkia juzi katika eneo la Kitangiri kwenye barabara ya kuelekea Bwiru
alipokuwa amekwenda kumrejesha nyumbani kwake, mwanamke aliyejulikana
kwa jina la Doroth Moses.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kaimu Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alisema msako dhidi ya wauaji
unaendelea kila kona ya Jiji la Mwanza na vitongoji vyake na kwamba kuna
matumaini makubwa ya kuwatia mbaroni.
“Kwa jinsi tulivyojipanga, tunayo imani kubwa wauaji watapatikana,
tupeni muda kidogo tutawaita na kuwapeni taarifa tukishawatia mbaroni,”
alisema Kamanda Matola.
Aliongeza kwamba kwa sasa maofisa wa polisi wanaendelea kukusanya
taarifa kwa njia za kawaida na pia kupitia mtandao wa simu (cyber),
hivyo hakuna mahali ambako wauaji hao wanaweza kukwepa mkono wa Jeshi
hilo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba kuna watu wamekamatwa wakiwa na baadhi
ya vitu alivyokuwa navyo Kamanda Barlow kabla ya kuuawa, Matola alisema
kwamba ni mapema sana kuzungumzia taarifa hizo, lakini wakati muafaka
ukifika taarifa rasmi zitatolewa.
KUAGWA LEO NYAMAGANA
Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel
Nchimbi, leo anatarajiwa kuongoza wakazi wa mkoa wa Mwanza na mikoa
jirani kuuaga mwili wa Barlow.
Matola alisema jana kuwa zoezi la kuuaga mwili wa Barlow linatarajiwa
kufanyika leo kwenye uwanja wa Nyamagana kuanzia saa 2:30 asubuhi na
kisha jioni marehemu atapelekwa uwanja wa ndege wa Mwanza kupelekwa Dar
es Salaam.
Kwa mujibu wa Matola, mwili wa Kamanda Barlow utafikishiwa nyumbani
kwake Ukonga Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa fursa kwa ndugu, jamaa na
marafiki kumuaga kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani
Kilimanjaro kwa mazishi.
Makamanda wa Polisi kutoka mikoa jirani ya Mara, Kagera, Shinyanga,
Geita, Simiyu na Kanda Maalum ya Tarime na Rorya ni miongoni mwa
wanaotarajiwa kutoa salaam za rambirambi wakati wa kuuaga mwili wa
Kamanda Barlow.
NCHIMBI: TUTAWASAKA KWA NGUVU ZOTE
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema majambazi waliomuua Barlow wataswakwa kwa nguvu zote za dola.
Alionya kuwa majambazi wanaoua raia kwamba serikali itapambana nao kikamilifu.
“Polisi ni walinzi wa raia na mali zao, wanapotokea watu wanaoua kingozi
wa polisi inaleta hofu kwa wananchi, hivyo serikali itapambana nao
kikamilifu,” alisema Dk. Nchimbi, jijini Mwanza jana.
LUKUVI: NI UKATILI USIOVUMILIKA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William
Lukuvi, ambaye jana alifika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza kusaini kitabu cha maombolezo, alizungumzia mauaji ya Kamanda
Barlow na kusema ni ukatili ambao serikali haiwezi kuuvumilia.
“Ni kifo cha ajabu, kimemshtua kila mtu, huu ni ukatili usiovumilika,
lazima wahusika wasakwe na kutiwa mbaroni. Kama watu wanadiriki kumuua
kiongozi wa polisi hii ni hatari sana sijui itakuwaje kwa raia wa
kawaida,” alisema Lukuvi.
Alitoa wito kwa wakazi wa Mwanza kushirikiana na Jeshi la Polisi
kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo wanatiwa mbaroni kwa sababu lazima
watakuwa wanafahamika.
“Wauaji hawakushuka kutoka kusikojulikana, wasingeweza kutekeleza mauaji
hayo bila wananchi kujua chochote, jambo la msingi hapa ni kushirikiana
na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa ambazo zitasaisia wahusika kutiwa
mbaroni,” alisema.
