Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU
*Polisi Yamtuhumu Uamsho, Yatangaza Kuwasaka Wauaji Popote, Vurugu Zaendelea
MACHAFUKO yanayoambatana na ghasia, yamechukua sura
mpya, baada ya askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), CPL
Said Abdulrahman kuuawa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa
kikundi cha Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki).
Tukio hilo limekuja ikiwa ni siku moja baada ya kikundi cha watu hao
kufanya ghasia wakitaka kiongozi wao, Sheikh Farid Hadi Ahmed
aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha arudishwe wakiamini kuwa,
polisi walimteka.
Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa mauaji hayo yalifanyika eneo
la Bububu katika mji wa Unguja Visiwani Zanzibar. Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema Mjini Unguja jana kuwa, askari
aliyeuawa ni mwenye namba F.2105 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
cha Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Wafuasi wa Uamsho wamempiga mapanga kichwani na mikononi wakati
akirudi kutoka kazini saa 6:30 usiku eneo la Bububu. Tuelewe kwamba
aliyeuawa ni askari polisi, ni raia wa Tanzania na ni muumini wa dini ni
lazima tuhakikishe waliofanya unyama huu wanakamatwa,” alisema na
kuongeza:
“Tutawasaka kwa udi na uvumba na kufikishwa mahakamani kwa mauaji na
sheria za nchi zitachukua mkondo wake,” alisisitiza Kamishna huyo.
Vurugu zaendelea
Pamoja na tamko hilo, hadi jana jioni vurugu hizo ziliendelea kwa
vijana hao kuchukua misalaba makaburini, viti na meza na kuviweka
barabarani kisha kuvichoma moto. Mwandishi wa habari hizi na wenzake
kadhaa, walinusurika kuvamiwa na wafuasi wa Uamsho wakati wanatokea eneo
la Kwerekwe, baada ya kundi la watu kuwazunguka na kuziba barabara kwa
magogo, kisha kuchoma matairi ya gari.
“Tumefukuzwa kwa mawe na hao ubayaubaya na nusura niligonge gari.
Jamaa walituzunguka katikati, wametuwekea magogo na huku wametuwashia
matairi ili tusipite. Kidogo leo tufe billahi!” alisema mwandishi huyo.
Kutokana na vurugu hizo, polisi iliwaita viongozi watano wa Uamsho na
kuhojiana nao kuhusu suala hilo, na hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa
na taarifa zaidi kuhusu hali hiyo.
Kutoweka kwa Farid
Akizungumzia tukio la kutoweka kwa kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid
Hadi Ahmed, Kamishna alisema: “Ilikuwa saa 6:30 mchana wa juzi tulipokea
taarifa kutoka kwa Sheikh Msellem Ally kwamba kiongozi mwenzao wa
Jumuiya ya Uamsho ametekwa na haonekani tangu jioni ya Oktoba 16.
“Baada ya taarifa hii, uchunguzi ulianza na mmoja wa watu waliohojiwa
ni Said Omar Said ambaye ni ndugu wa Sheikh Farid ambaye ni dereva na
ndiye aliyekuwa naye walipokwenda katika eneo la Mazizini kununua umeme
kutokana na maelezo ya dereva huyo.”
Kamishna Mussa alisema kwa mujibu wa Said, Sheikh Farid alimwamuru
dereva huyo kwenda nyumbani kupeleka umeme wakati yeye akizungumza na
watu walikuwamo ndani ya gari aina ya Noah ambalo hata hivyo nambari
zake za usajili hazikufahamika. Alisema ilipotimu saa 6:30 mchana juzi
wakati taarifa hizo zinapelekwa kituoni, wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho
walikuwa wanaendelea kujikusanya katika msikiti wa Mbuyuni na kuanzisha
fujo kwa kuwasha moto kwenye jaa lililokuwa karibu na msikiti huo.
“Baadaye fujo hizo zilisambaa katika maeneo mengine ya mjini kwa
kufanyika uharibifu wa mali za Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wananchi
wa kawaida,” alisema.
Alisema katika vurugu hizo watu hao walichoma moto magari kadhaa,
ambapo gari la Serikali lilivunjwa kioo kidogo cha pembeni, gari la
Zimamoto kuvunjwa kioo cha mbele pamoja kuvunja duka la pombe na kuiba
mali zilizokuwamo ndani. Kamishna Mussa alisema, mpaka sasa, watu 10
wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo.
Kauli ya SMZ
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, SMZ, imewataka wananchi kuendelea na
shughuli zao kama kawaida kwa maelezo kuwa vyombo vya ulinzi na usalama
vimeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya Zanzibar. Taarifa ya Serikali
iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed
Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika
hali ya amani na utulivu. Akizungumzia tukio la vurugu zilizotokea
juzi, Aboud alisema kwamba vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni
wafuasi wa Sheikh Farid vilifanya vurugu katika mitaa ya Darajani,
Michenzani, Mwembeladu, Magomeni na Amani wakidai kwamba kiongozi wao
ametekwa.
Alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya dola wakiwamo Polisi,
Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, KMKM, JKU, Chuo cha Mafunzo, Zimamoto na
Valantia na vyote vimeeleza kuwa havielewi chochote kuhusu Sheikh
Farid.
Aboud alisema wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wao,
wananchi wanapaswa kutulia na kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo
vya polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo
yao. Waziri Aboud alisema kuwa Serikali inawasihi wananchi kuacha
kujiingiza katika fujo na vurugu kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu
wa sheria na Serikali haitavumilia vitendo hivyo.
CCM, CUF walaani
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa CCM, wamelaani ghasia
zilizofanywa na kikundi cha Uamsho katika mitaa mbalimbali juzi.
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa CCM kwenye Ukumbi wa Baraza hilo
lililopo Bweni, Hamza Hassan Juma alisema wakati umefika kwa hatua
kali za kisheria kuchukuliwa kabla ya hali haijawa mbaya zaidi.
“Isifike mahali Zanzibar ikageuka taifa la machafuko na kuwafanya
wananchi kushindwa kuishi kwa amani,” alisema huku akimtaka Mkuu wa
Polisi, IGP Said Mwema kusimama kidete kumaliza hali hiyo. Wawakilishi
hao wa CCM, waliitaka Serikali kuwalipa fidia wote walioathirika na
ghasia hizo na vikosi vya usalama SMZ kusaidia kuweka ulinzi wakati
wote katika mji wa Zanzibar.
Juma alifika mbali zaidi na kusema kuwa, Jumiki si chama cha siasa,
hivyo kuiomba Serikali kuifuta kwa maelezo kwamba imekosa mwelekeo kwa
kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani. Wajumbe hao waligoma kuingia
Barazani jana ikiwa ishara ya kuonyesha msimamo wao kulaani hali hiyo.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi CUF kimeelezea kusikitishwa na
matukio ya vurugu Visiwani Zanzibar.
“Kutokana na vitendo hivyo, Chama cha Wananchi kinalaani kwa nguvu
zote matukio hayo ambayo yamesababisha uvunjifu wa amani, na
kusababisha hofu na taharuki kwa raia pamoja na wageni wanaotembelea
Zanzibar”, ilisema taarifa ya CUF iliyotolewa Zanzibar jana.
CUF katika taarifa hiyo, pia walieleza kushtushwa na habari za
kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed katika mazingira ya kutatanisha,
hivyo kuitaka SMZ kuzidisha juhudi za kumtafuta. Kwa upande mwingine,
CUF inawataka wanachama wake, wapenzi na wananchi wote kutojiingiza na
kutofanya vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani ya
nchi yetu.
0 Comments