Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka
Na Richard Makore
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, ameibuka na kusema yupo tayari kueleza
yaliyompata ikiwa serikali itaunda chombo huru kwa ajili ya kuchunguza
sakata hilo.
Kwa mara ya kwanza jana, Dk. Ulimboka alitoa tamko lilisosainiwa na
wakili wake, Rugemeleza Albert Nshala na kusomwa na wakili Nyaronyo
Kicheere, jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.
Dk. Ulimboka mwishoni mwa Juni, mwaka huu, alitekwa na watu
wasiofahamika katika barabara ya Tunisia, wilayani Kinondoni na kupigwa,
kung’olewa meno na kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje ya Jiji la
Dar es Salaam.
Hata hivyo, jana waandishi wa habari walishikwa na butwaa baada ya kuona
tamko hilo zito likisomwa na Wakili Kicheere badala ya Dk. Ulimboka
mwenyewe kama watu wengi walivyotarajia.
Wakili Kicheere aliwaambia waandishi wa habari kwamba Dk. Ulimboka,
alishindwa kufika mbele yao na kusoma tamko hilo kwa kuwa yupo nje ya
nchi kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Hata hivyo, Kicheere hakutaja nchi ambayo Dk. Ulimboka amekwenda kuchunguzwa afya wala siku aliyoondoka.
Katika tamko hilo, Dk. Ulimboka alisema yupo tayari kutoa ushirikiano
kwa vyombo huru na makini vitakavyoundwa na serikali ili aeleze ukweli
wa kilichompata.
Katika tamko lake hilo, Dk. Ulimboka alisema ametafakari sana na kuona
kwamba kama hatatoa tamko hilo, atakuwa hajawatendea haki Watanzania
wenzake kwa kuwa walihusika katika kumuombea kwa Mwenyezi Mungu
alipokuwa anaumwa.
Alisema kuwa mambo mengi yaliyoelezwa na vyombo vingi vya habari hasa
magazeti, yalikuwa yana ukweli ndani yake likiwamo lile la MwanaHalisi
lililofungiwa na Serikali Julai 30, mwaka huu.
Aliongeza kuwa kabla ya kutoa tamko hilo, alijiuliza maswali mengi
ambayo yalikosa majibu na kati ya mambo aliyojiuliza, ni jukumu la nani
atakayehakikisha haki inatendeka katika nchi ya Tanzania.
“Ni jukumu la asasi za kiraia ama mhusika mwenyewe, kuelezea kinagaubaga
kilichompata na baada ya kukosa majibu nikaona ni vyema niwaeleze
Watanzania hali halisi,” alisema.
Alieleza kuwa kabla ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika msitu wa
Mabwepande, alikuwa na kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake kwamba
anatokea Ikulu.
Alimtaja mtu huyo kuwa ni Ramadhan Abeid Ighondu, ambaye alitambulishwa
kwake kama ofisa anayetoka Ikulu kwa kuwa alikuwa anakutana naye mara
kwa mara kabla ya tukio hilo la kutekwa na kupigwa.
Sehemu ya tamko hilo lilisema Ighondu alitambulishwa kwake na kigogo
mmoja ambaye hakumtaja jina akiwa na wenzake ambao ni madaktari.
Dk. Ulimboka alisema walijulishwa kwamba hoja na madai mbalimbali ya
madaktari, yatakuwa yanachukuliwa na Ighondu na kuyapeleka serikalini
kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa kupandishiwa nyongeza za mishahara na
madai mengine.
Alisema siku hiyo aliyotekwa, alipigiwa simu na Ighondu kupitia simu ya
mkononi namba 0713 760473 na kwamba anamtambua Ighondu kwa sura.
Aliongeza kuwa katika mawasiliano hayo, yeye (Dk. Ulimboka), alikuwa
akitumia simu namba 0713 731610 na kwamba anaamini ofisa huyo wa Ikulu
yupo hai na yupo tayari na wenzake kutoa ushahidi.
Aidha, Dk. Ulimboka alisema kwa nyakati tofauti, ofisa huyo alitumwa
kwake na kumtaka ampatie nyaraka mbalimbali vikiwamo vyeti vya elimu kwa
ajili ya uthibitisho wa taaluma yake.
“Mimi Dk. Ulimboka nina haki ya kuishi kwa mujibu wa ibara ya 14 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wenzangu wana
haki ya kuulinda uhai wangu,” alisema.
“Je; uhai na maisha yangu vina thamani ndogo kama ya mnyama anayekwenda
machinjioni? Je, serikali itakubali lini kuunda tume huru kuchunguza
tukio hili?,” Alihoji.
Aliwataka madaktari kutovunjika moyo katika kudai haki zao za msingi na kwamba yupo pamoja nao katika harakati hizo.
Juni 26, mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa, akapigwa, akang'olewa kucha
kabla ya kuokotwa msitu wa Mabwepande na kupelekwa katika Taasisi ya
Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) kwa matibabu.
Hata hivyo, baadaye alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Dk. Ulimboka alirejea nchini Agosti 12, mwaka huu.
Tangu hapo, hajawahi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na sakata zima la kutekwa kwake hadi alipotoa tamko hilo jana.
0 Comments