Mbali na Waziri Lukuvi, kiongozi mwingine aliyefika kusaini kitabu cha
maombolezo ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk.
Asha-Rose Migiro ambaye pia alifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji
wafiwa.
MANUMBA AVUTA PUMZI
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, ambaye
alifika jijini hapa juzi kuongeza nguvu ya upelelezi wa mauaji hayo,
alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote, lakini wakati utakapofika
atasema.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote tunaendelea na kazi ya upelelezi wakati
ukifika nitazungumza kwa hiyo tuendelee kuvuta subira,” alisema
Manumba.
TAARIFA YA MAZISHI
Mwili wa Barlow, unatarajiwa kuzikwa keshokutwa mkoani Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na
Msemaji wa Jeshi la Polisi makao Makuu, Advera Senso ilisema: “Kamati ya
mazishi kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi, inapenda kuwataarifu
wananchi wote kuwa mwili wa Kamanda Barlow utaagwa jijini Mwanza kesho
(leo).”
Advera alisema kuwa leo jioni mwili huo unatarajiwa kusafirishwa kwenda
Dar es Salaam, na utawekwa nyumbani kwake Ukonga na kesho utaagwa
nyumbani kwake kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani
Kilimanjaro na kwamba mwili huo utazikwa mkoani humo Jumatano.
Advera aliongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu maziko hayo zitaendelea kutolewa.
CHADEMA YATOA POLE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa masikitiko na kinalaani mauaji ya Kamanda Barlow.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilieleza
kuwa Chadema kinatoa pole kwa familia ya marehemu, Jeshi la Polisi na
wote walioguswa na msiba huo.
“Chadema kinafuatilia taarifa zinazoendelea kutolewa kuhusu utata wa
chanzo cha kifo cha Barlow, hivyo kwa kuzingatia mazingira hayo badala
ya Jeshi la Polisi kutegemewa pekee katika kuchunguza chanzo cha kifo
cha kamanda wao, ni muhimu uchunguzi huru ukafanyika kwa mujibu wa
Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za
Tanzania.
Chadema kinaitaka Serikali kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria hiyo
ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria
kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika
maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi,” ilieleza
sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa wa Habari wa Chadema,
Tumaini Makene.
“Ikumbukwe pia kwamba matukio ya mauaji ya raia katika mikoa ya Mbeya,
Mara, Arusha, Ruvuma na mikoa mingine nchini yameelezwa kwa kina na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama Taifa na wasemaji wengine wa kambi rasmi ya
upinzani inayoongozwa na Chadema wakati wa mkutano wa nne wa Bunge
mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 bila ya hatua
kuchukuliwa.”
Makene alisema Chadema kinatoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya
Serikali na CCM kwa upande mwingine kutumia msiba huu kutafakari na
kuchukua hatua endelevu za kushughulikia mauaji hayo na mengine ya raia
ili kulinda ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi wa raia wote.
Hata hivyo, kifo cha Barlow kimetokea siku moja tu baada ya kutoa kauli
ya kutatanisha juu ya tukio la polisi kummiminia risasi Ofisa Uhamiaji
wa Mkoa wa Mwanza, Albert Buchafwe, kwamba aliingia katika mtego wao na
kwamba ilikuwa auawe kwa kupigwa risasi.
Akizungumza na NIPASHE alhamisi iliyopita Barlow alisema kuwa:" Ni kweli
kuna tukio kama hilo, lakini yalikuwa ni mashambulizi ya gizani kwa
sababu askari walimfananisha ofisa uhamiaji na jamabzi waliyekuwa
wamemuwekea mtego, nadhani ana bahati kwanindiyo akwaida yetu
hutubembelezani na majambazi."
Pamoja na kauli hiyo kamanda huyo hakueleza kwa jinsi gani ofisa huyo
haliingia katika mtego huo kwani hakuwa katika tukio la uporaji.
0 Comments